Wednesday 2 January 2013

MVUA KUBWA YASABABISHA MAAFA SINGIDA


Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida (wa kwanza kushoto mwenye fimbo) akiangalia daraja lililobomoka la Munung’una lililopo barabara kuu ya Singida – Mwanza eneo la  kijiji cha Msisi wilaya ya Singida.
Mhandisi wa TANROADS mkoa wa Singida,Yustaki Kangole akiwaelekeza jambo wahandisi wa kampuni ya CHICO iliyojenga daraja lililobomokajuzi la kijiji cha Msisi wilaya ya Singida.Daraja hilo lililopo kwenye barabara kuu ya Singida – Mwanza,limebomoka baada ya kuzidiwa na maji ya mvua kubwa iliyonyesha siku moja kabla ya mwaka mpya.
Baadhi wa wasafiri waliokwama baada ya daraja la Munung’una lililopo katika barabara kuu ya Singida – Mwanza eneo la kijiji cha Msisi wilayani Singida, kubomoka juzi kufuatia mvua kubwa zilizonyesha mkoani Singida. (Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu
Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani Singida,zimeendelea kuleta maadhara makubwa ikiwemo kuvunja daraja na barabara kuu ya Singida – Mwanza na kuua raia moja  wa nchini China.
Juzi mvua hizo zilisababisha familia ya watu wanne ya wilaya ya Mkalama mkoa wa Singida, kupoteza maisha baada ya kuangukiwa na nyumba ya tembe.
Mvua hizo kubwa  zilizonyesha kuanzia  mwaka mpya (1/1/2013) saa nane mchana hadi saa 12.30 jioni zilisababisha daraja la Munung’una lililopo katika kijiji cha Msisi wilayani Singida, barabara kuu itokayo Singida kuelekea mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani za Kongo, Burudi, Rwanda na Uganda, kubomoka na kusabaisha shimo kubwa.
Kubomoka kwa daraja hilo kumechangia foleni kubwa ya magari yanayokadiriwa kuwa ni zaidi ya mia tatu. Pia mawasiliano kati ya mikoa mbalimbali ikiwemo  ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani yamekatika.
Mmoja wa madereva walioathirika na kubomoka kwa daraja hilo, George Medadi, aliyekuwa akitokea Mwanza akirudi jijini Dar-es-salaam, alisema kubomoka kwa daraja hilo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na kujengwa chini ya kiwango.
“Wenyeji wa hapa wametueleza kuwa kalvati zilizotumika ni zile za zilizowekwa wakati Nalaila Kiula alipokuwa Waziri wa Ujenzi. Kampuni ya CHICO iliyojenga barabara hii kwa kiwango cha lami waliyatumia makalivati hayo hayo na walichofanya ni kulundika udogo juu tu,” Medadi alisema.
Naye dereva Iddi Mussa alisema kuwa barabara nyingi zinazojengwa na kampuni za kichina zimekuwa hazisimamiwi ipasavyo kitendo kinachochangia kuharibika haraka na kuisababishia serikali kuingia hasara kubwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mwalimu Queen Mlozi alisema kwa kuanzia wameimarisha ulinzi katika eneo hilo pamoja na kufungua kituo kidogo cha kutolea huduma ya afya na kudhibiti uwezekano wa kutokea kwa magonjwa ya mlipuko.
“Pia tumefungua barabara ya Singida-Ndago –Misigiri kwa ajili ya kutumiwa na mabasi ya abiria na yale yenye uzito chini ya tani kumi. Vile vile tunaangalia uwezekano wa kuangalia ni namna gani watu waliokwama wanapata chakula,” alisema.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Singida, Mhandisi Yustaki Kangole, ambaye alifika na wahandisi wa kampuni ya CHICO, alisema kuwa wamekubaliana na CHICO kwamba  wafukie shimo hilo kwa vifusi vya mawe makubwa ili barabara hiyo ianze kutumika mapema iwezekanavyo.
“Kwa sasa tunafanya kazi hii ya muda na baada ya eneo hili kukauka ndio ukarabati mkubwa utafanywa ili kuimarisha barabara hii muhimu kwa uchumi wa taifa,” alisema Mhandisi Kangole.
Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Edward Ole Lenga amesema kuwa raia moja wa China amefariki dunia baada ya gari lake kusombwa na maji ya mto jirani na kijiji cha Gumanga.
Alisema Mchina huyo ambaye jina lake bado halijatambuliwa hadi sasa, alisombwa na maji ya mto juzi  majira ya jioni wakati akikatisha mto wa kijiji cha Gumanga wilaya ya Mkalama. Ndani ya gari hilo alikuwa na mtoto wake ambaye alinusurika kufa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Linus Sinzumwa, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa taarifa zaid atatoa baadae.

Chanzo:moblog

No comments:

Post a Comment