Monday 7 November 2011

BEI YA MAFUTA YAPANDA TENA



MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imetangaza kupanda kwa bei ya mafuta kuanzia jana. Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkuu wa Idara ya Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo alisema petroli imepanda kwa Sh49.17, dizeli Sh2.69 na mafuta ya taa yamepanda kwa Sh19.43.

Kutokana na bei hizo mpya, petroli itauzwa kwa Sh2,043, dizeli Sh1, 983 na mafuta ya taa yatauzwa kwa Sh 1,975 kuanzia leo. Kaguo alisema kupanda kwa bei hizo kunatokana na kuongezeka kwa bei ya bidhaa hizo katika soko la dunia.

“Petroli imeongezeka kwa asilimia 2.55 kwa lita, dizeli imepanda kwa asilimia 0.14 wakati mafuta ya taa yamepanda kwa asilimia 1.03 katika soko hilo,” alisema Kaguo.

Kwa upande wa bei ya jumla, Kaguo alisema petroli itauzwa kwa Sh 1,975.64 wakati dizeli itauzwa Sh1,915.64 na mafuta ya taa Sh1,907.47.

Alisema kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ilimradi bei hizo ziko chini ya bei ya kikomo.
Alisema vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana na yakionyesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika.

Aliwataka wanunuzi kuhakikisha wanapata stakabadhi ya malipo inayoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.Kaguo alisema stakabadhi hiyo itatumika kama kidhibiti cha mnunuzi wa mafuta endapo mteja atakuwa ameuziwa mafuta yenye kiwango cha ubora usiofaa.

Katika hatua nyingine, mamlaka hiyo imesema hakuna mgomo wa wauza mafuta kama ilivyodaiwa.
“Hizi ni njama za watu wachache wanaotaka kuvuruga Bunge linaloanza ili mambo yaliyopangwa yasijadiliwe badala yake wajadili suala la mafuta,” alisema Kaguo.

Alisema baadhi ya watu walisambaza ujumbe kwa njia ya mtandao uliosomeka kama: “Kutakuwa na mgomo wa mafuta kwa siku nne mfululizo, Dola itapanda kwa Sh2,000 na vituo vya kuuzia umeme wa LUKU vitakuwa na tatizo la mtandao.”
Maeneo mengi jana hayakuwa na petroli. Kaguo alikiri kukosekana kwa nishati hiyo katika baadhi ya vituo na kusema kuwa hiyo imetokana na uvumi huo.

Hata hivyo, alisema nchi inayo akiba ya kutosha kwa aina zote za mafuta na kwamba akiba iliyopo ni lita milioni 152 ambazo zinaweza kutosheleza mahitaji kati ya siku 10 hadi 52. Mahitaji ya mafuta nchini ni lita milioni tano kwa siku.
Mbali na akiba hiyo, alisema meli nane ziko bandarini moja ikiendelea kushusha mafuta ya dizeli na petroli na meli zinatarajia kumaliza kupakua mafuta mwishoni mwa mwezi huu

mwananchi

No comments:

Post a Comment