Thursday, 28 June 2012

MH.PINDA ASITISHA KUTANGAZA TAMKO LA SERIKALI KUHUSU MADAKTARI

 

Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni na Waziri Mkuu, Pinda, alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mkuu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe, aliyetaka kujua Serikali ina mipango gani ya dharula ya kuumaliza mgomo huo.

Alisema kwa hivi sasa, Serikali imechukua dharula, kwa kuwaita madaktari wasitaafu kwenda kwenye baadhi ya Hospitali za Serikali, kushika nafasi maeneo ambayo madaktari waliogoma.

Vilevile Serikali imewataka wananchi waende kuhudumiwa kwenye hospitali za Jeshi, ikiwemo Lugalo.

Pinda ameseama kuwa hata yeye alipopokea taarifa kuwa Dk. Ulimboka ametekwa na kupigwa alisikitika sana, na anamuombea apone haraka ili waendelee na suluhisho la mgomo huo wa madakatari.

Alisema kuwa amemuagiza, Waziri wa Mambo ya ndani kuunda jopo la wataalamu kuchunguza kwa haraka kuhusu tukio hilo.

“Mahakama iliwaonya madaktari wasigome na waende kuvieleza vyombo vya habari kuwa vimesitisha mgomo,” alisema na kuongeza:

“Serikali ikaendelea kuwa sikivu, lakini mgomo uliendelea. Jana tena mahakama kuu ili waomba madaktari wasigome. Tungeweza kuchukua hatua stahiki lakini tulisubiri hatua za Mahakama,” alisema Pinda.

Mjadala huo ulianza baada ya kipindi cha maswali na majibu kwa Mbunge wa Mbozi Magharibi, Godfrey Zambi kuomba mwongozo na kupitia kanuni ya 68 (7)ambapo aliuliza hatua za Serikali kuhusu mgomo huo.
“Ni kweli kwamba Serikali ilishatoa taarifa hapa Bungeni na pia nilishaeleza kwamba, baada ya majadiliano ilibidi turudi kwenye chombo cha kisheria kwenda kutoa taarifa kwamba kuna maeneo hatujaridhiana,” alisema Pinda na kuongeza:

“Kauli ya Serikali ni kwamba, madaktari waheshimu amri ya mahakama…tutatoa kauli rasmi ya Serikali kesho (leo). Tumeamua kulitaarifu Bunge lako Tukufu maana kwa kweli Serikali imechukua jitihada za kutosha sasa hata waswahili wanasema "liwalo na liwe.”

Pinda alisema kuwa, Juni 22, mwaka huu , Mahakama iliwaagiza madaktari hao kusitisha mgomo na Juni 26, mahakama hiyo ilirudia kutoa amri na kwamba Serikali ilichelea kuchukua hatua dhidi ya madaktari hao kwa sababu tayari suala hilo liko mahakamani.

Katika mwongozo wake, Zambi alikumbushia taarifa ya Waziri wa Afya, Dk Hussein Mwinyi aliyoitoa Juni 22, Bungeni kuhusu madai ya madaktari ya kuboreshawa huduma zao katika hospitali karibu zote nchini.
“Nashukuru taarifa ya Serikali ilitolewa vizuri lakini kuanzia jumamosi hiyo, madaktari bila kujali taarifa ya Serikali wakaendelea na mgomo katika hospitali zote za rufaa na leo asubuhi madaktari wa hospitali ya Taifa ya Muhimbili wamenithibitishia kuwa mgomo upo, ni madaktari mabingwa tu wachache wanaoendelea na kazi,” alisema Zambi na kuongeza:

“Nimeongea na madaktari wa Mbeya wamenithibitishia kuwa mgomo upo na taarifa hii naweza kukusomea na wabunge wenzangu, imetoka kwa daktari mmoja, kwamba mgomo upo na wanaendelea tangu Juni 23…,”
Zambi aliitaka Serikali kueleza hatua itakazochukua kwa madaktari hao kwa kuendelea kugoma bila kujali maisha ya Watanzania wanaoteseka hospitalini.

“Katika hatua hii naomba kupata mwongozo wako, Watanzania wanateseka na madaktari wanaendelea kugoma, Serikali sasa inachukua hatua gani kama suala hili liko mahakamani…. na mimi nisingeomba wabunge wasimame ili waniunge mkono tulijadili maana liko mahakamani,” alisema Zambi.

Hata hivyo baada ya Waziri Mkuu kutoa maelezo yake, Mbunge wa Ubungo John Mnyika naye alisimama na kushauri kwamba Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii nayo itoe taarifa ili kuwe na taarifa za pande mbili kabla ya kujadiliwa bungeni.

“Taarifa kutoka vyombo vya habari ni kwamba kesi iliyopo mahakamani ni ya MAT siyo Jumuiya ya madaktari… nimeiandikia barua ofisi yako… tuipokee taarifa ya kamati ya Bunge ya mambo ya jamii ili tutakapojadili tuwe na taarifa ya upande wa pili,” alisema Mnyika.

Hata hivyo Naibu Spika, Job Ndugai alisema tayari kamati hiyo ya Bunge ilishalifanyia kazi suala hilo na kwamba hakuna maana ya kurudi tena katika jambo lilelile.
mwisho

No comments:

Post a Comment