Wednesday 15 May 2013

Lipumba: Kuna njama za kumwongezea JK muda



Dar es Salaam. 
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba amedai kuwa amenasa taarifa za siri za kuwapo kwa mipango ya kuongeza muda wa Serikali ya sasa kukaa madarakani.
Profesa Lipumba alisema hiyo inatokana na wasiwasi kuwa mchakato wa Katiba Mpya hautaweza kukamilika mwaka 2014 hivyo kutokuwa rahisi kwa uchaguzi kufanyika mwaka 2015.
Akizungumza Dar es Salaam jana, wakati akifungua kikao cha Baraza Kuu la CUF, Profesa Lipumba alisema kuwa Serikali inataka kuongezewa muda wa kukaa madarakani kwa miaka miwili ikimaanisha kuwa Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete itakaa madarakani hadi mwaka 2017.

Hata hivyo, madai hayo ya Profesa Lipumba yamepingwa vikali na Serikali na viongozi wake watatu waandamizi ambapo walijibu walipoulizwa kwa maandishi na mwandishi wetu mjini Dodoma wanakohudhuria kikao cha Bunge.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe alijibu: “Mchakato wa Katiba upo ‘on track’ (unakwenda vizuri) hatuna sababu ya kufanya hivyo.”
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alijibu” “Njooni ofisini kwangu nitasema ni kitu gani.”
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi alijibu kwa utani bila ya kufafanua: “Njooni niwajuze, unajua kamba haitoki Ukambani kama ilivyo kamba.”
Profesa Lipumba amemwomba Rais Kikwete asilikubali wazo hilo akisema wananchi hawatakubali na taifa linaweza kuingia katika mtafaruku.
“Nitapenda kuona Rais Kikwete akikataa jambo hilo kwani litachafua taswira ya nchi. Hatua hii ni kinyume cha utawala bora,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema Serikali haipaswi kuhofia uchaguzi kwa sababu ya Katiba kwani bado uwezekano wa kuandaa uchaguzi wa haki na huru unawezekana kwa utaratibu mwingine.
“Mchakato wa Katiba unaendelea, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatuambia kwamba mwaka 2014 tutakuwa na Katiba Mpya, sasa CUF tunasema kwamba hata kama Katiba Mpya haitapatikana kwa kipindi hicho kuwe na Tume huru ya Uchaguzi,” alisema Profesa Lipumba.
Jukwaa la Katiba kutinga mahakamani

MWANANCHI

No comments:

Post a Comment