Sunday 20 October 2013

Ufoo Saro aelezea kilichotokea kabla na baada ya kupigwa risasi

MWANDISHI wa Kituo cha Televisheni cha ITV, Ufoo Saro ambaye hivi karibuni alikumbwa na madhila ya kupigwa risasi na kujeruhiwa vibaya na mzazi mwenzie, ameanza kufunguka kidogo kidogo na kueleza kwa kina jinsi tukio zima lilivyotokea.

Akizungumza kwa sauti ndogo na taratibu na gazeti hili kando ya kitanda alicholazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, mwanahabari huyo alieleza kushangazwa na ujasiri na nguvu za aina yake ambazo zilimwezesha kutambaa na kujiburuza hadi eneo la karibu ya barabara ili kuomba msaada wa kukimbizwa hospitali.

Ufoo ambaye alionyesha dhahiri kutofurahishwa na baadhi ya taarifa zinazozingira tukio lake, alisema tayari alikuwa amewahakikishia polisi waliofika kumjulia hali hospitalini hapo kwamba alikuwa akisubiri afya yake iimarike kabla hajaeleza kwa kina kila anachokijua kuhusiana na tukio hilo.

“Alifika hapa kunijulia hali na kuangalia maendeleo yangu afande Msangi na nikasema nitakuwa tayari kueleza kila ninachokijua baada ya afya yangu kuimarika. Nasikitika kuna watu wanasema mambo wakifikia hatua ya kutaka kuonekana wananifahamu vizuri kuliko hata ninavyojifahamu mwenyewe,” alisema akionyesha kutofurahishwa na baadhi ya taarifa zinazoripotiwa kuhusu sakata lake.


Ufoo ambaye alifikishwa hospitalini hapo Jumapili ya wiki iliyopita kutokana na kujeruhiwa kwa risasi na mwanaume aliyezaa naye mtoto mmoja alisema anamshukuru sana Mungu kwa uzima alionao sambamba na kuelezwa kupata faraja kubwa na kutiwa moyo na mwajiri wake, ndugu, jamaa na marafiki.

Mwanahabari huyo ambaye bado yuko chini ya uangalizi wa karibu wa madaktari baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa risasi mwilini mwake siku chache zilizopita, amelazwa katika chumba cha peke yake ambacho ingawa kina seti ya televisheni alisema alikuwa haruhusiwi kuiangalia kwa ushauri na maelekezo ya madaktari.

Huku akionekana wa chini ya uangalizi mwingine wa karibu na wa kudumu wa muuguzi ambaye muda wote wa mazungumzo haya alionekana kuwapo katika chumba hicho, Ufoo alisema alikuwa ana mapenzi makubwa kwa mzazi mwenzake huyo ambaye alipoteza maisha katika tukio hilo.

“Nilimpenda sana Antheri. Alikuwa kijana mtaratibu na mpole sana. Najua kile kilichotokea ni shetani tu na binafsi nilishasamehe alfajiri ile ile baada ya tukio lile,” alieleza Ufoo ambaye pia alimpoteza mama yake mzazi katika mkasa huo.

TUKIO ZIMA LILIVYOTOKEA

Ufoo ambaye mara kadhaa katika mazungumzo na gazeti hili alionekana kukunja uso akiashiria kupata maumivu, alionyesha eneo la chini ya bega katika mkono wake wa kulia lililofungwa na bandeji ambalo alisema ndipo alipopigwa risasi ya kwanza wakati akigeuka na kujaribu kuepuka mauti muda mfupi baada ya Antheri kumfyatulia risasi zilizomkuta mama yake mzazi.

Akijaribu kuvuta kumbukumbu ya tukio lilivyoanza, Ufoo alisema mzazi mwenzake huyo alifika nyumbani kwake akitokea Sudan alikokuwa akifanya kazi usiku huo huo wa tukio na akamtaka kwenda kwa mama yake (Ufoo) eneo la Kibamba, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Kabla ya kufika Kibamba na kwa sababu ambazo Ufoo hakuzieleza, alimkariri mzazi mwenzake huyo akisema alikuwa amefikia uamuzi wa kujiua yeye na mtoto wao.

“Hata sijui ni nini kilitokea. Wakati tukitoka nyumbani Antheri alianza kwa kuniambia kwamba alikuwa amepanga kujiua yeye na mtoto wetu,” alisema Ufoo kabla ya kukaa kimya kwa sekunde kadhaa na kuendelea na simulizi yake ya kusikitisha.

Akiwa na sura ya ujasiri, Ufoo anasema pamoja na kumwambia maneno hayo bado Mushi alimsisitiza kwamba waende kwa mama yake (Ufoo) baadae warudi kumchukua mtoto wao japo Ufoo hakusema walitaka kwenda wapi baada ya hapo.

Alisema walipofika nyumbani kwa mama yake walikwenda moja kwa moja sebuleni na wakiwa wamekaa kwenye makochi baada ya salamu za hapa na pale ghafla Mushi akasimama akamwambia mama yake Ufoo kwamba; “Mama nimeishafanya maamuzi”

Kwa mujibu wa maelezo ya Ufoo, baada ya Mushi kutamka maneno hayo ghafla akaingiza mkono nyuma ya suruali alikokuwa ameweka bastola yake na kisha akaichomoa.

