Monday 13 February 2012

WARAKA KWA RAIS JAKAYA KIKWETE

 
 
Na Manyerere Jackton
Mpendwa Rais, ni muda mrefu umepita tangu nilipokuandikia waraka. Mara ya mwisho nilikuandikia nikikuomba “uwe mkali kidogo.”
Maudhui yangu kwa wakati huo, yalikuwa kwamba kuona unakuwa mkali ili mambo yaweze kusonga mbele. Nakumbuka sana wakati wa kampeni ulivyokuwa ukionyesha kukerwa na mambo mengi, na ukaahidi kutumia uzoefu wako ulioupata ndani na nje ya nchi, kusaidia kuboresha mambo.
Mheshimiwa Rais, wananchi wanalalamika kuwa hali ya maisha ni ngumu. Kwa upande mmoja nakubaliana nao, lakini kwa upande mwingine napingana nao. Nakubaliana nao kwa sababu bei za vitu zinazidi kupaa, ilhali kipato kikiendelea kuwa kile kile. Kwa watumishi wengi wa umma, hali imeanza kuwa mbaya. Heshima imeanza kurejea kwa wafanyabiashara-fedha zinahifadhiwa katika soksi.
Nakubaliana na wanaosema hali ni ngumu kwa sababu sasa wananchi wanalazimika kusomesha watoto na hata ndugu zao yatima kwa gharama kubwa mno. Wanaopenda elimu wanashangaa kuona kwenye maji kunawekwa EWURA ili idhibiti bei, hata kama si wote tunaopata maji ya mamlaka husika, lakini kwenye elimu ambayo ni hitaji la msingi, hakuna “EWURA”. Gharama za kusomesha zimekuwa kubwa mno. Watoto wanaosoma katika sekondari za kata wanataabika kweli kweli. Uliahidi kushughulikia suala hili la ada, lakini umekaa kimya kana kwamba si wewe uliyelisema.
Pili, napingana na wanaosema kuwa maisha ya sasa ni magumu kwa sababu naamini maisha hayajawahi kuwa mepesi. Maisha ni mapambano. Anayepambana kwa haki, hupata. Hata wanaopambana kwa hila, wanapata. Sasa tunao majizi wengi wanaofaidi rasilimali za nchi. Wanatajirika na kutaka wanaonekane kuwa wametajirika kwa juhudi halali. Pamoja na yote, ukweli unabaki kuwa kujibidisha ndiyo njia sahihi ya mtu kufanikiwa katika maisha. Waswahili walisema mgaagaa na upwa hali wali mkavu. Hata mimi na wenzangu tumethubutu kuanzisha gazeti hili ingawa wapuuzi wachache wanasambaza sumu kuwa ni la wagombea urais. Siku hizi kuna sifa nyingine ya ziada ya kumtambua Mtanzania! Ukiona mtu anataka uendelee kuwa katika hali duni, basi ujue huyo ni Mtanzania! Ukifanya juhudi za kujikwamua, kosa. Utazuliwa kila jambo baya.
Mheshimiwa Rais, upole wako unawatia shaka wananchi. Unatukatisha tamaa wale tuliokuamini na kusimama kidete kukuunga mkono. Bila shaka unao washauri. Wananchi wameanza kujiuliza maswali mengi. Wanasema inawezekana hao washauri ulionao si washauri wa kukufaa maana kuna mambo ya wazi ambayo ulipaswa uyashughulikie, lakini hakuna kinachoonekana. Wanasema hata Usalama wa Taifa sasa amekuwa ni wa kulinda, na si kunusa na kukupatia taarifa za kiintelejensia. Pili, wanasema inawezekana washauri wako wanakupa yale unayotaka kuyasikia ili ufurahi, basi. Tatu, wanasema inawezekana wewe mwenyewe ukawa ni mbishi usiyetaka kupokea ushauri, na hata ukiupokea, huufanyii kazi. Walau hili la ubishi naweza kulitilia shaka.
