Tuesday 23 April 2013

Wa Maasai watetea ardhi yao Tanzania



Katika kijiji kimoja Kaskazini mwa Tanzania, ndege aina ya Boeing 747 zinatua kwenye kiwanja binafsi, magari yenye nambari za usajili za milki za kiarabu, zikiendeshwa katika eneo hilo na yeyote mwenye simu ya mkononi anapotua hapo hupokea ujumbe ambao haukutarajiwa:
Kwa karne nyingi, (Savanna) katika eneo la Arusha lilikuwa makao kwa watu wa jamii ya wamaasai lakini siku hizi mtu sasa anaweza kudhania yuko Dubai moja ya nchi za milki za kiarabu.''Hujambo mgeni na karibu UAE.''
Hii ni kwa sababu sehemu kubwa ya ardhi mjini Arusha hasa katika eneo la Loliondo karibu na mbuga ya kitaifa ya wanyama ya Serengeti imekodishwa kwa kampuni ya uwindaji ya Emirati iitwayo Ortello
Tangu mwaka 1992, kampuni hiyo imekuwa ikiwapeleka kwa ndege watalii matajiri zaidi kuwinda simba na wanyama wengine hali iliyowaghadhabisha wenyeji wa eneo hilo ambao ni wamaasai ambao wamezuiwa kuwalisha mifugo wao katika maeneo ya kuwinda.
Sasa serikali ya Tanzania inataka kutoa ardhi zaidi kwa wawindaji hao kwa lengo la kujenga barabara ya umbali wa kilomita 1,500 ambako wanyamapori watakuwa wakipita kwa manufaa ya kampuni hiyo ya uwandaji.
Mpango huo utawaathiri takriban watu 30,000 watakaoachwa bila makao na pia kuwaathiri maelfu ya wengine, ambao huwalisha mifugo wao katika maeneo hayo wakati wa msimu wa kiangazi.

Wamaasai wameghadhabishwa mno na hata kufanya maandamano, wakisema kuwa maisha yao yataathirika pakubwa.
Zaidi ya asilimia ya 90 ya wakaazi wa Loliondo ni wa Maasai ambao hutegemea kuwalisha mifugo wao nyasi kutoka eneo ambalo serikali inanuia kuwakodishia waarabu.
"bila Ardhi hatuwezi kuishi,'' anasema mama Naishirita Tenemeri, mwenye watoto watatu.
Bi Tenemeri anafuga Ng'ombe na Mbuzi eneo la Loliondo, ili kuwanunulia chakula na kuwalipia karo ya shule wanawe.

Wa Maasai wana historia ya kupoteza ardhi yao nchini Tanzania tangu wazungu walipowahamisha kutoka mbuga ya Serengeti mwaka 1959.

Mapema mwezi huu, Bi Tenemeri, akiwa amejifunga shuka yake nyekundu, alijiunga na watu 1,000 wengi wao wakiwa wanawake chini ya miti ya mivule, katika kijiji cha Olorien kupinga mipango ya serikali kuuza ardhi yao.
Wengine walitembea kwa siku nyingi kuonyesha ghadhabu yao kwa kujiondoa katika chama tawala cha CCM kama wanachama.
"ikiwa sina ardhi, sina mahala pa kujifungulia watoto wangu,'' alisema Bi Morkelekei Gume,akitupa kadi yake ya uwanachama wa CCM chini .
"mwanangu yuko katika shule ya upili, kwa sababu ya nyasi zinazotoka hapa.''
''Ikiwa wanataka ardhi yangu wanaweza kuniua.''

Mwanamke mmasaai anashikia bango linalosema "tutapigania ardhi yetu hadi mwisho wake.'' Wanawake hapa ndio wamekuwa wakisikika zaidi katika maandamano yao.
Wanawake wamekuwa wakisikika zaidi, wameathirika zaidi kutokana na hatua ya serikali kuwafukuza, wakiachwa bila kazi kuwalea watoto wao kwa hali ngumu wakati wanaume wakienda katika sehemu za miji ambako wanapata kazi kama walinzi.
Pia wameongoza maandamano tangu viongozi wao wa kisiasa waliopinga mpango wa ujenzi wa barabara waliokuwa wamesema wataondoka katika chama tawala kukosa kutimiza ahadi zao.
Eneo la Loliondo lina wanyama wengi wa porini na hivyo kuvutia watalii ingawa sio wengi. Linapakana na mbuga ya wanyama ya Maasai Mara iliyoko Kenya pamoja na hifadhi ya wanyama ya Ngorongoro.
Waziri wa utalii Khamis Kagasheki anatetea hatua ya serikali kutaka kuwaondoa wamasaai katika eneo hilo akisema kuwa mradi huo utasaidia katika kuendeleza uhifadhi kwani Maasai wametumia ardhi hiyo vibaya.

Lakini wasomi wanasema kuwa jamii ya wamaasai kawaida hawaathiri wanyamapori.

"nina swali moja kubwa kwa wanaosema kuwa wamaasai ni tisho kubwa kwa wanyamapori kuliko kampuni hiyo ya kiarabu ya OBC," alisema Benjamin Gardner wa chuo kikuu cha Washington na ambaye amesomea maswala ya ardhi miongoni mwa wamaasai kwa miongo miwili.

Ni nadra kwa wamaasai kuwinda wanyama na hutumia ardhi kuzuia baadhi ya wanyama kujifungulia huko kwani ni tisho kwa mifugo wao.
Mashirika 13 ya kijamii kutoka kote nchini Tanzania, yamesema kuwa wamaasai, wana vibali vichache sana vya kumiliki ardhi, na kuwa serikali inawapotosha watu
Viongozi wa jamii hiyo wanapanga kwenda mahakamani kuishtaki serikali, lakini wanahofia kuwa huenda swala hilo likakosa kutatuliwa haraka kwani kuna kesi moja iliyowasilishwa mwaka 2009 na haijapata ufumbuzi hadi wa leo.
bbcswahili

No comments:

Post a Comment