Wednesday 5 October 2011

CHADEMA:TUNAKWENDA MAHAKAMANI



matokeo ya ubunge wa Jimbo la Igunga ambayo yalimpa ushindi mgombea wa CCM, Dk Dalaly Kafumu.

Katika taarifa yake kuhusu uchaguzi huo aliyoitoa jana, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alidai kwamba kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria, taratibu na maadili katika uendeshaji wake.

Hata hivyo, Mbowe alisema licha ya kupoteza jimbo hilo, chama chake kinajivunia mafanikio makubwa kilichopata katika muda mfupi kwa kupata kura nyingi ikilinganishwa na CUF ambacho licha ya kuwa na mtaji wa kura 11,000 kilizopata katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, kiliambulia kura 2,014.

Dk Kafumu alishinda kwa kupata kura 26,484 kati ya kura 52,487 halali zilizopigwa, sawa na asilimia 50.4, akiwashinda wenzake saba wa vyama vingine.

Mgombea wa Chadema, Joseph Kashindye wa Chadema alipata kura 23,260 sawa na asilimia 44.3 akifuatiwa na Leopold Mahona aliyepata kura 2,104 sawa na asilimia nne.

Akizungumzia nia yake ya kwenda mahakamani, Mbowe alisema CCM kilitumia kiasi kikubwa cha fedha na rasilimali nyingine katika uchaguzi huo kuliko ambavyo imewahi kutokea katika chaguzi nyingine ndogo na kwamba kulikuwa na hujuma za wazi zilizofanywa, hivyo kukiukwa sheria na maadili yanayoongoza uchaguzi.

Alisema kulikuwa na vitendo vya rushwa vilivyofanywa na chama kimoja cha siasa na kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ilishindwa kuchukua hatua licha ya kuwa na uwezo wa kufanya hivyo kisheria.

Mwenyekiti huyo wa Chadema pia aliilaumu polisi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) akidai kwamba wamechangia kuharibu mchakato mzima wa uchaguzi huo mdogo.

Alidai kwamba CCM kilitumia chakula cha msaada kwa waathirika wa njaa kama silaha ya kisiasa kwenye uchaguzi na kwamba wananchi wa Igunga walipewa mahindi wakirubuniwa ili wakipigie kura chama hicho.

Viongozi wa Serikali
Mbowe alisema ushindi wa CCM pia ulichangiwa na chama hicho kupuuza sheria za uchaguzi kwa kutumia viongozi na rasilimali za umma kwa ajili ya kukinufaisha.

“Mawaziri na viongozi kadhaa waandamizi wa Serikali walifanya kampeni za waziwazi kwa niaba ya CCM na kwa kutumia magari na muda wa Serikali… viongozi haohao wa Serikali walitumia rasilimali za Serikali kama chakula cha msaada, ahadi ya kiserikali kuhusu mgawo wa fedha za ujenzi wa daraja na ahadi ya kutoa pembejeo kwa wakulima,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo ya Mbowe.

Kuhusu NEC, alisema kulikuwa na ukiukwaji wa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 kutokana na Tume hiyo kuwanyima haki ya kupiga kura baadhi ya watu ambao utambulisho wao ulikuwa na utata.

“Mpigakura yeyote ambaye utambulisho wake ni wa mashaka, anatakiwa aruhusiwe kupiga kura baada ya kupewa onyo na kujaza tamko la kisheria kuthibitisha kuwa ana haki ya kupiga kura katika kituo husika,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Licha ya msimamo huo wa kisheria, NEC ilitoa maelekezo kwa maandishi kwa wasimamizi wa vituo vya kupigia kura yanayokataza wapigakura wasiokuwa na kadi za kupiga kura, kutoruhusiwa kupiga kura.”

Alisema mbali na kukiuka Sheria ya Uchaguzi, maelekezo hayo yalitoa mwanya wa ununuzi wa kadi uliofanywa na chama cha siasa kimojawapo na kwamba ndiyo chanzo cha watu wachache kujitokeza kushiriki uchaguzi huo, ikilinganishwa na idadi ya walioandikishwa.

Wapigakura walioandikishwa katika Jimbo la Igunga ni 171,019 na waliojitokeza kupiga kura mwaka huu ni 53,672 sawa na asilimia 31.3, kukiwepo ongezeko la asilimia 2.7 ikilinganishwa na idadi ya waliopiga kura mwaka jana ambao walikuwa 49,013 sawa na asilimia 28.6 ya 171,077 waliokuwa wamejiandikisha.

Mbowe alisema kutokana na upotoshwaji wa kisheria uliofanywa na NEC, ipo hatari ya siku za usoni kukatokea madhara makubwa zaidi kwa watu walioandikishwa katika Daftari ya Kudumu la Wapigakura kunyimwa haki yao.
“Kwa rekodi yake hii na kwa sheria za uchaguzi zilizopo, NEC haina tena sifa ya kuweza kusimamia kazi hii muhimu ya kusimamia kura ya maoni itakayopitisha Katiba mpya ya Tanzania. Chadema itafanya kosa kubwa kama itafumbia macho ukweli huu,” alisema Mbowe.

