Monday 9 January 2012

WAKAZI WA JANGWANI WAPINGA KUHAMISHWA

 
 
Wakazi wa Jangwani jana tarehe 8 /jan/2012 waliitisha kikao katika eneo la jangwani kujadili mustakabali wao baada ya kuwepo na mpango wa serikali wa kuwataka wahame eneo hilo hatari wakati wa mvua.Diwani wa kata ya Michikichini Gharib Diyami CCM lilipo eneo hilo ndiye alikuwa akiongoza kikao hicho ambacho kilitawaliwa na jazba na hasira kali kutoka kwa wananchi wote wakipaza sauti kulaumu azma ya serikali.Walimshambulia diwani na kutaka kumuondoa madarakani kwa kile walichodai ni nguvu ya umma.
   Diwani huyo akionyesha hasira vilevile aliwaambia hawawezi kumfanya kitu jambo lililoibua tafranikaribia na kuvuruga kabisa mkutano huo

MADAI YAO
Wakazi wa jangwani wanadai wanao uzoefu wa ulaghai wa serikali kila inapohamisha watu na kuwapeleka makazi mapya na kusema ikiwaonyesha viwanja huwa inawatelekeza wasijue waanze vipi ujenzi na hata maisha kwa ujumla.Hivyo hawataki kuhama mpaka wameridhika kuwa fedha wamepata za kutosha.
  Wanadai pia kuwa kuna namba zimewekwa katika baadhi ya nyumba na nyingine hazikuwekewa hivyo kujenga hisia kwao kuwa fidia ya nyumba itakuwa ya kibaguzi kwani hakuna anayejua namba hizo zina maana gani.
   Wanadai hakuna haja ya kuhama mahali ambapo wamezoea na kwamba mafuriko ni kwa sababu ya miundombinu mibovu,hivyo kushauri pesa zinazotaka kutumika kuhamisha watu zitumike kujenga miundombinu bora eneo hilo
    Wengine wanasema majengo yao ya jangwani yana gharama kuliko fidia ambayo serikali huwa inatoa kwani wanaona kuna usiri kwenye swala la kutathmini fidia hivyo wanahofia hasara kubwa na kukumbwa na umaskini ikiwa watavunja nyumba zao
    Wengine wanasema ni dhahiri serikali ndiyo inayowachanganya wananchi kwani baadhi yao wamekuwa wakilipia kodi maeneo hayo na wanazo leseni za ardhi na wengine wamemilikishwa kisheria na mahakama zaidi ya mara mbili hivyo kuwaambia sasa wahame ni kuwaonea na kuwasababishia hasara zaidi.
    Kutokana na madai yote haya ni dhahiri wakazi wa jangwani hawataki kuhama eneo hilo na wameazimia kuunda kamati ndogo ili kushughulikia swala hilo haraka kwenye ngazi ya mkuu wa mkoa na hata waziri mkuu na rais waliyedai walimchagua hivyo anapaswa kuwasikiliza.
Katika hatua nyingine, mdau alipata shida kwani baadhi ya watu walionyesha kukerwa na waandishi habari wanaokuja kuandika habari na kuwahoji watu kisha habari zinatoka zikionyesha kawa wao ni wakaidi,wakanitaka kuandika ukweli niliouona na ndicho mdau nilichofanya.Mwisho wananchi wanasubiri kwa hamu ujio wa mkuu wa mkoa ili watoe dukuduku lao
 
KUTOKA MJENWABLOG

No comments:

Post a Comment