SAKATA la mtuhumiwa, Joshua Mulundi, anayekabiliwa na kesi ya kumteka na kutaka kumsababishia kifo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, sasa limechukua sura mpya baada ya kudaiwa kuondolewa kiaina katika mahabusu ya Gereza la Keko na kufichwa katika selo ya adhabu.

Chanzo chetu ndani ya mahabusu hiyo kilieleza kuwa mshitakiwa huyo ambaye ni raia wa Kenya, alikuwa ameanza mgomo wa kutokula, kisha kupanda juu ya paa la gereza hilo, akitishia kujiua endapo wapelelezi wa kesi yake hawatafanya juhudi za kumleta Dk. Ulimboka ili amtambue.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, Mulundi baada ya kukaa juu ya paa na kunyeshewa mvua kwa saa kadhaa akiwa na mahabusu wenzake, uongozi wa gereza ulitumia nguvu za ziada kuwashusha watuhumiwa hao kwa nguvu huku mtuhumiwa huyo akipatiwa kipigo kikali kabla ya kuhamishwa.

Kwamba, Magereza waliwaleta baadhi ya askari wake wa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Fujo, ambao inasemekana walimcharaza Mulundi na wenzake na kisha kumwondoa ndani ya mahabusi hiyo na kupelekwa sehemu isiyojulikana.

Tanzania Daima ilifanya juhuzi za kuzungumza na msemaji wa Magereza, Omary Mtiga, lakini hakuwa na ushirikiano wa kutosha, badala yake alitoa maneno ya kejeli kwa gazeti hili kuwa linaandika habari za kizushi.

“Mimi ndiye msemaji wa Magereza, huo umbea unaopenyezewa na hao wanaojiita vyanzo vya ndani, si ‘official’ (rasmi). Mulundi anachotaka ni kuonana na hakimu kwa tarehe aliyopangiwa,” alisema.

Mtiga bila hakukubali wala kukataa, alipoulizwa uongozi wa gereza hilo umemsaidiaje kufikia anachokitaka kama mahabusu mwenye haki zake, alijibu kwa hasira kuwa hayo ni mambo ya ndani ya utawala.

“Wewe kama unataka kufanya uchunguzi wa kina wa jambo hili unalolihangaikia, njoo ufungwe gerezani, utapata yote. Hayo unayoniuliza ili niseme amepelekwa wapi ni mambo ya ndani, hayawahusu kuandika,” alisema.

Mtiga ambaye alikuwa akizungumza kwa mkato kwenye simu yake ya kiganjani, alihoji kama mwandishi anaweza kuandika masuala ya mgogoro wa ndoa yake hadharani na kusisitiza kuwa; ‘Hayo mambo ya kutafuta habari za hovyo hovyo yaacheni.”

Alisema kuwa anashangazwa kuona Tanzania Daima lilivyolivalia njuga sakata hilo wakati mshitakiwa Mulundi ni mahabusu kama wengine, asiye na sifa yoyote ya pekee.

Mtiga licha ya kusisitiza kuwa mahabusu huyo hajagoma kula, bado hakuweza kuthibitisha amehamishiwa gereza gani, akisema hiyo ni siri ya utawala.

Gazeti dada na hili la Tanzania Daima Jumapili iliyopita lililitoboa siri jinsi Mulundi anavyoitaka serikali imlete mbele yake Dk. Ulimboka ili afanyiwe gwaride la utambulisho kubaini kama alihusika katika tukio la kumteka.

Imeelezwa kuwa amechukua uamuzi huo mgumu baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa kesi ambayo tangu Julai 3, mwaka jana bado iko kwenye hatua ya upelelezi na hajui utakamilika lini.

Askari mmoja wa Jeshi la Magereza kutoka ndani ya gereza hilo alikiri kuwa mtuhumiwa huyo amegoma na usiku wa kuamkia juzi alishinda juu ya paa la gereza hilo akinyeshewa mvua.

Habari zaidi zinasema kuwa ndugu wa mtuhumiwa huyo ambaye hana wakili mahakamani, wamewasili kutoka nchini Kenya kwa ajili ya kutoa msaada wa kisheria.

Kwa mujibu wa ndugu hao, hadi sasa hawaoni maendeleo ya kesi hiyo kwani kila ikifika mahakamani upande wa mashitaka hutoa hoja ya kutaka iahirishwe kwa madai kuwa upelelezi haujakamilika.

Hata hivyo Mulundi anadai kuwa amewahi kutoa malalamiko kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), akiiomba serikali imlete mbele yake Dk. Ulimboka ili amtambue na kuhakikisha upelelezi wa kesi hiyo unafikia tamati.

Dk. Ulimboka ambaye alikuwa kinara wa mgomo wa madaktari uliotikisa nchini kwa wakati tofauti mwaka jana; alitekwa, kuteswa, kupigwa hadi kung’olewa meno na kucha na kisha kutupwa katika msitu wa Mabwepande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Baada ya tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alitangaza kuunda tume ya wataalamu kutoka ndani ya jeshi hilo iliyoongozwa na ACP Ahmed Msangi.

Hatua hiyo ilikuja baada ya Dk. Ulimboka mwenyewe kuwataja baadhi ya watu aliodai kuwa ndio walihusika kumteka na kumtesa, lakini hadi sasa Mulundi ndiye mtuhumiwa pekee aliyekamatwa.

Hata hivyo tume hiyo haijawahi kutoa ripoti yake kama Kova alivyoahidi pamoja na kwamba hata majeruhi mwenyewe, Dk. Ulimboka hajahojiwa, huku vigogo wa jeshi hilo wakitupiana mpira kuhusiana na sakata hilo.

Hivi karibuni jeshi hilo kupitia kwa msemaji wake, Advera Senso, limekanusha kuwapo kwa tume hiyo, likisema walioteuliwa ni polisi ambao watafanya kazi za kiuchunguzi kwa taratibu za polisi.

Kauli ya Senso ilipingana na ile ya Kova, ambaye hivi karibuni alikiri kuwapo kwa tume hiyo, lakini akasema hawezi kulizungumzia suala hilo kwa vile taarifa zake alishazipeleka kwa wakubwa wake makao makuu baada ya kukamilisha wajibu wake.

Wakati vigogo hao wakisigana katika kulifafanua sakata hilo, Dk. Ulimboka mara kadhaa amekuwa akieleza kuwa yupo tayari kutoa maelezo yake kama kutakuwa na tume huru ambayo si hiyo iliyoundwa na polisi.

Chanzo: Tanzania Daima