Monday 18 June 2012

Chadema yavuna vigogo wa CCM

NI KATIKA MIKOA YA IRINGA, SINGIDA,NAPE AWABEZA, AWAFANANISHA NA OILI CHAFU  Send to a friend
Monday, 18 June 2012 09:07
0digg
Pg 1 Mjumbe wa Kamati kuu ya CHADEMA Aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema (Katikati) akisindikizwa na wanachama wa chama hicho alipokuwa akiingia katika uwanja wa Shule ya Msingi Tabata jijini Dar es Salaam jana kwa ajili ya mkutano wa hadhara. Picha na Venance Nestory

Tumaini Msowoya, Iringa
WIMBI la viongozi na makada wa CCM kuhamia vyama vya upinzani linaendelea kukitikisa chama hicho, baada ya viongozi wa chama hicho mikoa ya Iringa na Singida kujiunga Chadema.Chadema kimewateka makada hao kilipofanya mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Kihesa Sokoni, juzi mjini Iringa kwa lengo la kuendeleza mkakati wake wa Movement For Change-M4C (Vuguvugu la Mabadiliko) na kufafanua bajeti ya Serikali ya mwaka 2012/13.Wimbi la makada wa CCM kuhamia Chadema lilipamba moto Aprili mwaka huu baada ya Ole Millya kuondoka akifutiwa na viongozi kadhaa wa chama hicho, akiwamo Katibu wa Uhamasishaji wa UVCCM Wilaya ya Longido, wenyeviti watano wa vitongoji na wanachama 2,402 wa CCM wilayani Ngorongoro.
Viongozi wa CCM waliojiunga Chadema jana, ni Katibu Mwenezi wa chama hicho Wilaya ya Iringa Vijijini, Yohana Mwena na Mjumbe wa Baraza la Utekelezaji la Umoja wa Vijana (UVCCM) wilayani humo.

Wengine ni Katibu wa UV-CCM Mkoa wa Singida anayesoma katika Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco) kilichopo Iringa, Kasifia Sumpta, mwanazuoni wa chuo hicho, Dk Matabazi Lugazia, na kada wa siku nyingi wa chama hicho, Zuberi Mwachura ambaye alirejesha kadi sita za CCM kutoka katika familia yake.
Licha ya Chadema kupewa kibali cha kufanyia mkutano huo kwenye uwanja mdogo uliozungukwa na barabara zenye magari mengi, umati wa watu ulifurika, huku wengine wakilazimika kukaa juu ya nyumba na miti.
Katika mkutano huo ambao ulihutubiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, Mwenyekiti wa zamani wa UVCCM,  Mkoa wa Arusha, James ole Millya na Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, wanachama wengine zaidi ya 200 wa CCM walirudisha kadi na kujiunga na Chadema.
Mbali na shughuli ya kupokea wanachama hao kwa mtindo wa ‘kuvua gamba na kuvaa gwanda’, viongozi wa Chadema waliichambua bajeti ya Serikali inayoanza kujadiliwa bungeni leo, wakifafanua ni kwa jinsi gani haitamnufaisha mwananchi wa kawaida.

Waliovua gamba
Wakizungumza wakati wakirudisha kadi hizo, makada na viongozi hao walisema kuwa, wameamua kufanya hivyo baada ya kuchoshwa na sera za CCM, ambazo walidai kuwa hazitekelezeki.
Akizungumzia kuhama kwake CCM, Mwena alisema amechoka kuona rasilimali za taifa haziwanufaishi wananchi, badala yake zinawanufaisha matajiri, huku kukiwa na tofauti kubwa ya kipato.

“Mwenzenu nimevumilia nimeshindwa, leo nimeamua kuondoka CCM, nimechoka kuona sera ambazo hazitekelezeki, huku wananchi maskini wakiendelea kuwa maskini wa kutupwa wakati kuna rasilimali nyingi za taifa zinazoliwa na matajiri,” alisema Mwena.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya wakazi Mji wa Iringa na vitongoji vyake, baadhi ya waliopewa nafasi kueleza kero zao walisema, hawaikubali bajeti iliyosomwa hivi karibuni kwa kuwa haijalenga kuwasaidia wananchi maskini.

 “Bajeti iliyosomwa inataja kupandisha kodi ya pombe na sigara, ikimaanisha kuwa uchumi wetu unategemea vilevi hivyo, hivi Watanzania tukigoma kunywa pombe ina maana Serikali itashindwa kujiendesha, bajeti iliyosomwa tunaikataa na tunawaagiza mkawaeleze, kuwa hiyo imelenga kuwaneemesha wao na siyo sisi maskini,” alisema Yohana Mkule, mkazi wa manispaa hiyo.
Kutokana na wananchi wengi, kuigomea bajeti hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe aliwaunga mkono, huku akiahidi kuwa Kambi ya Upinzani haitakubali bajeti hiyo ipitishwe.

“Uwendawazimu ni kufanya jambo lilelile, kwa njia zilezile huku ukitegemea matokeo tofauti. Serikali inatumia njia zilezile ikidhani mfumko wa bei unaweza kupungua, huu ni uwendawazimu, nawatoa hofu kwa sababu hatutakubali bajeti hii ipitishwe,” alisema Kabwe.
Alisema vitu vinavyofanya maisha ya Watanzania kuwa magumu ni mfumko wa bei, hasa katika vyakula ambao ni asilimia 25, na nishati ambayo ni asilimia 27, huku Serikali ikishindwa kudhibiti hali hiyo kwa kuandaa bajeti inayolenga kukomoa wananchi.

Hata hivyo, aliwataka wakazi wa Iringa kuendelea kuwa wavumilivu wakati mbunge wao atakapokuwa akifanya kazi za kuleta mabadiliko katika maeneo mengine, ili kukiandaa chama hicho kushika dola mwaka 2015.

Mwenyekiti wa zamani wa UVCCM Mkoa wa Arusha, James Millya aliwataka wakazi wa Manispaa ya Iringa kutoendelea kuivumilia CCM ambayo imeshindwa kutambua kitu gani  wananchi wake wanataka.

“Mimi niliondoka baada ya kuona hoja zangu hazifanyiwi kazi ndani ya CCM, nimeingia Chadema nikitarajia mabadiliko makubwa kwa nchi yangu, msikubali kuumia, lazima tulete mabadiliko,” alisema.

Millya alisema nchi nyingi ikiwamo Kenya zimeving’oa vyama tawala, isipokuwa Tanzania ambayo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 lengo hilo litatimia.

Mbunge wa Iringa Mjini, Msigwa alisema viongozi wa Chadema wameamua kugawana siku za mwisho wa wiki kufanya kazi za chama hicho kutokana na mkutano wa Bunge unaoendelea katika siku za kawaida.

mwananchi

No comments:

Post a Comment