Wednesday 12 October 2011

TANZANIA KUANZA KUTOA TUZO YA UPISHI BORA




Asasi ya utafiti wa vyakula salama Tanzania (TAHEFORO) inatarajia kutoa tuzo ya upishi bora Tanzania (Bema Chef’s Award Tanzania) kwa lengo la kuendeleza ubunifu wa sanaa ya mapishi ya vyakula vya asili ya Kitanzania.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na mwenyekiti wa asasi hiyo Bw. Benedict Maato wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu azma ya asasi yake kuanzisha tuzo hiyo.
Amesema kuwa tuzo hiyo itakuwa ikisimamia ubunifu na uendelezaji wa sanaa ya mapishi ya vyakula vya asili ambavyo vipo katika hatari ya kutoweka.
“Jamii yetu leo, tumeacha kula vyakula vyetu vya asili ambavyo vina virutubisho vingi vya asili na usalama kwa afya zetu, badala yake tunapendelea kula vyakula hivi vya kisasa ambavyo vina matatizo makubwa kwa afya zetu” amesema Bw. Maato.
Amefafanua kuwa tuzo hiyo itakuwa ikishindaniwa kila mwaka ili kupata Wapishi bora wa vyakula vya Kitanzania, Mgahawa bora unaotoa huduma ya vyakula vya asili, vituo bora vya Redio na Luninga viinavyorusha vipindi vya mapishi ya vyakula vya asili, Waandishi bora wa makala au vitabu vya mapishi ya vyakula vya asili na Watafiti bora wa vyakula vya asili.
Aidha mwenyekiti huyo amebainisha kuwa lengo kubwa la utoaji wa tuzo hiyo ni kurudisha sanaa ya mapishi nchini na kusisitiza kuwa washiriki wote watakaoshindania tuzo hiyo watatakiwa kuonyesha ubunifu wao katika kupika vyakula hivyo na kutoa wito kwa wananchi kupenda kutumia vyakula vya asili

No comments:

Post a Comment