Tuesday 6 March 2012

WARAKA WA 4 KWA RAIS JAKAYA KIKWETE


Na Manyerere Jackton
Mpendwa Mheshimiwa Rais Kikwete, leo naomba nihitimishe waraka huu ambao nimeuandika kwa wiki nne sasa.

Nashukuru kwamba wengi wameusoma. Kumekuwa na mitazamo mbalimbali, lakini kubwa na zuri zaidi ni kwamba wachangiaji wengi wanaonyesha wazi kuwa wanaipenda kweli kweli Tanzania.

Mimi, kama walivyo Watanzania wengine wengi, ninaipenda nchi yetu. Mara zote tunapokuwa katika mataifa ya kigeni tunajivuna kwa namna tunavyozungumzwa.

Tulisifiwa kwa ushujaa, uungwana na huruma, lakini sasa tuna sifa nyingine. Tunasifiwa kwa umbumbumbu, uzuzu na udhaifu wetu wa kushindwa kuipenda nchi yetu na hata kuwa tayari kuifia.

Tanzania imekuwa shamba la bibi. Watu wanakuja wakiwa masikini wa kutupwa, lakini ndani ya muda mfupi wanakuwa matajiri. Hili linauma sana. Katika Afrika, nadiriki kusema nchi zinazotafunwa vilivyo na wageni, katika 10, Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) tupo juu!

Kwa DRC tunaweza kuwasamehe kwa sababu kwa miaka mingi hawakuwa na Serikali imara. Wameuana wenyewe kwa wenyewe kwa kuchochewa na mataifa ya kigeni. Wamepitia kila aina ya adha.

Tanzania ni tofauti. Amani na utulivu wetu havijatusaidia kujiondoa kwenye unyonge wa kiuchumi. Dhiki zimetufanya wengi wetu sasa tuwe mawakala wa wageni wapora rasilimali zetu.

Tunawakaribisha na kuwaonyesha kila mwanya wanaoweza kuutumia, alimradi tu wachume kadri wanavyoweza, na sisi tubaki kuambulia ‘ten par cent’.

Mheshimiwa Rais, hivi karibuni Rais Paul Kagame wa Rwanda alitoa kauli iliyotosha kabisa kukufanya ujitambue. Ilitosha kabisa kukufanya ubadilike. Lakini huelekei.

Rais Kagame aliomba Tanzania impe Bandari ya Dar es Salaam japo kwa miezi sita tu, ili aweze kuuonyesha ulimwengu ni kwa namna gani inaweza kubadili, si uchumi wa Tanzania pekee, bali wa mataifa yote yanayoitegemea bandari hiyo, ikiwamo Rwanda.

Anaamini kuwa kwa kuwa na bandari inayofanya kazi vizuri, Tanzania isingeweza kuanza kutumia rasilimali nyingine kama za madini, misitu na kadhalika.

Rais Kagame alitumia lugha ya kidiplomasia tu kusema hivyo. Kimsingi ni alikwambia kuwa “umeshindwa”. Kauli hii ilitosha kukufanya uitishe kikao cha dharura cha Baraza la Mawaziri ili kusaka majibu ya vitendo kwa Rais Kagame. Hukufanya hivyo. Hukufanya kwa sababu, ama hukumwelewa au ulimpuuza.

Mheshimiwa Rais, mara kadhaa Serikali yetu imekuwa ikijitetea kuwa Rwanda imeendelea kwa sababu ni nchi ndogo. Sawa, Rwanda ni ndogo. Ukubwa wa Tanzania ni sawa na kuziunganisha Rwanda, Burundi, Uganda na Kenya pamoja. Lakini utetezi huu ni mwepesi mno.

