Thursday 7 June 2012

BAJETI: Upinzani kulia na kodi ya mishahara, vyakula

WATAKA MISAMAHA YA KODI IPUNGUZWE, KUIBANA SERIKALI BUNGENI KUHUSU POSHO  Send to a friend
Wednesday, 06 June 2012 20:45
0digg
Fidelis Butahe na Raymond Kaminyoge
KAMBI ya Upinzani Bungeni imetoa mwelekeo wa bajeti mbadala yenye vipaumbele 10, ikilenga kufuta misamaha ya kodi na kupunguza kodi ya mishahara na mazao ya chakula ili kukabiliana na ugumu wa maisha.Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa kambi hiyo itaishinikiza Serikali kupunguza misamaha ya mbalimbali ya kodi kutoka asilimia tatu hadi moja ya Pato la Taifa, huku kodi ya mishahara ya wafanyakazi (Paye), ikipunguzwa kutoka asilimia 14 hadi tisa.

Tayari Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa ametangaza mwelekeo wa Bajeti Kuu ya Serikali ambayo itatumia Sh15 trilioni, huku ikiwa na maeneo saba ya vipaumbele ikiwamo miundombinu ambayo imegawanyika katika makundi manne ya reli, umeme, usafirishaji na uchukuzi.
Maeneo mengine ni maji salama, kilimo, viwanda, rasilimali watu, huduma za jamii, utalii, biashara ya ndani nje ya nchi na  huduma za fedha.

Vipaumbele hivyo kwa pamoja, vimetengewa Sh5 trilioni huku Sh10 trilioni zikiwa ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.

Zitto alisema hivi sasa misamaha ya kodi ni mikubwa, sawa na misaada yote kutoka nchi wahisani ambayo ni Sh1.03 trilioni.

“Tunataka misamaha ya kodi ipunguzwe hadi kufikia asilimia moja, hivi sasa misamaha hiyo inatolewa kwa wingi tena bila kuwa na sababu ya msingi,” alisema Zitto.

Alisema kambi hiyo ilitoa wazo kama hilo katika Bajeti ya mwaka 2011/12, lakini Serikali haikutekeleza, hivyo wataibana bungeni kuanzia wiki ijayo ili ieleze kwa nini haikutekeleza.
Kuhusu Paye kwenye mishahara ya wafanyakazi hasa wa kipato cha chini, alisema watashinikiza ishushwe hadi asilimia tisa ili kuwasaidia wafanyakazi wa kipato cha chini kubakiwa na angalau kiasi fulani cha mshahara, kitakachowasaidia kumudu kupanda kwa gharama za maisha.

Alisema kipaumbele kingine ni kufuta au kupunguza kodi kwenye bidhaa za vyakula kwa muda maalumu ili kushusha mfumuko wa bei, jambo ambalo litawezesha kushuka kwa bei ya bidhaa za vyakula.
“Kwa mfano, katika kipindi hiki ambacho bei ya mchele ni kubwa, turuhusu wafanyabiashara kuagiza mchele kutoka nje ya nchi bila kutozwa kodi ili wauze kwa wananchi kwa bei ya chini, suala hili nitalipigania bungeni,” alisema Zitto.

Alisema mfumuko wa bei kwa sasa ni asilimia 26, hivyo ni muhimu Serikali ikaruhusu wafanyabiashara kwa muda wa miezi mitatu kuagiza vyakula kutoka nje bila kodi.

Zitto alisema pia wanataka kuhakikisha fedha nyingi zinaelekezwa katika raslimali fedha hasa maendeleo vijijini ikiwa ni pamoja na kujenga barabara na umeme vijijini, hatua ambayo itasaidia wakulima kusafirisha bidhaa zao kwa bei ya chini.

“Tumependekeza zitengwe fedha za kutosha kwa ajili ya kukarabati reli ya kati na kufufua njia za reli zikiwemo za Tanga, Moshi na Arusha ili ziendelee kufanya kazi. Katika mpango huu zinahitajika Dola 200milioni,” alisema Zitto.

Alisema kipaumbele kingine ni kuongeza wigo wa Tozo la Ujuzi (Skills Development Levy) ili kuanzia waajiri wote, ikiwamo Serikali na mashirika ya umma, waanze kuilipa.

