Wasimulia maisha ya Joseph Kaniki - Tanzania, Sweden na “unga” kutoka Brazil

11/09/2013
0 CommentsKaniki
Maisha mazuri kwa mshambuliaji wa zamani wa Simba, Joseph Kaniki ‘Golota’ sasa ni ndoto kwa kuwa huenda akafungwa miaka saba au zaidi kama atakutwa na hatia baada ya kukamatwa na madawa ya kulevya nchini Ethiopia, Alhamisi iliyopita.

Kama hiyo haitoshi, Kaniki hataruhusiwa kuingia barani Ulaya tena kwa kuwa makazi yake yalikuwa nchini Sweden na siku chache zilizopita, serikali ya nchi hiyo ilikuwa imempa kibali cha kuishi nchini humo kwa miaka mitano.

Kwa mujibu wa sheria za Sweden, aliyepewa kibali cha kuishi akikamatwa na madawa ya kulevya, basi mara moja anapokonywa na kuzuiwa kuingia tena katika mipaka ya nchi hiyo milele na mara moja taarifa inatolewa kwa nchi nyingine za Ulaya, iwe hivyo.

Alivyokamatwa:
Alikuwa na Mkwanda Matumla ambaye wakiwa Ethiopia alifanikiwa kuvukakatika sehemu za ukaguzi hadi kwenye ndege, mbwa akamnasa Kaniki.

Baada ya kupatikana na madawa hayo ambayo awali yalielezwa ni kilo tano, aliuruka mzigo na kusema alimbebea Mkwanda ambaye ‘alichomolewa’ kwenye ndege na kukutwa ana mzigo pia.

Uchunguzi ukaanza mara moja na wakashikiliwa na kitengo cha kupambana na madawa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole jijini Addis Ababa kabla ya kuhamishwa.

Habari za uhakika kutoka Sweden zinaeleza, Kaniki alikuwa akiishi nyumbani kwa Mkwanda katika mji wa Norrkoping takribani kilomita 200 kutoka mji mkuu wa Stockholm na kazi yake kubwa ilikuwa ni ufagiaji.

“Alikuwa akifanya kazi katika kampuni ya ufagizi (ufagiaji) hapa Norrkoping, kuna siku tuligundua ameanza kuuza unga na alisema kwamba alipewa na rafiki yake ambaye ni Mtanzania anayeishi Brazil. Kaniki alisema rafiki yake huyo ambaye alikataa kumtaja alikuwa akiingiza unga Sweden kupitia Tanzania. Siku chache baadaye akaacha kazi ya ufagizi na inaonekana aliingia kwenye kusafirisha unga, maana safari zilikuwa haziishi kurudi Afrika,” kilieleza chanzo cha uhakika kutoka Sweden.

Kwa mara ya kwanza, miaka minne iliyopita, Kaniki alikwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa katika Klabu ya Kalmar FF, akafeli na Haruna Moshi ‘Boban’ akapasi, lakini wakashindwa kuelewana, akaenda kujiunga na Gefle IF.

Mpenzi:
Kutokana na kufeli, ingawa alikuwa hataki lakini hakuwa na ujanja, akarejea nyumbani. Baada ya miezi kadhaa akarudi tena Sweden ambako alipata mpenzi mwenye umri zaidi ya miaka 50.

Alirejea Sweden baada ya mpenzi huyo kumfuata nchini, lakini si chini ya zaidi ya miezi kumi, wakawa wameachana, kila mmoja akimshutumu mwenzake ndiye chanzo, akachukua hamsini zake.

Soka:
Akiwa Sweden, aliendelea kutafuta timu ya kuichezea na baada ya miezi kadhaa akafanikiwa kusajiliwa na timu ya daraja la pili ya Konya Spor akiwa pamoja na Mtanzania mwingine aliyewahi kuichezea Simba, William John.

Hata hivyo, Kaniki hakuweza kupata mafanikio akiwa na Konya kutokana na kushindwa kuonyesha kiwango, lakini yeye akalaumu timu haikuwa makini.

Kaniki alilalamika kwamba timu hiyo haikuwa ikimlipa vizuri hivyo akaamua kuachana nayo na kutafuta maisha kivyake.

Msaada:
Maisha yake yalikuwa ya kutangatanga huku akikaa kwa rafiki zake, wakati fulani aliishi na Mtanzania mwingine aliyekuwa anacheza soka huko lakini baadaye ikaelezwa alimfukuza kwake.

Mtanzania huyo alimuamuru Kaniki kuondoka kwake kwa madai alikuwa na tabia ya kutotaka kushirikiana na wenzake katika suala la usafi na masuala mengine.

Kazi:
Kutokana na ugumu wa maisha, Kaniki aliamua kuhama Stockholm na kwenda Norrkoping ambako alianza kuishi pamoja na Mkwanda Matumla.

Inaelezwa pamoja na kufanya kazi hiyo ya ufagiaji katika majengo mbalimbali yaliyoingia mkataba na kampuni iliyomuajiri, lakini bado maisha yalikuwa magumu kwake.

Inaelezwa hicho ndicho chanzo cha kuamua kuingia kwenye biashara hiyo haramu na inaelezwa alianza na kuuza rejareja katika eneo lake la kazi.

Ndani ya Dar:
Kama Championi Jumatatu lilivyoeleza lilipoandika kwa mara ya kwanza habari yake, Kaniki alirejea jijini Dar hivi karibuni na kuonyesha jeuri ya fedha kila alipokwenda.

Moja ni ile ya kumwaga zaidi ya shilingi milioni mbili kwenye ukumbi ambao bendi ya FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’ ilikuwa inatumbuiza.

Rais wa FM Academia, Nyoshi El Saadat ‘Sauti ya Simba’, jana alithibitisha kwamba Kaniki aliwatembelea.
“Kweli tulikuwa naye kwenye shoo ya kule Mbezi, Kaniki ni mtu wa Ngwasuma sana na rafiki yangu. Alikuja pale, alicheza sana siku ile na alitoa fedha nyingi kututuza kutokana na kazi nzuri.”

Taarifa nyingine kutoka vyanzo mbalimbali zinaeleza, baada ya kurudi nchini akitokea Sweden wiki kadhaa zilizopita, Kaniki alimalizia ujenzi wa nyumba yake na kununua gari jipya.

Timu:
Mwanzoni mwa miaka ya 2000, Kaniki amewahi kung’ara akiwa na Simba. Lakini pia alifanya vizuri akiwa mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Rayon Sports ya Rwanda na timu ya taifa, Taifa Stars.

Wakati fulani aliwahi kuwaniwa na Yanga na kuzua mtafaruku mkubwa, mashabiki zaidi ya 2000 wa Yanga wakajitokeza kwenye Uwanja wa Kaunda kumshuhudia akitua Jangwani baada ya uongozi kutangaza.

Lakini Kaniki aliyekuwa amefanya mazungumzo na uongozi huo, alibadili mwelekeo na kurejea makao makuu ya Simba pale Msimbazi na kesho yake stori kubwa kwenye vyombo vya habari ikawa ni namna Golota alivyowaacha wazi Yanga wakimsubiri hadi kiza kinaingia.

Sifa yake kubwa ilikuwa ni upigaji mashuti makali ingawa hakuwa fundi kwa upande wa kontroo.

Chanzo cha makala: Gazeti la CHAMPIONISource: Wasimulia maisha ya Joseph Kaniki - Tanzania, Sweden na