Rwanda ni ndogo, sawa. Tujiulize, ina rasilimali nyingi kiasi gani? Jibu ni kwamba haina ukwasi wa rasilimali kama Tanzania. Bahari ya Hindi pekee kwa Tanzania, yenye urefu wa kilometa 1,000 ilitosha kuifanya nchi yetu iwe mbali kimaendeleo. Tumeiacha hazina hiyo itafunwe na majahili wa kiuchumi kutoka ng’ambo kwa kushirikiana na wenzao wa ndani.

Mheshimiwa Rais, kuna wazazi wenye watoto 10 au zaidi. Wanawahudumia vizuri sana watoto wao. Lakini kuna kina baba wenye mtoto mmoja au wawili wanazikimbia familia zao kwa sababu wameshindwa kuzihudumia. Hii ina maana kwamba kigezo cha wingi au uchache si hoja.

Kama wingi wa watu na ukubwa wa nchi vingekuwa kikwazo kwa maendeleo, basi leo hii China, India, Urusi, Marekani, Brazil yangekuwa ndiyo mataifa masikini zaidi kuliko yote duniani maana yana maeneo makubwa na idadi ya watu ni kubwa mno.

Kama uchache ni hoja, basi Rwanda ingekuwa mbali mno kimaendeleo kuliko Japan, Uingereza, Ufaransa na kadhalika. Kwa hiyo hili la udogo halina maana. Ni viji-sababu visivyokuwa na maana.

Pili, kuna mambo ambayo si lazima tuwe matajiri ndipo tuweze kuyatekeleza. Rwanda ni masikini, lakini miji yao ni misafi mno.

Hivi kusafisha mitaro, kuzuia utupaji taka hovyo, kuzuia ukojoaji hovyo mitaani na kadhalika, nako kunawezekana tu kama nchi ni tajiri au kama nchi ni ndogo? Mbona Rwanda wameweza? Mbona Moshi wameweza, lakini Dar es Salaam wameshindwa?

Mheshimiwa Rais, kila siku tunaomboleza vifo vinavyosababishwa na ajali za barabarani. Kama taifa, tumeshindwa kabisa kupunguza na hatimaye kulimaliza tatizo hilo. Matokeo yake tumeamua kuweka matuta kila mahali. Kila akigongwa mwanafunzi au mwenda kwa miguu, yanafuata maandamano. Kesho kunajengwa matuta. Matuta haya ya barabarani ni kielelezo cha mtindio wetu wa kukabiliana na matatizo yanayotukabili.

Tangu watu muhimu, akiwamo Waziri Mkuu Edward Sokoine wafariki dunia katika ajali, hatujajifunza kitu! Inasikitisha sana.

Mheshimiwa Rais, ni ukweli ulio wazi kwamba mara nyingi timu inaposhindwa kuleta ushindi, lawama zinamwendea kocha. Kocha ndiye anayepanga timu. Kocha hawezi kujitetea kwamba hakuleta ushindi kwa sababu wachezaji kadhaa walikuwa wazembe uwanjani! Hakuna aina hiyo ya utetezi kwenye soka.

Uongozi wa nchi, kama ilivyo kwa klabu, kocha wetu ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wachezaji wake ni mawaziri, makatibu wakuu, watendaji mbalimbali, mameneja, wakurugenzi na viongozi wa aina kwa aina.

Tuna viongozi wasiokuwa na sifa ya kuwamo kwenye timu, lakini kocha (Rais) umebaki ukiwatazama tu bila kuwaondoa au kuwafanya wawajibike uwanjani (kuwatumikia wananchi). Kwa sababu hiyo, ni wazi kwamba siku ya siku utastahili lawama kutokana na kikosi chako kushindwa kutuletea ushindi. Na kwa kweli unastahili kuzipokea lawama hizo.

