Wednesday 12 December 2012

Wadau waigomea Tanesco kupandisha bei ya umeme

WADAU mbalimbali wamepinga ombi la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuongeza bei ya nishati hiyo kwa asilimia 155 ifikapo Januari mwakani.

Pamoja na mambo mengine, wadau hao wamesema si wakati mwafaka sasa kwa Tanesco kupandisha bei ya umeme, kwani bado ina fursa ya kutosha kujikwamua katika matatizo yake, ikiwamo usimamizi wa rasilimali zake na kuboresha huduma kwa wateja.

Mambo mengine ambayo wadau hao waliyataja kuwa ni kikwazo kwa Tanesco kupandisha bei ya umeme ni rushwa ndani ya shirika hilo, mikataba mibovu, upotevu wa umeme kuanzia vyanzo vyake hadi kwa mteja na ukusanyaji mbovu wa madeni.

Wakizungumza jijini Dar es Salaam jana katika mkutano wa pamoja wa kupata maoni ya wadau kuhusu nia hiyo ya Tanesco, wadau hao walisema Tanesco haina sababu ya kupandisha bei ya umeme kwani bado inaweza kutumia rasilimali zake kujiendesha.
Tanesco imeomba ipandishe bei ya umeme kuanzia mwakani kutokana na sababu kadhaa ikiwamo ongezeko la gharama za uendeshaji na kukithiri kwa madeni ya shirika hilo la umma.

“Ongezeko la bei ya umeme ambalo linawezesha shirika kukidhi gharama za uendeshaji bila kupata faida ni asilimia 81.7 kutoka bei iliyoko sasa,” ilisema sehemu ya taarifa ya shirika hilo iliyowasilishwa kwenye mkutano huo na Kaimu Mkurugenzi wake Mkuu, Felchesmi Mramba.

Mramba alisema hadi Oktoba mwaka huu, Tanesco ilikuwa inadaiwa kiasi cha Dola za Marekani 250 milioni (Sh400 bilioni), madeni ambayo kimsingi yanachangia kurudisha nyuma maendeleo ya shirika. Hata hivyo, Mramba hakueleza madeni ambayo shirika hilo linawadai wateja wake ambayo yanaelezwa kuwa ni mengi yanayoweza kufidia kwa kiwango kikubwa pengo hilo.

Katika michango yao kwa nyakati tofauti, wadau hao walipinga maombi hayo ya Tanesco kuongeza bei ya umeme, badala yake wakalitaka shirika hilo kuongeza ufanisi katika utendaji wake ikiwamo kukusanya madeni kutoka kwa wateja na kutoa huduma bora kwao.
Mwakilishi wa Shirika la Ugavi wa Umeme Zanzibar (Zeco) Mohamed Suleiman Khatib, alisema hawakubaliani na ombi hilo la Tanesco akisema hata bei ya iliyopo sasa inawakandamiza wakazi na wawekezaji wa Zanzibar.

“Iwapo bei hizi zitaongezwa, basi wananchi wa Zanzibar watakuwa na maisha magumu kutokana na gharama za maisha kuongezeka. Pia wawekezaji watahama na kukimbilia Bara ambako kutakuwa na bei nafuu ya umeme.”

Khatib alieleza kuwa Zeco inatumia kati ya Mega Watti 55 hadi 60 sawa na asilimia 4 ya umeme wote nchini, lakini ripoti ya mshauri elekezi ilishindwa kumtambua kuwa ni mtumiaji mkubwa wa umeme, hali ambayo itaibebesha mzigo mkubwa
Makamu Mwenyekiti wa Barazala Ushauri la Ewura, Said Mohamed alisema hawakubaliani na kupandishwa kwa bei ya umeme kwa kiwango hicho ambacho Tanesco imekiomba.

Alisema hiyo inatokana na mshauri elekezi kutumia kiwango cha ongezeko la asilimia 40.29 kilichoanza mwaka huu kama msingi wa kutafuta bei mpya kwa miaka mitatu ijayo.

Katika mchanganuo wake wa miaka mitatu, mshauri huyo elekezi alitaka bei ya wastani ya sasa iongezeke kwa asilimia 29.49 sawa na Sh253.76 ya bei ya sasa ya Sh195 ambayo ilipangwa kutozwa mwaka huu na alipendekeza ongezeko la asilimia 4.69 sawa na Sh265.65 kwa mwaka 2013; asilimia 0.9 sawa na Sh268.03 kwa mwaka 2014 na asilimia 8.64 sawa na Sh291.19 kwa mwaka 2015.

“Inaelekea mtaalamu elekezi kutoka Hispania (AF-Mercados), aliyepewa kazi ya kutafiti gharama za Tanesco na kupanga bei ya umeme ana uelewa au uzoefu mdogo wa kufanya kazi za namna hiyo kwenye nchi za dunia ya tatu kama Tanzania,” alisema Mohamed.
Aidha, baraza hilo limepinga mfumo wa bei wa moja kwa moja uliopendekezwa na mshauri huyo elekezi likisema kuwa unakusudia kuilinda Tanesco dhidi ya mtumiaji ambaye ni mlalahoi kutokana na bei za umeme kupanda.

mwananchi

No comments:

Post a Comment