Monday 23 April 2012

lulu amepandishwa tena kizimbani leo,kesi imeahirishwa mpaka tar 7 may

Lulu akitoka mahakama ya Kisutu leo kurejeshwa Segerea
MWIGIZAJI nyota wa filamu Tanzania, Elizabeth Michael ‘Lulu’ leo amewatoa machozi baadhi ya watu waliohudhuria kesi yake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam.
Lulu mwenye umri wa miaka 17, anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya mwigizaji mwenzake, Steven Charles Kanumba, aliwasikitisha watu na baadhi kumwaga machozi, kutokana na jinsi alivyowasili Mahakamani hapo akiwa chini ya ulinzi mkali wa askari Magereza.
“Masikini biti anapata matatizo sasa, inatia huruma, nawaonea huruma wazazi wake, wanakosa raha sasa,”alisikika mtu mmoja akisema mahakamani hapo.
Pamoja na kufikishwa mahakamani hapo,
Hakimu Mkazi wa Mahakama Kisutu, Ritha Tarimo aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 7, mwaka kwa sababu upelelezi bado unaendelea.
Lulu anayekabiliwa na tuhuma za kumuua The Great Kanumba aliyefariki dunia, Aprili 7, mwaka huu nyumbani kwake Vatican, Sinza Dar es Salaam, hii ni mara ya pili kufikishwa mahakamani hapo.
Lulu aliyecheza filamu kadhaa na marehemu Kanumba waliyeibuka naye katika kundi la Kaole, Magomeni, hakutakiwa kutoa maelezo yoyote Mahakamani, kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.
Wakati kesi hiyo ikiwa katika hatua za mwanzoni, Polisi bado inaendelea na uchunguzi wake na baadhi ya watu wakiwemo wasanii wamekuwa wakihojiwa kulisaidia jeshi hilo upelelezi.
Taarifa za awali baada ya kifo cha Kanumba, zilisema kwamba mwigizaji huyo alifariki baada ya kusukumwa na Lulu nyumbani kwake Sinza Vatican, ambaye inadaiwa alikuwa mpenzi wake.
Inaelezwa baada ya tukio hilo, Lulu alikimbia nyumbani kwa Kanumba na mdogo wa Ther Great, Sethi Bosco akaenda kuchukua gari kumpeleka kaka yake hospitali ya Muhimbili, ambako alipofika iligundulika amekwishafariki dunia.
Sethi alikaririwa akisema kwamba siku ya tukio, Lulu alikwenda kwao usiku wa manane na alipofika yeye (Sethi) alimuacha aongee na kaka yake. Sethi alidai aliwaacha sebuleni akaingia chumbani kwake na baadaye akasikia wameingia chumbani (kwa Kanumba).
Sethi alisema baada ya muda alisikia kelele za dalili ya ugomvi na baada ya muda Lulu alitoka kumwambia (Sethi) juu ya hali ya Kanumba kubadilika na kuwa mbaya.
Sethi alidai aliposikia hivyo akashituka na kwenda chumbani ambako alimkuta kaka yake katika hali mbaya, povu likimtoka mdomoni hivyo kuchukua hatua ya kumuita daktari wake, kabla ya kumkimbiza Muhimbili.
Lulu alikamatwa asubuhi ya kuamkia siku ya tukio hilo, linalodaiwa kutokea usiku wa manane na kuwekwa kizuizini katika kituo cha Polisi Oysterbay, Kinondoni, Dar es Salaam.
Tayari baadhi ya wanaharakati wa haki za wanawake wamekwishatangaza azma yao ya kumsaidia Lulu katika kesi hii.
Miongoni mwao ni Mbunge wa Jimbo la Kawe, (CHADEMA), Halima Mdee.
Bado watu wanajiuliza maswali mengi kuhusu kifo cha Kanumba, mojawapo kama kweli Lulu anayedaiwa kumuuwa wakati wakigombana ‘ana ubavu’ huo.
Lakini pia, siku ya kifo cha Kanumba, inadaiwa alionekana katika ukumbi wa starehe, Club Maisha akinywa pombe.
Uchunguzi wa madaktari katika hospitali ya Rufaa ya Muhimbili ulisema pombe kali aina ya Jackie Daniels ilisababisha kifo cha mwigizaji huyo.  
Lakini baadhi ya vielelezo vilipelekwa kwa mkemia mkuu wa serikali, ili kutaka kujua kama msanii huyo aliwekewa sumu.
Kifo cha Kanumba kimewaumiza wengi, kwani msanii huyo alikuwa mahiri na kipenzi cha wapenzi wa filamu nchini.
Wapembuzi wa mambo wanasema huu ni msiba wa kwanza kuteka hisia za watu wengi zaidi, tangu kifo cha baba wa taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Oktoba mwaka 1999.

habari:dinamariosblog

No comments:

Post a Comment