Yapata
wiki tatu sasa tangu msanii mwenzangu Steven Kanumba aage dunia, na
kama ilivyo kwa kila kitu kinapotokea huandamana na kila aina ya maneno
na hisia mbali mbali kutokana na mitazamo ya watu kupishana kuhusiana na
jambo husika. Kulingana na muktadha huo, msiba wa Steven Kanumba
umekumbwa na maneno na hisia kama hizo, hususan mazingira ya kifo chake;
kinachosikitisha zaidi watu wengi (ambao wanajitambulisha kama wapenzi
wa Kanumba), na baadhi ya vyombo binafsi vya habari vimekuwa
vikinihusisha na kifo hicho, kwa kusema kwamba kwa njia moja au nyingine
ninahusika na mauaji ya Steven Kanumba. Kwa muda wote huo tangu msiba
ulipotokea mpaka leo hii nashika kalamu kujaribu kuyaweka sawa na
kuondosha hisia chafu katika fikra za watu, nimekuwa nikipitia katika
wakati mgumu sana kwa jinsi ambavyo nimekuwa nikinyooshewa vidole kila
upande nikihusishwa na kifo hicho, kiujumla nimezingatia maoni ya
wapenzi ya mashabiki wangu wakinitaka kuwa na subira, ila
kuna ukweli usemao kwamba, uongo ukirudiwa sana jamii huusadiki na
kuuona ukweli, nimeona nisikae kimya ila niweke sawa hili kwamba
sihusiki na kifo cha Steven Kanumba.
Nasema
wazi kwanza sihusiki kabisa na kifo cha Kanumba kwanza kwa kuzingatia
mazingira yenyewe ya kifo kilivyotokea. Wakati kifo hicho kinatokea,
nilikuwa sehemu nyingine kabisa na mimi nilikuwa mtu wa tatu kutaarifiwa
kwamba Kanumba amepatwa na mkasa ambao baadae ulisababisha kifo chake.
Na na hata nilipofika katika hospitali ya Muhimbili (tofauti na watu
wanavyodhani kuwa nilifika nyumbani kwake; ukweli mimi nilimkuta tayari
amepelekwa Muhimbili), nilikuta tayari alikuwa ameshafariki ndio maana
hata Polisi wanaohusika na usalama wa raia, si tu kwamba hawakuniweka
chini ya ulinzi, sikuitwa hata kuhojiwa kwa sababu hakuna mazingira
yoyote yanayonihusisha mimi na kifo hicho.
Pili,
watu wanahusisha tofauti za kibinadamu zilizokuwepo baina yetu na kifo
hicho, nasema hii sio sahihi kwa sababu kwanza ni kawaida kwa binadamu
kutofautiana, isipokuwa kwetu sisi baadhi ya vyombo vya habari vilikuwa
vinakuza kwa sababu nisizozijua, hivyo jamii ikachukulia kuwa tofauti
zile ni uadui kitu ambacho sio sahihi, kwani sisi hatukuwa watu pekee
tunaotofautiana kwani huu ni mwenendo wa kawaida wa dunia; hivi jana
tumeshuhudia Waziri mmoja akieleza bayana katika mkutano na waandishi wa
habari kuwa na tofauti na naibu wake, lakini hatuajasikia ikiandikwa
wana ‘bifu’ bali imetafutwa lugha nzuri ya kupamba tofauti hizo, kwa
kuwa waliohusika ni waheshimiwa, ila kwa wengine kutokana na sababu
tusizozijua, inaonekana kama ni haki yetu kuandikwa vibaya.
Kinachosikitisha, kwa nini jambo hili linachukuliwa kwa mkazo mkubwa
sana, kwani hatujawahi kusikia watu wakiwa wanatofautiana na ndugu jamaa
hata na marafiki zao na inaonekana kawaida tu? Kwani vyombo vya habari
havikuwahi kuandika kuwa marehemu Steven Kanumba alikuwa na tofauti na
baba yake, na yeye mwenyewe alitamka hivyo katika vyombo vya habari,
mbona wameliongea bila kuongeza chumvi, na jamii inaona kuwa ni jambo la
kawaida la kibinadamu.
