Friday 4 March 2011

Mahakama yazuia mkataba wa Tanesco, Dowans

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini,Januari Makamba

KAMATI ya Bunge ya Nishati na Madini imependekeza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuingia mkataba mpya na Kampuni ya kufua umeme ya Dowans ikiwa ni hatua za muda mfupi kukabiliana na tatizo la umeme nchini.

Hata hivyo, Mahakama Kuu imeizuia Serikali na Tanesco kuchukua hatua yoyote inayohusiana na mazungumzo au mkataba wa aina yoyote baina yake na Dowans bila ridhaa yake.

Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Januari Makamba alisema: "Kamati imependekeza mambo 30 ikiwamo kuwashwa kwa mitambo ya Dowans haraka na serikali itoe fedha zaidi kununua mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya IPTL. Hatua hii imefikiwa kama suluhisho la muda mfupi la kupambana na mgawo.''

Makamba alisema pia kwamba kamati imependekeza kupunguzwa kwa megawati 50 kutoka katika migodi ya madini inayotumia umeme wa megawati 125 ili zipelekwe kwa wananchi.

Makamba ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga alisema mapendekezo hayo watayakabidhi katika Ofisi za Bunge na kwamba yatatangzwa na Spika, Anne Makinda

Lakini, wakati kamati ikitoa mapendekezo hayo, jana Jaji Emilian Mushi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam anayesikiliza maombi ya usajili wa tuzo ya Kampuni ya Dowans iliyoshinda iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara(ICC), dhidi ya Tanesco alitoa agizo kuwa lisifanyike jambo lolote kuhusu Dowans nje ya mahakama.

“Naagiza jambo lolote lisifanyike nje ya mahakama wakati ikiendelea na shauri hili. Kama kutahitajika kuwa na majadiliano yoyote basi pande husika zilete maombi mahakamani ili iweze kusimamisha kwanza mchakato huu kusubiri majadiliano hayo."

Jaji Mushi alisema: "Haitakuwa vyema mahakama kuendelea na mchakato wakati na huko nje majadiliano yakiendelea. Kama pande hizo zikiafikiana, basi zinaweza kuja ‘ku-withdraw’ (kuondoa shauri) na kama zitashindwana basi ndipo tutakapoendelea na mchakato.”

Habari zilizolifikia gazeti hili jana na kuthibitishwa na Makamba zinasema kuwa mapendekezo ya kamati hiyo yamefikiwa kama suluhisho la muda mfupi la kupambana na mgawo.

Chanzo chetu ndani ya kamati hiyo, jana kiliiambia Mwananchi kuwa kamati imependekeza kabla ya kuwashwa mitambo hiyo, Tanesco liingie mkataba maalumu wa miezi michache usiokuwa na utata wa kisheria wa kuuziwa umeme na kampuni ya Dowans kulingana na mahitaji.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, katika mkataba huo kamati imependekeza Tanesco iuziwe umeme kwa uniti na kwamba iwe inalipa kila siku kulingana na kiwango inachouziwa.

"Kwa kuwa suala la gharama za uuzaji umeme kwa uniti ni la kitaalamu, kamati imependekeza Tanesco iingie mkataba maalumu wa miezi michache wa makubaliano ya kuuziwa nishati ya umeme na ilipe kulingana na uniti iliyouziwa,'' kilisema chanzo chetu.

Awali, kabla ya kuanza kwa kikao cha kamati hiyo katika Ofisi Ndogo za Bunge, Dar es Salaam, Makamba aliimbia Mwananchi kuwa: "Leo (jana) wajumbe wa kamati, tunakutana ili kusahihisha herufi, maneno pamoja na kuweka koma na nukta katika ripoti yetu ya mapendekeo ya suluhisho la muda mfupi na mrefu la tatizo la umeme nchini."

Mwenyekiti huyo alisema mapendekezo hayo yalifikiwa juzi katika kikao chao cha majumuisho na Tanesco kilichomalizika saa 2:00 usiku.

Tofauti ya wananchi na wafanyabiashara kuhusu Dowans
Hata hivyo, mapendekezo ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini yametolewa kukiwa na msuguano kati ya wafanyabiashara na wananchi. Wafanyabiashara wanataka mitambo ya Dowans iwashwe huku baadhi ya wananchi wakipinga na kutaka itafutwe mitambo mingine kupunguza tatizo hilo.

Kwa takriban wiki mbili, kamati hiyo ilifanya vikao vya ndani na mikutano ya wazi na wadau mbalimbali kukusanya maoni kuhusu suluhisho la muda mfupi na mrefu la tatizo la umeme nchini.

Lakini Jumamosi iliyopita katika kikao cha wazi kilichofanyika katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam baadhi ya wananchi walikataa kuwashwa kwa mitambo ya Dowans huku wasomi, wamiliki wa viwanda na wafanyabiashara kutaka mitambo hiyo iwashwe ikiwa ni njia ya haraka na suluhisho la muda mfupi la kupatikana kwa umeme.

Hatua hiyo ililenga kuongeza kiwango cha nishati hiyo kilichopungua katika Gridi ya Taifa kutokana na kushuka kwa uzalishaji katika mitambo ya umeme Mtera kulikosababishwa na kupugua kwa maji.

Kwa sasa Gridi ya Taifa ina upungufu wa megawati 297 kwa kuwa vyanzo vilivyopo vinazalisha megawati 540 huku mahitaji halisi yakiwa ni megawati 833 za umeme.

source:mwananchi

No comments:

Post a Comment