=================

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa nyota wa zamani wa timu ya soka ya Simba na Taifa, Joseph Kaniki ‘Golota’ na bondia Mkwanda Matumla wanashikiliwa huku Addis Ababa, Ethiopia wakituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya.

Kukamatwa kwao kumezidi kuongeza idadi ya Watanzania maarufu waliotiwa mbaroni nje ya nchi katika siku za karibuni wakituhimiwa kwa makosa hayo.

Tukio hilo limetokea miezi miwili baada ya Watanzania wawili, wasanii Agnes Gerald Masogange na Melisa Edward kukamatwa kwenye Uwanja wa Oliver Tambo, Afrika Kusini wakituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 150 na thamani ya Sh6bilioni.

Aidha, hilo limetokea baada ya meli ya mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa nchini kukamatwa na maofisa Forodha na askari wa doria wa Italia katika Pwani ya Sicily, Bahari ya Mediterranean ikiwa na tani 30 ya dawa za kulevya aina ya bangi zenye thamani ya Pauni za Uingereza 50milioni (Sh125 bilioni).

Kaniki na Matumla walikamatwa Agosti 31, mwaka huu kwenye Uwanja wa
Ndege wa Bole, Addis Ababa wakati wakijiandaa kupanda ndege ya Shirika
la Ndege la Ethiopia tayari kwa safari ya kuelekea Paris, Ufaransa.

Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Samuel Shelukindo alithibitisha
jana kwamba wanamichezo hao wanashikiliwa nchini humo na Polisi wa
Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Jinai.

Wanamichezo hao wamepandishwa kizimbani katika Mahakamu Kuu ya
Ethiopia iliyoko kwenye eneo la Arada, Addis Ababa kujibu tuhuma za kubeba kilo saba za dawa hizo haramu.

Mkwanda anadaiwa kubeba kilo nne wakati Kaniki akidaiwa kubeba kilo tatu.

Kama watapatikana na hatia, wanaweza kufungwa kifungo cha miaka tisa hadi 15.

Alisema uwezekano wa kesi ya Kaniki na Matumla kurudishwa Tanzania haupo kwa kuwa nchi hizi mbili hazina utaratibu wa kubadilishana wafungwa.

“Wameshikiliwa hapa Ethiopia kwa zaidi ya siku 10 sasa, sisi tulipigiwa
simu na polisi wa hapa Alhamisi iliyopita kujulishwa kwamba kuna
Watanzania wawili wameshikiliwa kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya, tulipokwenda tukamkuta ni Kaniki na Matumla,” alisema Shelukindo.

“Wao wenyewe wanaeleza kwamba walipitia Mombasa na huo mzigo
walipewa na mtu mmoja. Lakini Kaniki yeye anajitetea kwamba huyo aliyewapa huo mzigo pale Mombasa anajuana vizuri na Mkwanda. “Kwa hiyo alichofanya yeye ni kuubeba tu.

Walikuwa wapitie hapa Addis wakashuke Paris, Ufaransa ndipo warudi
Sweden kwa njia zao wanazojua wenyewe. Walipofika hapa Mkwanda
alifanikiwa kupenya akapanda ndege lakini Kaniki akanaswa na mbwa ndipo
akajitetea kwa polisi kwamba lile begi lilikuwa lake lakini mizigo mingine
ilikuwa ya Mkwanda.

“Ndipo hapo sasa Mkwanda akashushwa kwenye ndege wakashikiliwa na
Jumatatu ya wiki iliyopita wakapandishwa kwenye Mahakama ya hapa kutajiwa kesi yao lakini hawakupewa nafasi ya kujitetea. Kesi itatajwa tena Jumanne (leo) na Jumatano (kesho) na uchunguzi wa polisi bado unaendelea.”

Wanamichezo hao walidai kwamba walikabidhiwa mizigo hiyo kwenye
Uwanja wa Ndege wa Mombasa walipokuwa wakikabidhiwa pasi za
kupandia ndege baada ya kupita sehemu zote za ukaguzi.

Source: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Ki...y/-/index.html