Monday, 6 May 2013

VITA YA LADY JAYDEE NA CLOUDS YAENDELEA RUGE AANIKA YAKEJudith Wambura Mbibo ‘Jide’ au ‘Lady Jaydee’.

Jumatano iliyopita, Jide kupitia akaunti ya mtandao wake wa kijamii aliandika wosia wake mzito akizungumzia kwa sehemu kubwa ‘ugomvi’ wake na uongozi mzima wa Clouds Media ambapo alithubutu kuwataja majina walengwa, habari ambayo ilichapishwa na Gazeti la Ijumaa la Mei 3, 2013.
Gardner G. Habash.
MAMBO YAMGEUKIA GARDNER
Baada ya wosia huo kutoka, wadau mbalimbali walitoa maoni yao kwa kutumia mitandao au kuzungumza na gazeti hili moja kwa moja, wengi wakimshukia mume wa Jide, Gardner G. Habash kwamba alishindwaje kumshauri mkewe kuacha kuandika wosia mzito kama huo.
“Jamani siyo siri, wosia wa Jide kwa Clouds ni mzito sana, mtu unasoma unasisimka. Lakini mimi namlaumu mumewe (Gardner), kwa nini alishindwa kumzuia mkewe asiandike maneno mazito kama yale?
“Ni wosia uliotakiwa kutunzwa na wakili lakini si  kuuanika kwenye vyombo vya habari, ni mkali sana. Gardner ameonesha upungufu wa usimamizi wa nyumba kama kichwa,” hayo ni maneno ya msomaji wetu, Elisha Mjata, mkazi wa Makumbusho, Dar es Salaam.
Naye Mwalije Jumula wa Mbezi Beach, Dar alisema: Ningekuwa mume wa Jide nisingekubali aandike wosia kama ule na kuuachia kwenye mtandao, licha ya kujaa ukali lakini pia umesheheni vijembe, kuanikana wakati wosia unatakiwa ujae maelekezo na ufafanuzi.
Ruge Mutahaba.
WANACHOELEZA WENGINE
Ukiwaacha waliomshushia lawama Gardner kwa kushindwa kumuonya mkewe kuhusu kuandika wosia huo, wengine walikwenda mbele zaidi kwa kudai kwamba wanaamini mumewe huyo ndiye aliyeandika wosia huo kwa sababu maneno mengi ya kijasiri si rahisi kutoka kwenye kichwa cha mwanamke.
“Mimi siamini kama akili za Jide zinaweza kutoa maneno yale, lazima wosia umeandikwa na mumewe. Maneno mengi ni ya kijasiri, Jide hawezi bwana,” alisema Simon William, mkazi wa Mbweni, jijini Dar.
Waliozungumza kuhusu imani zao juu ya mkono wa Gardner kuhusika na wosia huo ni wengi.

GARDNER AIBUKA, AJIBU MAPIGO
Habari zinadai kuwa Gardner alipata vijembe hivyo kupitia mitandao na midomo ya watu aliokutana nao laivu wakimsema kuhusu udhaifu wa kushindwa kusimamia nyumba, naye akaamua kutoa yake ya moyoni.
Akizungumza kupitia Kipindi cha Take Over cha TBC1, Ijumaa iliyopita ambapo mtangazaji alimuuliza nini majibu yake kuhusu wosia mzito wa mkewe, kwanza Gardner alikiri maneno ya kwenye wosia huo yalitoka moyoni mwa Jide, yeye hahusiki hata kidogo.
Gardner: Ni maneno ambayo yametoka moyoni mwake (Jide) na ni maneno mbayo anajitetea kama msanii. Mimi kama meneja ukiacha pia kama mke wangu naendelea kumsapoti kwa kile ambacho anaona ni sawa, basi mimi nitaendelea kumsapoti na kujaribu kuzungumza na Lady Jaydee.
“Mara nyingi anasema tu kwamba watu wasifikirie ni suala la wimbo kupigwa au kutokupigwa, hayo ni mambo ya kawaida lakini wafikirie tu kwamba huyu mtu anaongea kutokana na experience (uzoefu) aliyokuwa nayo na wale watu.
“Baada ya mwaka 2003 kuacha kufanya kazi kwenye management yao ya Smooth Vibe, yalitokea mambo mengi hapa katikati ila hakusema lakini siku za hivi  karibuni kuna mengine ambayo yametokea, ndiyo akaona hapana, nisiposema nitazidi kukandamizwa na matokeo yake nitakufa kisabuni.