Mheshimiwa Rais, hakuna nchi iliyoendelea duniani kwa kuamua kuua reli, na badala yake ikatumia barabara halafu itarajie kupiga hatua kimaendeleo. Angalia, mizigo mizito yote dunia, ama husafirishwa kwa reli, au kwa maji. Haiwezekani barabara ya lami, hata iwe imejengwa kwa kiwango gani, idumu baada ya kutumiwa na maelfu kwa maelfu ya malori yenye kupakia shehena nzito kupindukia. Barabara zote za Tanzania zipo hatarini kutopitika kipindi kifupi kijacho kwa sababu zimelemewa na mizigo ya malori.

Kuna habari kwamba wapo wafanyabiashara wanaowahonga wasaidizi wako ili usafiri wa reli utoweke kabisa. Wanasema viongozi watoa uamuzi ndiyo wamiliki wakuu wa malori hayo. Kwa kuwa ni wamiliki, hawana jeuri ya kukemea uuaji huu wa reli.

Hata pale wanapojitutumua kukemea, wamekuwa wakifanya hivyo kama njia ya kuwapumbaza Watanzania. Tuna sababu gani ya kuwa na Wizara ya Uchukuzi?

Mheshimiwa Rais, ni kweli kwamba siku zako za kuendelea kushikilia nafasi uliyonayo zinazidi kuyoyoma. Sidhani kama kwa muda uliobaki unaweza kufanya maajabu ili kunyoosha haya ninayojaribu kuyaainisha hapa.

Muda hautoshi, lakini bado hujachelewa sana. Umeweza kwenye Katiba. Umeweza kwa Chuo Kikuu cha Dodoma. Bila shaka bado unaweza kuthubutu kufanya jambo au mambo kubwa ya maana zaidi. Hili la reli ni miongoni mwa hayo.

Angalia majirani zetu Wakenya. Wanajenga Bandari ya Lamu kwa kutumia dola bilioni 23 za Marekani. Mradi huu unatajwa kuwa mkubwa kabisa katika Afrika.

Wanajenga ‘Kigamboni’ ya ajabu kabisa huko kwao, wakati sisi hapa tumebaki kujadili nani anataka kuwa rais! Nani gamba! Wanajenga Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Taita. Hapa ni wazi kuwa hakuna mtalii atakayetua KIA.

Wanajenga “flyovers” nyingi, kubwa na nzuri kabisa katika Jiji la Nairobi. Wanafanya mambo makubwa makubwa ilhali sisi tukiwa tumeganda kwenye mijadala isiyokuwa na maana, tukichonga midomo asubuhi hadi asubuhi.

Angalia, Wanyarwanda wameamua kufundisha lugha ya Kichina katika nchi yao. Watoto wa Rwanda muda si mrefu watakuwa wafanyakazi kwenye kampuni na ofisi za Wachina hapa Afrika na duniani.

Watakuwa wanazungumza Kichina, Kifaransa, Kiingereza, Kinyarwanda, Kiswahili, Kibelgiji na lugha nyingine nyingi. Sisi hapa tumebaki kurundika mabango ya kijinga kwenye nguzo za umeme tukiwasoma matapeli wanaoleta mvuto wa kimapenzi, kupandishwa vyeo, kufufua waliokufa, kuleta bahati na ujinga wa kila namna.

Majirani zetu wanaboresha shule zao ili watoto wapate elimu nzuri. Wanahakikisha vyuo vinakuwa vingi na ubora wake unakuwa wa hali ya juu. Sisi hapa tumebaki kuwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi isiyojua walimu gani wako hai, wangapi wamestaafu au kufariki dunia. Kama unashindwa kutambua walimu wako waliofariki dunia au kustaafu, utaweza kweli kuwa na uwezo au akili ya kujenga maabara?

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imekomaa kusajili makanisa ya matapeli. Makanisa yenye maaskofu matapeli wanaodai sadaka kwa M-Mpesa, Tigo Pesa na kadhalika. Maaskofu wauza mihadarati! Matapeli wanaopanga viti katika makanisa kulingana na ukwasi wa mtoa sadaka! Haya yanafanywa ilhali tukiwa na Rais na watendaji waliokaa tuli kana kwamba hawaoni kuwa ni hatari kwa taifa.