Katika maelezo yake Ufoo alisema baada ya kuichomoa bastola hiyo mama yake naye alisimama na kwenda kujaribu kumpokonya, kitendo hicho kilimfanya amiminiwe risasi mfululizo.

Alisema kuona hivyo aliamua kukimbia kuelekea jikoni ambapo Mushi alimuona na kuanza kumiminia risasi ambayo moja ilimpata eneo la mkono wa kulia ambayo ilitokezea mbele na kuchana titi la kulia.

Kwa mujibu wa Ufoo jeraha hilo halikumfanya akate tamaa ya kunusuru maisha yake kwani alijaribu kukimbia ingawa Antheri alifyatua risasi nyingine kadhaa ambazo zilimpata juu kidogo ya mgongo na kutokea tumboni ambazo zilisababisha aanguke chini

Akiendelea kusimulia, anasema ingawa alikuwa akivuja damu nyingi, na huku akijiburuza ardhini, Ufoo alisema wakati akitambaa aligeuka nyuma na akamuona Antheri akijielekeza bastola eneo la kidevu na alipofyatua risasi alianguka chini.

“Nikiwa chini nilimuona Antheri akijipiga risasi kidevuni na akaanguka chini, sikujua kilichofuata baada ya hapo kwani niliendelea kujiburuza ili kuokoa maisha yangu,” alisema Ufoo

ALIVYOJIOKOA

“Nyumbani kwetu, pale Kibamba si mbali sana na barabarani, wakati nikikaribia kufika barabarani wakati huo nikitokwa na damu nyingi huku nikihisi tumbo langu limejaa sana nilikutana na dada mmoja ambaye nilimuomba khanga ili nijifunge kuzuia damu zisitoke kwa wingi”.

Anasema dada yule alimpa khanga akajifunga na aliposogea barabarani alikutana na gari lililokuwa likiendeshwa na mwanamke mmoja.

“Nilipoona kuna gari linapita nikainuka kuomba msaada. Liliposimama nilimuona mwanamke akiendesha nikamweleza kwamba nilikuwa nimepigwa risasi na nilikuwa nikiomba msaada wake anikimbize hadi katika hospitali ya Tumbi na kwamba akifika pale tu aniache mlangoni.

“Si rahisi kuamini, yule mama alikataa kunisaidia akisema alikuwa akiwahi sehemu kumchukua mzazi. Sina la kusema niliamua kumsamehe tu yule mama ingawa niliumia sana,” alisema Ufoo.

Alisema muda mfupi tu baadaye alitokea kijana aliyekuwa na pikipiki, maarufu kwa jina la bodaboda ambaye alimuomba msaada wa kumkimbiza hospitali ya Tumbi na akakubali.

“Yule kijana aliniuliza iwapo nilikuwa ninao uwezo wa kujishikilia vizuri na niliposema nitaweza akanisaidia kupanda katika bodaboda.

“Wakati huo nilikuwa naona kama tumbo linazidi kujaa. Nikiwa kwenye pikipiki kuna wakati nilikuwa nikihisi kwamba naweza nikaishiwa nguvu na kuanguka katika barabara na kisha kupitiwa na gari na kupoteza maisha. Lakini nilipata ujasiri na kujishikilia,” alieleza kwa sauti ya chini.

Alisema anakumbuka wakati walipofika eneo la Kibaha ilipo mizani ya kupima uzito wa magari makubwa walikuta barabara ikiwa imejaa magari na yeye alimuomba dereva huyo wa bodaboda kupita hata nje ya barabara eneo la nyasi ili kumwahisha hospitalini jambo ambalo kijana yule alilifanya.

“Nilipofika eneo la mapokezi pale Tumbi nilimueleza muuguzi niliyemkuta kwamba nilikuwa nimejeruhiwa kwa risasi na nikamuomba asaidie kuokoa maisha yangu. Yule nesi alisita akitaka kwanza kupata kibali cha polisi (PF3) lakini nikaumuomba apigiwe simu, Kaimu Mganga Mkuu wa Tumbi, Dk. Dattan ambaye tunafahamiana”

“Baada ya muda mfupi Dk. Dattan alifika na nikamweleza yaliyonipata na mara moja nikaanza kuhudumiwa kwa kuniwekea dripu, na nikamsikia akiwaeleza wauguzi kwamba isingekuwa busara kwa hali niliyonayo kama wangeanza kuchukua picha za X-ray kwani hatua hizo zingeweza kusababisha kupoteza maisha,” alieleza akikumbuka yaliyojiri hapo Tumbi.

Kwa mujibu wa Ufoo, akiwa bado ana fahamu alimsikia daktari aliyekuwa akimhudumia akiomba msaada wa gari la kubeba wagonjwa ili limchukue na kumkimbiza katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wito ambao ulijibiwa kwa maelezo kwamba lilikuwa halina mafuta.

Majibu hayo kwa mujibu wa Ufoo, yalisababisha daktari huyo aombe kuletewa gari la wagonjwa la wagonjwa maarufu (VIP) ambalo lililitwa na muda mfupi baadaye akapakizwa tayari kwa safari ya kukimbizwa Muhimbili.

Alisema wakati akikimbizwa Muhimbili anakumbuka namna alivyokuwa akipatwa na maumivu makali wakati wote gari ile ya wagonjwa ilipokuwa ikipanda matuta ya barabarani na kuna nyakati alikuwa akihisi kupoteza pumzi na kuishiwa nguvu.
MTANZANIA

No comments:

Post a Comment