Nne, wanasema wewe ni mtu usiyetaka lawama hata kidogo. Wanasema una utaratibu wa kutaka “mambo yajimalize yenyewe”. Wanasema una utaratibu wa kujiweka kando na mambo mengi, makubwa na mazito kitaifa, kana kwamba nawe unaamini kuwa zaidi yako na Mungu, kuna kiongozi mwingine mkubwa kuliko wewe katika taifa hili. Wanasema marais wengine unaowasikia-Rais wa TFF, Rais wa Chama cha Ngumi, Rais wa Masharobalo, Rais wa Mashabiki wa Arsenal, na kadhalika-si wenzako. Wewe uko juu ya wote. Usitarajie kuwa ni wasaidizi wako!
Wananchi wanatoa mfano wa karibuni kabisa wa mgomo wa madaktari. Wanashangaa kuona mgomo huo umedumu kwa zaidi ya nusu mwezi wewe ukiwa kimya. Unakwenda ughaibuni ilhali wapigakura wako wakikata robo kwa kukosa matibabu. Waziri Mkuu alitoa kauli ambayo wanaamini ulimtuma. Kauli ya kuwatisha madaktari kuwa wangefukuzwa kazi endapo wasingerejea kazini. Ulifanya hivyo eti kupima upepo. Ulipoona upepo umekuwa mkali, ukaendeleza ukimya kabla ya kumtumia tena Waziri Mkuu kupooza mambo. Sasa madaktari mnawatekelezea matakwao yao, je, hao waliokufa kwa uzembe wa Serikali, utawapa kifuta machozi?
Mheshimiwa Rais, wananchi bado wanakumbuka namna ulivyokaa kimya wakati misuguano mikali ikiendelea ndani ya Serikali na Chama Cha Mapinduzi. Leo suala la kujivua gamba limekuwa kama tukio la kiimani la kurejea kwa yule tunayembiwa kuwa atarejea wakati wowote. Tukiuliza lini anarejea, tunapozwa kwa kuambiwa kuwa kwake yeye miaka elfu moja ni sawa na siku moja! Wewe ndiye Mwenyekiti wa CCM, bila shaka ukiamua jambo fulani limalizwe ndani ya chama, litamalizwa tu. Lazima tuwe na utaratibu wa kumaliza mambo ili tuweze kuendelea na mengine yenye tija kwa taifa, hasa masuala ya uchumi.
Mheshimiwa Rais, wananchi wanajua namna ulivyo na moyo wa huruma na upendo kwa watu wako. Wakati fulani Sinza tulifungiwa barabara karibu saa nzima, baadaye tukaambiwa kuwa ulikuwa ukienda kuhani msiba wa ndugu wa mmoja wa wasaidizi wako. Kwa siku za karibuni katika jiji la Dar es Salaam na miji mingine nchini umeshiriki sana kuhani na hata mazishi ya wapendwa wetu wengi. Umewajulia hali wagonjwa hopitalini na hata nyumbani. Bila shaka hata kama ningekuwa mimi, kitendo cha kutembelewa na Rais wa nchi nyumbani au hospitalini ni cha kufurahisha na kunitia moyo. Naweza kukiongeza kwenye “CV” yangu!
Lakini, Mheshimiwa Rais, wananchi huku mitaani wanasema umezidisha. Wanasema si lazima kila msiba uhudhurie, na wala si kila mgonjwa lazima umjulie hali wewe mwenyewe kwa kufika. Wanasema kama ungeweza, basi ungekuwa ukiwatuma wawakilishi wako, na kwa kweli kwenye msiba zikitolewa salaamu na ubani kutoka kwa Mheshimiwa Rais, naamini kila mmoja atasisimkwa na kuguswa na upendo wa kiongozi wetu mkuu. Mgonjwa anapokuwa hospitalini, akapata salaamu rasmi kutoka kwa Rais, atafarijika. Hawezi kuzikataa eti kwa sababu Rais kamtuma mwakilishi. Wanasema, ingawa watu wote ni sawa mbele ya Mungu, bado kuna ukweli kwamba akiugua jenerali, waziri, katibu mkuu, ni tofauti na atakavyougua mtendaji wa kitongoji, mjumbe wa nyumba kumi, mwana muziki wa Bongo Fleva mchuuzi au mwandishi wa habari wa aina yangu!