“Wigo wa tozo hili ukipanuka na kupunguza kiasi cha tozo hadi kufikia asilimia nne, sehemu ya fedha hiyo iende katika Vyuo vya Mafunzo na Ufundi Stadi (Veta) na sehemu nyingine iende Bodi ya Mikopo ili kukabiliana na tatizo la mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu,” alisema
Jambo jingine ambalo kambi hiyo itatilia mkazo ni kuongeza mapato ya ndani na kupunguza mikopo ya kibiashara kwa kuhakikisha mapato hayo yanafikia asilimia 20 ya pato la taifa.

Alisema hali hiyo itaongeza nguvu za kisheria na udhibiti ili Mamlaka ya Mapato Tanzania  (TRA), iweze kukusanya kodi zaidi kwenye kampuni za simu na katika shughuli za uchimbaji wa madini, mafuta na gesi.

“Kampuni nyingi za simu za mkononi hazilipi kodi kama inavyotakiwa, hivyo tunatakiwa kutafuta njia maalumu za kuzibana ili ziweze kulipa kodi kama inavyotakiwa,” alisema Zitto.
Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini (Chadema) na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (POAC), alitaja kipaumbele kingine kilichopendekezwa na upinzani katika Bajeti yake kuwa ni kuhakikisha Taifa linajiandaa kuwa na uchumi ambao utategemea rasilimali nyingine ikiwemo gesi.
“Tafiti zinaonyesha kwamba tuna gesi nyingi nchini sasa tunatakiwa kujiandaa namna ya kuiendesha rasilimali hiyo, ikiwamo kutunga sheria ya gesi,” alisema na kuongeza:

“Ni muhimu kuzalisha gesi zaidi ili wananchi waweze kupata gharama nafuu kuliko ilivyo sasa ambapo bei ya umeme ipo juu, jambo linalofanya wananchi wengi washindwe kutumia.”
“Kipaumbele kingine ni kuweka mfumo mpya wa elimu kwa kushirikisha sekta binafsi katika kutoa elimu kwa ubora zaidi, ikiwemo kuundwa kwa chombo cha udhibiti wa elimu (regulatory authority),” alisema Zitto.

Aliongeza kuwa jambo jingine ni kutoa kipaumbele na unafuu wa kodi kwa viwanda vya ndani vinavyotumia malighafi za hapa nchi, hasa za kilimo na zenye kuongeza ajira kama korosho, pamba na mkonge.

Hata hivyo, Zitto alisema kuwa pamoja na Serikali kupendekeza bajeti ya Sh15trilioni kwa mwaka 2012/2013, bado ni tatizo kwani bajeti ya mwaka  2011/2012  ambayo ilikuwa Sh13trilioni ilikuwa na changamoto kubwa katika utekelezaji wake.

Alisema katika bajeti ya mwaka jana, kambi hiyo ilitoa vipaumbele mbalimbali lakini kwa kiasi kikubwa ilifanikiwa katika kodi ya mafuta ya petroli na dizeli na tozo za ujuzi katika bodi ya mikopo na kwamba Serikali ilikataa kutekeleza pendekezo la kufuta posho za vikao.
“Tutaibana Serikali kwa nini imeshindwa kufuta posho za vikao hadi sasa, ingawa sisi tulipendekeza zifutwe,” alisema Zitto.

Changamoto
Akizungumzia deni la taifa, alisema badala ya kushuka limekuwa likiongezeka siku hadi siku na kufikia Sh22 trilioni kutoka Sh11 trilioni katika mwaka wa fedha uliopita, hivyo kuwapo umuhimu wa kufanya uchunguzi maalumu kwenye vitabu vya mikopo hiyo.

“Tatizo siyo Serikali kukopa, bali inakopa kwa ajili ya kufanyia kitu gani? Tunapendekeza kwamba kabla ya kukopa iwe inatolewa idhini na Kamati ya Hesabu na Uchumi badala ya sasa kuamriwa na waziri wa fedha,” alisema Zitto.

Alisema changamoto nyingine ni kuendelea kuwepo kwa matumizi yasiyo ya lazima hasa katika magari na posho mbalimbali na kuongeza kuwa, watasimamia ili kupata ufumbuzi wa suala hilo.
   
    

No comments:

Post a Comment