Mgambo wanahangaika na kina mama wauza mihogo kwenye masinia mitaani, huku polisi wakiwasindikiza majambazi na wapora rasilimali za nchi.

Tuna mamilioni ya wanafunzi wanaokosa usafiri, ilhali tukiwa na kundi dogo la watoto na wake wa viongozi wanaopanda Land Cruiser VX V8 kwa ajili ya kupelekwa na kutolewa saluni. Tuna mamilioni ya watu wanaokufa kwa kukosa huduma za tiba kwa sababu hospitalini hakuna dawa. Dawa zote zinachukuliwa na viongozi na watumishi wa zahanati, hospitali na vituo vya afya.

Dhuluma hii imempa umaarufu usio rasmi Babu wa Loliondo. Wengi wanakwenda Loliondo si kwa sababu nyingine, bali kwa kushindwa kupata tiba kwa bei nafuu katika sehemu zetu za kutolea huduma.

Hili linachangia ushirikina na mauaji katika jamii. Watu wanaugua maradhi ya kawaida, wanakosa dawa, wanaishia kushikana uchawi na hatimaye kinachotokea ni mauaji.

Mheshimiwa Rais, nayasema haya kwa uchungu kwa sababu nchi yetu haiashirii hatima njema. Senegal lilikuwa taifa la kusifika kwa amani na utulivu. Kinachoendelea huko tunakijua.

Mataifa mengi yaliyoingia kwenye matatizo yamefikia hali hiyo kutokana na uongozi legelege, uongozi ulioridhika, uongozi unaofukuza wapigakura barabarani ili wakubwa wapite na vimulimuli, uongozi ambao hauwajali makabwela.

Nihitimishe kwa kusema kwamba dalili ya mvua ni mawingu. Mgongano wa kauli za viongozi wa Serikali, mgongano wa mihimili katika nchi yetu na shutuma zinazotoka kila kona juu ya viongozi wetu, ni dalili ya pambazuko.

Kuwakosesha wananchi uongozi mzuri ni dhuluma. Msomaji mmoja ambaye ndugu yake kauawa, lakini vyombo vya sheria vya kidunia vimewaachia wauaji, amenukuu maneno mazuri katika Biblia Takatifu. Amemlilia Mungu (soma toleo lijalo).

Maneno hayo kutoka Hakakuki 1: 2-4 yanasomeka, “Ee Bwana hata lini wewe usitake kusikia? Nakulilia kwa sababu ya udhalimu...maana uharibifu na udhalimu u mbele yangu; kuna ugomvi na mashindano yatokea. Kwa sababu hiyo sheria imelegea, wala hukumu haipatikani; kwa maana watu wabaya huwazunguka wenye haki; kwa sababu hiyo hukumu ikipatikana imepotoka.

Manyerere
0759 488 955
manyerere@hotmail.com

1 comment:

  1. Big upp Manyere, msg imetulia sana sana naungana nawe ktk hoja, imefikia hatua huduma ya afya inatutisha sana sisi watu wa chini yaani tusiotoka ktk familia za wenye uwezo au za viongozi, mfano eti mtu unakuta unaumwa unapewa rufaa nenda Muhimbili sababu hospitali za mikoan hazina baadhi ya vipimo vikubwa vya muhimu kuweko mahospitalini, haya unafika Muhimbili unaambiwa uende Aghakan kupima vipimo hivyo, haya bei ya vipimo hivyo ni kubwa ajabu. dah jaman kwa nini serikali isinunue hivyo vipimo ikaviviweka kwa hospital zote ili kila raia aweze pata vipimo kwa uhakika na urahisi? hili linawezekana kama serikali ikiamua kuacha nunua magari ya gharama ya viongozi ktk kipindi cha hata miaka miwili kwa kuanzia

    ReplyDelete