Monday, 12 August 2013

Sheikh Ponda awekwa chini ya ulinzi Muhimbili


Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania Sheikh Ponda Issa Ponda akiwa amelazwa kwenye chumba maalumu katika taasisi ya mifupa Muhimbili (MOI), muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini hapojana. Picha na Venance Nestory 
Dar es Salaam/Moro. Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda yupo chini ya ulinzi huku akitibiwa majeraha katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Sheikh Ponda alisafirishwa usiku wa manane kutoka Morogoro baada ya juzi kupigwa na kitu kinachodaiwa kuwa ni mtutu wa bomu saa 12:25 jioni alipokuwa akisindikizwa na wafuasi wake kwenda katika Msikiti wa Mungu Mmoja Dini Moja mara baada ya kumaliza kutoa mhadhara katika kongamano mjini hapo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kongamano hilo, Sheikh Idd Mussa Msema, alidai kuwa Sheikh Ponda alipigwa risasi tatu begani.
Taarifa kutoka ndani ya familia ya Ponda zilisema kwamba baada ya kupata taarifa za kupigwa risasi, baadhi ya masheikh walifunga safari kwenda Morogoro na kumrejesha Dar es Salaam usiku huohuo. Kabla ya kurudishwa Dar es Salaam, imeelezwa kuwa Sheikh Ponda alipelekwa katika Zahanati ya Islamic Foundation.
Mmoja wa wanafamilia alidokeza kwamba Sheikh Ponda alifichwa na alikuwa chini ya ulinzi mkali wa wafuasi wake na hakuna aliyeruhusiwa kumsogelea.
Muhimbili
Hata hivyo, habari zilizopatikana baadaye jana zilisema kuwa alifikishwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Sheikh Ponda alifikishwa Muhimbili jana saa 7:18 mchana na alipelekwa kwenye chumba cha wagonjwa wa dharura na baadaye alitolewa na kupelekwa kwenye chumba cha x-ray kwa ajili ya vipimo. Baadaye alipelekwa chumba cha upasuaji.
Eneo kubwa la hospitali hiyo lilikuwa na idadi kubwa ya askari na mmoja wa askari waliokuwa doria hospitalini hapo alisema walitawanywa kwenye hospitali mbalimbali za Dar es Salaam baada ya kupata taarifa kuwa angeletwa kwa matibabu.
“Nakuambia tuko hapa tangu saa kumi na moja asubuhi, tumetawanywa hospitali mbalimbali baada ya kupata taarifa kuwa analetwa Dar. Bahati nzuri kaletwa hapa Muhimbili... tunasubiri apate matibabu na tutamtia mbaroni,” alisema askari huyo.
Taarifa ya polisi
Msemaji wa Polisi, Advera Senso alisema jana katika taarifa yake kuwa Sheikh Ponda yuko Hospitali ya Muhimbili akitibiwa baada ya kupata majeraha yaliyotokana na purukushani na polisi wakati wafuasi wake walipokuwa wanataka kumtorosha.

mwananchi

No comments:

Post a Comment