Wednesday 1 February 2012

ICTR yawaombea hifadhi walioachiwa huru


 31 Januari, 2012 - Saa 18:46 GMT

ICTR
Majaji katika mahakama ya ICTR
Mahakama inayoendesha kesi za mauaji ya kimbari yaliyotokea Rwanda mwaka 1994 imetoa wito kwa mataifa kutoa hifadhi kwa wale walioondolewa mashtaka.
Watu 5 kati ya watu 10 walioondolewa lawama za kuhusishwa katika mauaji hayo wanasema hawawezi kurejea nchini Rwanda.
Wanaishi chini ya ulinzi wa Polisi katika nyumba moja mjini Arusha, Tanzania, ambako ndiko makao ya mahakama hiyo ya ICTR.
Mahakama hiyo ya ICTR inatarajiwa kufunga mwishoni mwa mwaka huu.
Watu 800,000 kutoka jamii ya waTutsis na waHutus wenye msimamo wa kadiri waliuwawa katika kipindi cha siku 100 nchini Rwanda mwaka 1994.
Msemaji wa ICTR Roland Amoussouga ameambia BBC kupatikana nchi za kuwahifadhi wale ambao hawakupatikana na hatia ndio changamoto kuu inayokabili mahakama.
"Ni mzigo mkubwa kwetu kuendelea kuwahifadhi watu hawa walioachiwa huru kwa muda wa miaka mingi hivi, na tumeshirikiana nao, pamoja na mawakili wao kutafuta nchi ambako wanaweza kupelekwa. Hadi sasa hatujafanikiwa," alisema.
Wote 5 walioko mjini Arusha ni kutoka kabila la waHutu na miongoni mwao ni afisa wa zamani wa jeshi wa cheo cha Brigadier generali, mawaziri wa zamani na mfanya biashara mmoja.
Wanaishi pamoja katika nyumba inayolindwa, wanaweza kwenda mjini na kanisani, lakini hawawezi kuondoka huko.
Waziri wa zamani wa uchukuzi Andre Ntagerura amekuwa akisubiri kupata hifadhi kwa kipindi cha miaka 6 tangu mashtaka dhidi yake yalipoondolewa.
Wengine wawili wameshatumika vifungo vyao lakini hawana pa kwenda.
Wote wana familia nchini Ubelgiji, Canada na Ufaransa lakini hadi sasa hawawezi kupewa vibali kujiunga na familia zao, licha ya maombi kutoka baraza la usalama la umoja wa mataifa.

bbcswahili

No comments:

Post a Comment