Friday 11 November 2011

MANENO YA MWANANCHI

Bunge letu sasa limekuwa ‘Bunge maslahi’  

TUMEFADHAISHWA sana na habari kwamba, badala ya kutumia muda wa vikao vya Bunge kutafuta jawabu la matatizo lukuki yanayowakabili wananchi hivi sasa, wabunge wa Bunge la Muungano juzi walipoteza muda mwingi kudai maslahi yao, wakimtaka Spika Anne Makinda kuhakikisha Serikali inapandisha viwango vya posho na mishahara yao.
Bila kujali hali mbaya ya uchumi wa nchi yetu na ukweli kwamba wananchi wengi mijini na vijijini sasa wanalia na kusaga meno kutokana na ukali wa maisha kiasi cha kuhangaika kupata angalao mlo mmoja kwa siku, wabunge waliweka kando tofauti za vyama vyao na wakapaza sauti kwa pamoja kwa kusema viwango vya posho na mishahara yao hivi sasa vimepitwa na wakati, hivyo viongezwe.
Suala la maslahi ya wabunge lilichukua sehemu kubwa ya mjadala ndani ya kikao hicho cha juzi, huku baadhi ya wabunge wakitaka wenzao wanaopinga nyongeza za posho na mishahara wapuuzwe. Hivi sasa posho na mshahara wa mbunge kila mwezi ni zaidi ya Sh7 milioni, kiwango ambacho wabunge wanadai hakilingani na kazi wanazofanya.
Suala la malipo, hasa ya posho liliibuka kwa mara ya kwanza wakati wa Mkutano wa Bunge la Bajeti miezi miwili hivi iliyopita kwa hoja ambayo chimbuko lake ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ambaye alisusia posho za vikao kwa kusema siyo sahihi kwa wabunge kulipwa posho wakati tayari wanalipwa mishahara kwa kazi hiyo. Wabunge wengi walipinga msimamo huo kwa kudai kwamba wanaokataa posho wanavyo vyanzo vingine vya mapato.
Kikao cha juzi kilionyesha picha na taswira halisi ya wabunge wetu wanaounda Bunge la Kumi, kwani msimamo wao wa kudai maslahi makubwa zaidi katikati ya umaskini wa kutisha unaowakabili wananchi unatia shaka kama kweli wabunge hao wanaguswa kwa aina yoyote na mateso waliyomo wapigakura ambao ndiyo waliwapeleka bungeni.
Madai yao kwamba maslahi wanayopata hayalingani na wanayopata wenzao katika nchi jirani ni ya kipuuzi kwa sababu wanashindwa kutambua kwamba uchumi wetu umo katika chumba cha wagonjwa mahututi kinyume na ilivyo kwa majirani zetu. Uchumi wa Kenya, kwa mfano umesimama juu ya msingi imara wa sekta za utalii na viwanda ambazo zinaingiza fedha nyingi za kigeni, wakati hali ni tofauti hapa nyumbani kutokana na kuuza nje bidhaa kidogo, huku tukiingiza bidhaa nyingi nchini, tena za kipuuzi.
Ni aibu iliyoje kwa wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi kufanya vitendo vya kuwasaliti. Katika kutoa hoja ya kupandisha viwango vya posho na mishahara, mmoja wa wabunge juzi alitoa kioja cha mwaka aliposema amepata mialiko 26 ya kwenda kuchangia ujenzi wa shule na shughuli nyingine za maendeleo katika jimbo lake na kwamba shughuli hizo zinamuhitaji atoe fedha kama mbunge, huku akiuliza fedha hizo atazipata wapi? Lakini kama walivyo wabunge wengi, hakutaka kuongelea matumizi ya fedha za Mfuko wa Jimbo ambazo wamepewa wabunge wote wanaowakilisha majimbo.
Tatizo tunaloliona hapa ni kwamba Bunge limeishika Serikali mateka na limejipa mamlaka makubwa na kujiweka juu ya mihimili nyingine ya Dola. Ndiyo maana, tofauti na Mahakama, Bunge linajiamulia masuala ya fedha na Serikali inalazimika kutoa fedha hizo, kwani isipofanya hivyo Bunge linalo fimbo ya kuiadhibu.
Tunawashauli wabunge watambue kwamba jukumu lao siyo kugawa fedha kwa wananchi, bali kuwaongoza na kuwaonyesha njia ya kujiletea maendeleo. Sisi tunadhani kuwa, kudai kupandishiwa posho na mishahara wakati hospitali hazina dawa; watoto wetu wanakaa chini mashuleni bila walimu wa kutosha na vifaa vya kufundishia;
ujenzi wa kilomita 2,405 za barabara ukiwa umesimama kutokana na makandarasi kudai malimbikizo ya Sh287 bilioni; mahakama zetu zikiwa hoi kutokana na uhaba wa fedha; na wanafunzi vyuo vikuu wakiwa hawapati mikopo ya elimu, ni kukosa uzalendo na kuendekeza ubinafsi kwa kiwango cha ajabu.

No comments:

Post a Comment