Wednesday, 1 May 2013

Majengo ya serikali yazingirwa Libya




Ofisi za wizara ya sheria mjini Tripoli, Libya,zimezingirwa na watu waliojihami wakitaka kufurushwa kwa maafisa wa serikali waliokuwa wanafanya kazi wakati wa utawala wa Gadaffi.
Wanaume walio ndani ya malori wakiwa wamejihami kwa zana nzito wanawataka wafanyakazi kuondoka nje pamoja na waziri wa sheria.Waziri huyo aliingia ndani ya gari lake na kuondoka katika eneo hilo.
Jengo lenye makao ya wizara ya mambo ya nje, pia lilikuwa limezingirwa na watu hao tangu siku ya Jumapili.
Watu hao wanataka sheria ambayo itawaharamisha maafisa waliofanya kazi chini ya serikali ya Muammar Gaddafi kutoshikilia nyadhifaa kuu serikalini.
Hata hivyo, maafisa nchini Libya hawajaweza kukubaliana na matakwa hayo.

'hawatumii nguvu'

"watu hawa walifika hapa saa za asubuhi ndani na magari yao na kuzingira jengo hilo. Kulikuwa na magari 15. Waliwataka wafanyakazi wote kuondoka pamoja na waziri wa sheria. Waziri aliingia ndani ya gari lake na kuondoka,'' alisema mmoja wa wafanyakazi waliokuwa ndani ya jengo hilo.
"Hawakutumia nguvu.Hawakufyatua risasi wala kutumia nguvu,'' alisema mfanyakazi huyo.
Mwandishi wa BBC Rana Jawad, taswira au picha ya kikosi cha wapiganaji kuzingira jengo la serikali ilikuwa zamani ikihusishwa sana na wabunge.
Mwezi Machi, waandamanaji waliwazuia wanachama wa GNC kuondoka kutoka jengo hilo kwa masaa manne,wakisisitiza kuweka sheria itakayowazuia maafisa wa zamani waliohudumu chini ya utawala wa Gaddafi kuondolewa katika siasa za nchi.
Tangu kifo cha Gaddafi kutokea, mji mkuu Tripoli pamoja na miji mingine imekuwa ikikumbwa na ghasia.
Serikali imekuwa ikijaribu kusambaratisha makundi ya wapiganaji yaliyoanza kujipa umaarufu baada ya kuong'olewa mamlakani kwa Gaddafi.
Wiki jana , bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari, lililipuka nje ya ubalozi wa Ufaransa mjini Tripoli na kuwajeruhi walinzi pamoja na kusababisha uharibifu mkubwa.

BBCSWAHILI

No comments:

Post a Comment