Na Hans Mloli


KIUNGO wa zamani wa Klabu ya Yanga SC, Credo Mwaipopo, baada ya kukaa kimya kwa muda, ameibukia katika timu ya Friends Rangers inayoshiriki michuano ya Ligi Daraja la Kwanza.
Championi Jumatano lilimshuhudia kiungo huyo aliyewahi pia kuichezea Panellenois ya nchini Sweden, akiichezea timu hiyo yenye maskani yake maeneo ya Manzese dhidi ya Villa Squad ya Magomeni, mechi ilipigwa kwenye Uwanja wa Karume uliopo Ilala ambapo Friends ilishinda 2-1.
Akizungumza na gazeti hili mara baada ya kumalizika kwa mechi hiyo, Credo alisema kuwa kwa sasa amesaini kuichezea timu yake hiyo ya awali kutokana na kusubiri kukamilika kwa mipango yake ya kwenda kukipiga kwenye klabu moja iliyopo nchini Sweden.
Alisema kuwa anashindwa kabisa kukaa bila kucheza mpira wa ushindani, ndiyo maana akajiunga na timu hiyo kwa sasa ambayo hajasaini kuitumikia kwa miaka bali ni fomu inayomuonyesha kuwa kwa sasa anamilikiwa na timu fulani.
“Nimerudi kwenye timu yangu ya nyumbani kwa muda nikisubiri mipango yangu ya kurudi Sweden ikamilike, kuna hatua nzuri, kwa hiyo mipango itakapokamilika muda wowote nitaondoka.
“Naweza kuondoka muda wowote kama nikipata timu nje ya nchi lakini kama nikipata Tanzania lazima Friends izungumze na hiyo timu kutokana na fomu niliyosaini ambayo inanionyesha kuwa ninamilikiwa na Friends kwa sasa msimu wote huu,” alisema mchezaji huyo ambaye msimu uliopita alikuwa akiichezea JKT Ruvu.

Gpl