Hili jambo linazungumzwa sana jijini Dar es Salaam. Sijui ni kwa sababu gani, lakini unaweza kuamini kuwa Dar es Salaam wanalalamika kwa sababu mara nyingi wamezuiwa kwenye foleni kwa sababu, ama Rais anakwenda kuhani msiba, au anatoka kumjulia hali mgonjwa hospitalini. Mheshimiwa Rais, haya maneno yanazungumzwa sana. Inawezekana ukawa umeyapata. Kama hayajakufikia, basi naomba kupitia waraka huu, ujue hizi ndizo hisia za watu. Wanataka kuona ukishughulika zaidi na kero zinazowakabili. Kero zinazohusu taifa zima lenye watu zaidi ya milioni 40, na si kwenda huku na kule kwa mambo binafsi.
Mheshimiwa Rais, huku mitaani wanasema kwamba umeshindwa kuboresha uchumi kwa sababu wewe ukiwa kiongozi mkuu, umeacha mambo yajiendeshe yenyewe. Ni kama umeridhika. Umeshindwa kuwakemea waziwazi viongozi wanaopoteza muda kujadili mambo yasiyokuwa na tija, na umeendelea kuwalea wanaonekana kuwa ni mzigo.
Kwa mfano, wanajiuliza, iweje Waziri aliye katika Baraza lako la Mawaziri, awe na ugomvi hadharani na mawaziri wenzake? Iweje waziri mmoja asimame na kuitaka Serikali iwaombe radhi wananchi kwa ukosefu wa umeme na huduma nyingine za kijamii? Je, huyu anakuwa wapi wakati Baraza la Mawaziri linapokutana kujadili mambo yanayolihusu taifa? Wanajiuliza, iweje waziri awe mgonjwa, Waziri Mkuu aulizwe, na yeye ajibu kuwa mwenye haki ya kueleza ugonjwa unaomsibu ni waziri mwenyewe, lakini ajitokeze waziri mwingine na kusema ni lazima Serikali isema huyo waziri mwenzao anaumwa nini? Hivi ni haki kweli kwa Serikali yako kubebeshwa mzigo wa kuzungumzia ugonjwa wa waziri, tena ugonjwa ambao si wa ajali? Je, tuna hakika kuwa waziri huyo ugonjwa wake unatokana na majukumu yake ya kitaifa, na si mambo mengine binafsi? Kweli ugonjwa wa waziri unaweza kuwa mjadala wa kitaifa hadi wananchi washindwe kufanya mambo mengine ya kimaendeleo? Kwanini afya ya waziri itutatize kana kwamba anayeumwa ni rais wa nchi? Kama ugonjwa wa waziri tu, Serikali inalazimishwa iutangaze, rais akiugua, ugonjwa unaomsumbua utangazwe na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa?
Mheshimiwa Rais, wananchi wengi wanaamini kuwa kuyumba kwa mambo kunatokana na wewe mwenyewe. Wanatoa mfano kuwa ili mabehewa yaweze kusafiri, ni lazima injini iwe inafanya kazi, na tena iwe inavuta mabehewa yasiyo na matatizo ya kiufundi. Injini ikiwa na kushkeli, mabehewa hayawezi kutekeleza wajibu wake. Injini ikiwa nzuri, lakini mabehewa yakawa na matatizo ya magurudumu au ya kiufundi, safari haipo. Dawa yake ni kuyaondoa na kuweka yaliyo salama. Katika hili, wewe unachukuliwa kuwa ni injini, hivyo una wajibu wa kuwaonyesha njia viongozi walio nyuma yako. Lakini kama wewe mwenyewe huwafanyi walio nyuma yako wafanye kazi, kwanini wabebeshwe lawama?
Mheshimiwa Rais, leo naomba niishie hapa. Nitaendelea na waraka huu wiki ijayo. Ninayasema haya kwa nia njema ili ikiwezekana, yakusaidie katika kutekeleza dhima yako kubwa uliyoaminiwa na kukabidhiwa na Watanzania.
 
Manyerere J. N

No comments:

Post a Comment