Thursday, 14 June 2012

Dk Mwakyembe awasha moto TRL


 Send to a friend
Wednesday, 13 June 2012 20:50
0digg
Mussa Juma, Dodoma
BAADA ya kusafiri kwa treni kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amebaini hujuma nzito katika Shirika la Reli Tanzania (TRL) ikiwamo ofisa mmoja kuwaibia abiria kwa kughushi viwango vya nauli na ameagiza afukuzwe kazi.

Licha ya kuagiza kutimuliwa kwa ofisa huyo, pia alitangaza kuandaliwa utaratibu wa kufanya mabadiliko kadhaa katika kuboresha usafiri huo, ikiwamo kuondoa malipo ya nusu nauli kwa watoto wadogo kuanzia miaka mitatu hadi miaka 10 na pia kuondolewa kwa utaratibu wa malipo ya mizigo midogo ya abiria.

Juzi, Dk Mwakyembe ambaye tayari amewang’oa vigogo wanne wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), aliamua kusafiri kwa treni hadi Dodoma akitokea Dar es Salaam ili kujionea utendaji kazi wa shirika hilo.

Mara baada ya kuwasili katika Stesheni ya Dodoma saa 1:30 asubuhi, Waziri Mwakyembe alizungumza na waandishi wa habari na kusema akiwa katika safari hiyo, amepata fursa za kutembelea mabehewa yote na kuzungumza na abiria.

Dk Mwayembe alisema ingawa safari ilikuwa nzuri, kuna mengi ambayo ameyabaini ambayo ni pamoja na abiria kulipa nauli kubwa na kuandikiwa tiketi tofauti jambo ambalo alisema ni wizi na kamwe wizara yake haiwezi kulifumbia macho.

“Unakuta nauli halali ni Sh9,000 lakini, abiria ameandikiwa Sh29,000. Sasa nimeagiza huyu anayehusika afuatiliwe na kujulikana na nipewe taarifa ameondolewa,” aliagiza Dk Mwakyembe.
Alisema pia katika safari hiyo, alibaini uchakavu mkubwa wa mabehewa na hakuna tofauti ya daraja la tatu na la kwanza, upungufu mwingine ni katika utendaji na taratibu jambo ambalo linapaswa kuchukuliwa hatua.

Dk Mwakyembe alisema si vyema mtoto kuanzia miaka mitatu kulipishwa nusu nauli, kwani taratibu zinapaswa kufanywa ili hadi mtoto wa miaka 10 ikiwezekana asilipishwe nauli kwani treni ndiyo usafiri wa umma.

Kuhusu mizigo, alisema kwa sasa mizigo ya abiria inalipiwa kwa kilo kama ilivyo usafiri wa ndege jambo ambalo si sawa kwani mzigo wa abiria kuanzia kilo 20 unalipishwa jambo ambalo linapaswa kuangaliwa.

“Usafiri huu mimi nasema ndiyo wa umma hivyo, tusizuie watu kupeleka hata zawadi nyumbani kwao ni vyema tuwe na utaratibu walau mizigo kidogo ya abiria isilipiwe,” alisema Dk Mwakyembe.

Safari tatu kwa wiki
Akizungumzia tatizo la ratiba za usafiri, Dk Mwakyembe alisema mipango inafanywa ili kufikia Desemba, mwaka huu walau kuwe na safari tatu za kutoka Dar es Salaam hadi  Kigoma na Tabora na kuondoa kero zilizopo sasa.

Waziri huyo alisema anaamini safari hizo zikirejea, zitapunguza wingi wa abiria na msongamano wa watu kwenye treni na pia zitasaidia kuanza kwa usafirishaji wa mizigo kwa kutumia usafiri huo.
“Tutawaomba wabunge wapitishe bajeti yetu na wapande treni ili kuona usafiri huu, nina amani tukiondoa upungufu kidogo, huu utakuwa usafiri mzuri sana,” alisema.

Hujuma
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tzeba ambaye allimpokea Dk Mwakyembe alisema licha ya kuwepo hujuma katika nauli za abiria, pia wamebaini hujuma kubwa katika mizigo inayosafirishwa kwa reli katika mashirika yote ya TRC na Shirika la Tanzania na Zambia (Tazara).

Alisema maofisa wasio waadilifu wa mashirika hayo, wamekuwa wakisafirisha mizigo mingi lakini inayoandikiwa na kulipwa serikalini ni ile yenye uzito mdogo.

“Utakuta mzigo wa tani 40 hadi 60 unaandikiwa tani 10 au 20 fedha nyingine zinaingia mifukoni mwa wajanja, hatutakubali jambo hili,” alisema Dk Tzeba
Alisema yeye na waziri wake, pamoja na maofisa wengine, watakuwa wakisafiri kwa kushtukiza kwa reli mara kwa mara ili kubaini hujuma zote na kuwachukulia hatua wahusika mara moja.
“Mimi nilikuja hapa Dodoma kwa kiberenge na baadhi ya wabunge wa kamati ya miundombinu na leo amekuja waziri kwa treni hii haitakuwa mara yetu ya kwanza, tutasafiri sana kwa reli ili kubaini hujuma zilizopo,” alisema Dk Tzeba
 .

No comments:

Post a Comment