Uchaguzi wa Igunga pia uliwashirikisha wagombea wengine ambao ni Steven Mahuyi (AFP) aliyepata kura 235, Hassan Rutegama (Chausta) aliyepata kura 182, Said Cheni DP kura 76 na Hemed Ramadhani (SAU) kura 63.

CCM walaumu wasimamizi

Kwa upande wake, CCM kimetoa shutuma kali kwa wasimamizi wa uchaguzi vituoni, kikisema kwamba walisababisha kupungua kwa kura zake katika uchaguzi huo.

Juzi, baada ya Dk Kafumu kutangazwa mshindi, Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama alidai kuwa chama chake kingeweza kupata ushindi mkubwa zaidi lakini kilihujumiwa na wasimamizi ambao alidai kuwa wengi walikuwa na mapenzi kwa Chadema.

“Ushindi huu unaonyesha kwamba kuna uongozi mpya ndani ya nyumba. Tumefanya vizuri lakini kama si hujuma za wasimamizi tungeshinda kwa kishindo kikubwa zaidi,” alisema Mukama.

Tuhuma hizo za Mukama kwa wasimamizi zinatokana na matokeo ambayo yanaonyesha kuwa licha yaa kushinda, CCM kimefanya vibaya katika jimbo hilo ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka jana wakati mgombea wake, Rostam alipopata ushindi wa kura 35,674 sawa na asilimia 72.7 ya kura halali zilizopigwa akimshinda aliyekuwa mgombea wa CUF, Mahona ambaye alipata kura 11,321 sawa na asilimia 23.1.

Kauli ya Mukama haikuwa ya kwanza kutolewa na viongozi wa CCM dhidi ya wasimamizi kwani siku ya uchaguzi, Oktoba 2, mwaka huu, Katibu wa Siasa na Mambo ya Nje wa chama hicho January Makamba alitoa tuhuma kama hizo akidai kwamba baadhi ya wasimamizi walikuwa wakiwapa wapigakura karatasi za kupigia kura ambazo tayari zilikuwa na alama ya tiki kwa mgombea wa Chadema.

Hata hivyo, Msimamizi wa Uchaguzi Igunga, Protase Magayane alipuuza tuhuma hizo akisema kuwa kulikuwa na fursa kwa vyama na umma kwa ujumla kutoa pingamizi pale wa wasimamizi hao walipoteuliwa kwa mara ya kwanza.

Alisema vyama vya siasa vilipaswa kufanya mapitio ya makini katika orodha ya wasimamizi na kwamba hatua zingechukuliwa kabla ya uchaguzi, badala ya kusubiri kulalamika siku ya uchaguzi.

CCM yairushia kombora Chadema
CCM kimeibuka na kudai kuwa vurugu za wanachama wa Chadema ndicho chanzo cha idadi kubwa ya watu kutojitokeza kupiga kura.

Katika uchaguzi huo, idadi kubwa ya watu hawakujitokeza kupigakura kwani kati ya watu 171,019 waliojiandikisha ni 53,672 tu sawa na asilimia 31.3 waliojitokeza Jumapili iliyopita.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema mabadiliko makubwa ya uongozi ndani ya chama hicho ndiyo yaliyokipa ushindi Igunga.

“Ushindi huu ni uthibitisho kuwa mapinduzi makubwa yaliyofanyika ndani ya chama yamezaa matunda na yanaungwa mkono na wananchi na ndiyo maana tumeibuka washindi Igunga,” alisema Nnauye na kuongeza:

“Kutokana na fujo za Chadema, idadi kubwa ya watu haikujitokeza kupiga kura. Uchaguzi huu umeonyesha jinsi Chadema walivyokuwa wabakaji wa demokrasia. Watanzania wanatakiwa kuikataa hali hii, hakuna demokrasia ya namna hii.”

Nnauye alisema kitendo cha CCM kushinda udiwani katika Kata 17 kati ya 22 katika Mikoa ya Arusha, Dodoma, Iringa, Manyara, Mara, Mbeya, Mwanza, Rukwa, Ruvuma na Sinyanga ni ishara kuwa hicho kinakubalika.

Mapokezi mazito
Nnauye alisema viongozi wakuu wa CCM ambao walikuwa Igunga watafanyiwa mapokezi mazito Jumamosi ijayo, Dar es Salaam.

“Kesho (leo) watapokewa na wananchi mkoani Singida, Oktoba 6, watakuwa Dodoma, Oktoba 7 watakuwa Mkoa wa Pwani na Oktoba 8 watakuwa Dar es Salaam. Tumefanya hivi kwa lengo la kuwashukuru wananchi,” alisema.

MWANANCHI

No comments:

Post a Comment