Pengine
watu wanaojaribu kuongea hayo, hawajui mimi na Steven Kanumba tumetoka
wapi? Sisi si watu tuliokutana barabarani, tuna historia katika kazi
yetu ya sanaa na pia katika maisha maisha yetu. Mwanzoni kabisa, mimi
ndiye niliyempokea Kanumba pale Kaole na ndiye niliyemfundisha sanaa
pale (nadhani watu wanakumbuka tamthiliya za wakati huo ITV) na baada ya
hapo tulienda pamoja katika kampuni ya Game 1st Quality
pamoja na tukafanya filamu kama Johari, Sikitiko Langu, Dangerous Disire
na nyinginezo, na tuliendelea kuwa pamoja katika kampuni hiyo mpaka
tulipofanya filamu ya Oprah mwaka 2008 ambapo niliingia rasmi kufanya
kazi za kampuni yangu, lakini tuliendelea kuwa pamoja hata wakati
nikiendelea na kazi za kampuni yangu. Pia mimi nilikuwa wa kwanza kuanza
kufanya kazi na Steps na baadae Kanumba alipoanza kufanya kazi zake
mwenyewe na kunikuta huko tuliendelea kuwa pamoja kama siku zote. Kitu
kikubwa kilichokuwa kinaendelea baina yetu, ni kwamba tulijenga
ushindani wa kuendeleza kazi mbele kwa kila mmoja akitoa kazi, mwingine
anamjibu, Isitoshe hata vitu
vyetu binafsi utaona kama kuna kufanana; kuna wakati Kanumba alinunua
Toyota Ruv 4 nyeusi mimi nikanunua ya kijani, aliponunua Harrier na mimi
nikanunua pia, na hata gari za hivi karibuni, ukitazama utaona kuwa
zinafana kwa karibu; hii ilikuwa ni kama maisha yetu, hatukuwa na uadui,
ilikuwa tunapeana changamoto za maendeleo.
Watu
wanaojaribu kuonesha kuwa tofauti zetu ilikuwa ni uadui, huwa hawajui
wapi tulikotoka ndio maana wanasema wasemavyo na katika kuthibitisha
kuwa tofauti hizo hazikufikia katika uadui, kuna watu ambao wanafanya
kazi nami katika kampuni yangu ya RJ ndio hao hao Kanumba alikuwa
anawatumia siku zote katika kazi zake, hata baada ya tofauti hizo hakuna
aliyekoma kufanya kazi na yeyote kati yetu. Hii inathibitisha kuwa
tofauti ilikuwa kati yetu kama binadamu, sio chuki za kimafanikio,
ingekuwa hivyo watu kama Junior Syaary ambaye mara nyingi hufanya final
editing katika RJ ndio huyo huyo alikuwa akifanya na Kanumba, Ally
Yakuti ambaye anaandika script za RJ, ndiye huyo huyo aliyekuwa
anaandika kwa Kanumba, Steven Shoo ambaye ni mtaalamu wangu wa light,
ndiye huyo huyo anayetumiwa na Kanumba na wengine wengi kama Juma
Chikoka aliyecheza kikamilifu katika filamu ya kijiji cha Tambua Haki,
ambaye pia anashiriki filamu nyingi za RJ, na wote hao, hawakuanzia kwa
Kanumba, wote wameanza kwangu mimi ndio niliompatia na hata baada ya
hayo yanayosemwa kuwa kuwa ni uadui, sikuwahi kuwakataza kufanya kazi na
Kanumba.
Tatu
kumtuhumu mtu kwa namna yoyote ile bila ya uthibitisho wa tuhuma hizo,
ni kosa kwa sheria za nchi na pia kama ni mfuasi wa dini yoyote ni
dhambi, kwani wakati ukisema hayo huku hujui uhalisia bali unasukumwa na
nguvu za hisia tu ni sawa na kumchafua mtu huyo katika jamii bila ya
kujua jamii inamchukuliaje. Napenda kusema wazi wazi kuwa, kwa kila
anayetekwa na wimbi hili, ajaribu kufikiria leo ipo kwangu mimi, kesho
inaweza kuhamia kwako, kwani mimi sio wa kwanza kufikwa na haya, inaweza
kukukuta hata wewe au ndugu yako, utajisikiaje.
Mwisho
kabisa napenda kumaliza kwa msemo usemao, ajidhaniaye amesimama,
aangalie asianguke, kwani kadri mambo haya yanavyoendelea, usidhani
yataishia kwangu, kwani mkono wa dhuluma haushii karibu, ukisikia jirani
anapiga kelele za mwizi, usilale kamsaidie, usiseme kuwa hatuhusiki
kwani hayupo kwetu, kesho utafikwa na wewe utakosa wa kukusaidia. cha
msingi kama tunampenda sana ndugu yetu ni kumuombea kwa Mungu, kwani
hatujui makao yake huko aliko, na sio kuunda vitu ambavyo kamwe hata
yeye angekuwa hai asingeviafiki.
MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU STEVEN KANUMBA MAHALI PEMA
PEPONI
MUNGU IBARIKI AFRIKA MUNGU IBARIKI TANZANIA