Thursday 3 November 2011

JIDE ALAZWA UFARANSA


Sifael Paul na Musa Mateja NYOTAmwenye heshima tele ndani ya muziki wa Bongo Fleva, Judith Wambura Mbibo ‘Jaydee’ amelazwa katika hospitali moja iliyopo jijini Paris, Ufaransa kwa ugonjwa ambao mwenyewe anauita ni wa heri, ingawa baadhi ya wadau wanasema ‘amenasa’, Amani linashuka kikamilifu.

Kwa mujibu wa mtandao wake, Lady Jaydee au Jide ambaye ni mke wa ndoa wa aliyekuwa mtangazaji ‘babkubwa’ wa Clouds FM, Gardner G. Habbash, alilazwa wiki iliyopita na juhudi za madaktari zilikuwa zikiendelea kumuweka sawa.

NI UJAUZITO KWELI?
Baadhi ya watu waliotembelea mtandao huo na kusoma maelezo yake, waliweka maoni yao na kumpongeza kwa kulazwa wakibashiri kuwa ugonjwa huo wa ‘heri’ ni ujauzito ingawa Jide hajakiri wala kukutaa.

Maelezo katika mtandao wake ambayo aliyaandika mwenyewe yalisomeka hivi:
“Nashukuru kwa kuwa natoka leo Jumamosi (Oktoba 29, 2011) hospitali.

“Nashukuru kwa pongezi mlizozitoa bila hata kujua kama hicho mnachonipia hongera kipo au hakipo, ila si mbaya. Huwezi kuzuia mtu akidhania kitu lakini naona mnafikiria hivyo kwa ajili ya mapenzi yenu kwangu, nashukuru pia kwa kuwa ni mapenzi mema.”

Jide akaendelea: “Nitaendelea kushukuru mwezi wote wa Novemba na siku zote za maisha yangu kwa nilipotoka mpaka nilipo hivi sasa, wengi wameishia njiani, wengine wamekata tamaa, lakini mimi namshukuru Mungu ananipa nguvu kila siku.

“Nashukuru fans (mashabiki) wanaonipenda kiukweli, nashukuru na wengine wanaojaribu kutonipenda, naamini ipo siku watagundua hakuna sababu ya kufanya hivyo kwani kumchukia mtu ni sawa na kuwa umeshamuua. Sasa je! Nani anataka kuendelea kuwa mmoja wa wauaji?
“…nawaombeni msubiri kusikia kutoka kwangu direct (moja kwa moja) na siyo magazeti, blog za uzushi wala minong’ono,” alimaliza kujieleza Jide.

AMANI LAMSAKA GARDNER ATHIBITISHE
Ili kujua kwa undani ugonjwa wa ‘heri’ wa msanii huyo, Timu ya Waandishi wa Amani ilijikusanya Jumatatu ya wiki hii na kuingia mitaani kumsaka Gardner ambaye angeweza kufunguka.

SAA 5:23 ASUBUHI- NYUMBANI LOUNGE
Breki ya kwanza ilikuwa kwenye sehemu yao ya biashara katika Mgahawa wa Nyumbani Lounge uliopo Ada Estate, Kinondoni, Dar.
Waandishi walimuweka ‘mtukati’ mrembo mmoja aliyekuwa akifanya usafi sehemu hiyo na kumuuliza alipo Gardner ambaye ni meneja wa mgahawa huo.

“Mh! Mi sifahamu, sijamuona siku mbili hizi, sasa sijui yuko wapi?” alijibu mhudumu huyo.
Hata hivyo, upelelezi wa kina katika eneo hilo ulionesha kuwa, mara nyingi Gardner hupendelea kutembelea kwenye Pub ya Jack’s Masaki.

SAA 6:35 MCHANA-JACK’S PUB
Amani lilitua Jack’s Pub na kuzungumza na mhudumu mmoja ambaye alikiri kumfahamu Gardner, lakini akasema kwa siku kadhaa hajamuona.

SAA 7:47 MCHANA-KIMARA TEMBONI
Gazeti hili liliwasili nyumbani kwa wanandoa hao, Kimara Temboni, Dar na kukutana na geti kubwa likiwa limefungwa. Licha ya kugonga kwa nguvu geti hilo, ndani ya nyumba hakukusikika mlio wowote, hata wa sufuria kuanguka achilia mbali maji kumwagika sakafuni.

SAA 8:35 MCHANA-NYUMBANI LOUNGE TENA
Timu yetu ilirudi Nyumbani Lounge kwa kuamini pana siri kubwa ya alipo Gardner.
Safari hii mfanyakazi mmoja wa kike ambaye aliomba jina lake lisichorwe gazetini aliweka wazi kama ifuatavyo:
“Gardner hayupo, amesafiri, si mnaona gari lake (Nissan Murano, namba T 375 BDX) lile pale?”

Amani: Oke, tutakulinda dada‘etu, amesafiri kwenda wapi?
Mfanyakazi: Mh! Aliko mke wake, wapi vile?

Amani: Ufaransa?
Mfanyakazi: Eee, huko huko. Aliacha majukumu akaondoka hapa ghafla tu.

Amani: Ahsante anti, kwa heri.
Mfanyakazi: Poa. Hamuungishi japo kwa kununua maji ya kunywa jamani?

Amani: Tehe! Tehe! Tehe! Siku nyingine.
Mwanamuziki huyo anatarajiwa kurudi Bongo Februari, 2012.

HERI JUU YA HERI
Kama walivyotoa maoni wadau wa Jide kwamba, ugonjwa wake wa ‘heri’ ni ujauzito. Ikiwa ni kweli, dawati la Amani nalo linamtakia kila la kheri msanii huyo juu ya hali hiyo.

MAKABRASHA YA AMANI
Katika makabrasha ya gazeti hili, mara kadhaa nyota huyo aliwahi kuripotiwa kunasa mimba, habari ambazo amekuwa akizikanusha mara kwa mara. Wadau wanasubiri ufafanuzi wake wa safari hii.

habari toka.globalpublishers

No comments:

Post a Comment