WOSIA HUO NI KAMA VITA, AMEJIPANGAJE?
Gardner: Unapoamua kusema ukweli suala la kujipanga mara mbili huwa halipo, ni kwamba unasema ukweli
watu... watauliza juu ya uhasama lakini ulikuwepo tayari kwa hiyo watu wajue kwa sasa Jide ameamua kuongea, lakini alikuwa na matatizo na wale watu tangu kipindi cha nyuma, kwa sababu wale wana mfumo dume wa kufanya kazi na alipoachana nao aliona kama wanamfuatilia kulekule alipo.

CHOKOCHOKO ZILIANZIA WAPI?
“Unajua kwa mfano, unaweza kumuomba mtu maji akakwambia sina, ukayaona yale pale, ukamwambia niuzie akakuuzia ila bado alivyokuuzia akaona kama unafaidi, mwisho akakwambia yameisha, ukaenda sehemu ukayapata bure, akaona umepata, akakufuata kulekule na akakukuta unakunywa kwenye glasi kisha ‘akakuputa’, sasa hapo inabidi useme hapa unavyofanya siyo sawa ndiyo hicho alichokifanya Jaydee,” alisema Gardner.
Aliendelea kusema kuwa uwepo wa msanii na stesheni za redio hutegemea uwepo wa umma wa Watanzania au mashabiki kwa jumla.
Akaendelea: Jaydee anapata sapoti kutoka kwa Watanzania, kwa hiyo hajaathirika chochote, pia  anaendelea kufanya kazi kwa bidii.
“Woga ni kitu ambacho binadamu tumeumbiwa, wakati mwingine unasaidia wakati mwingine unakudhuru kwa   sababu wanasema adui wa maendeleo yako ni wewe mwenyewe, ndiyo maana woga wako unaweza ukasababisha ukakandamizwa zaidi.”

RUGE KUFUNGUKA LEO
Wakati Gardner akimpigania mkewe, habari za uhakika zinadai leo Jumatatu, Bosi wa Clouds Media, Ruge Mutahaba anaongelea suala hilo kupitia Clouds FM, asubuhi kwenye kipindi cha Power Breakfast.
Ili kupata uhakika, Jumamosi iliyopita, Wikienda lilimwendea hewani Ruge kwa lengo la kupokea sehemu ndogo ya atakachozungumza leo.
“Siwezi kusema chochote ila kweli Jumatatu (leo) nitaongea,” alisema Ruge.

ATASEMA HIKI?
Wakati bosi huyo akiweka msimamo wa kutosema chochote, vyanzo vilidokeza kwamba miongoni mwa mambo atakayoweka wazi Ruge ni ukweli kuhusu sakata hilo na kujibu lawama za Jide.
“Ruge ataongea Jumatatu, ataweka wazi sakata hilo. Atajibu lawama za Jide moja baada ya nyingine. Unajua ukweli ni kwamba Jide amelipuka tu, hana data za kutosha za kumbebesha lawama mtu,” kilisema chanzo.

JIDE AULIZWA, KWA NINI IWE SASA?
Baadhi ya watu mitaani wamekuwa na mjadala mpana kuhusu wosia wa Jide, wakisema kwa nini ameuanika  kipindi hiki ambacho pia anapigia debe shoo yake ya Miaka 13 ya Lady Jaydee ambapo anasema atazindua albamu yake mpya ya ‘Nothing  But The Truth’.
“Mimi jamani naamini Jide ameuanzisha mgogoro na akina Ruge ili kujipandisha kwa ajili ya shoo yake ya Miaka 13 ya Lady Jaydee, kama kweli ana bifu na wale jamaa kwa nini iwe sasa? Anataka kupanda yule,” alisema Gabriel Malaika, mkazi wa Oysterbay, Dar.

SALAMU KWA RUGE
Hata hivyo, Malaika alikwenda mbele zaidi kwa kumshauri Ruge kwamba anapaswa kukaa chini na kujipima kwani shutuma za wasanii kwake ni nyingi, ingawa alisema anaamini zinatokana na bosi huyo kupenda kukaa kimya anapotupiwa madongo.

GPL  

No comments:

Post a Comment