Wednesday 18 May 2011

Membe apinga fedha za rada kutolewa kwa NGOs

Membe apinga fedha za rada kutolewa kwa NGOs

SERIKALI ya Tanzania imepinga uamuzi wa Kampuni ya Vifaa vya Kijeshi nchini Uingereza ya BAE Systems kuunda jopo litakalosimamia malipo ya fidia ambayo iliamuliwa na
mahakama kuilipa Tanzania kwa kuwa uamuzi huo unakwenda kinyume na msimamo wa serikali ambayo inataka fedha hizo ziingizwe serikalini.

Mbali na hilo, imesema kuwa lugha iliyotumiwa na BAE kwamba fedha hizo zikiingizwa serikali zinaweza kutumika vibaya ni matusi kwa Serikali ya Tanzania na hivyo kuitaka Serikali ya Uingereza kushinikiza fedha hizo kurejeshwa kwa serikali ya Tanzania badala ya kuingizwa kwenye mashirika ya hiyari.

Uamuzi ulioitaka BAE kuilipa Serikali ya Tanzania kiasi cha paundi milioni 29.5 ulitolewa na Jaji Bean wa Mahakama ya Southwark ya Uingereza Disemba 21, mwaka jana baada ya jaji huyo kutoridhika na maelezo pamoja na makubaliano ya SFO na BAE ambapo mahakama iliamuru fedha hizo zilipwe kwa wananchi wa Tanzania.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe aliwaeleza waandishi wa habari jana, “Uamuzi huu wa BAE una lengo la makusudi kuonesha sura ya kutokuamini dhamira ya Serikali ya Tanzania kutumia fedha hizo kwa kusudi lililokuwa limetolewa.. Unalenga kuonesha umma wa Uingereza kuwa Serikali ya Tanzania inatawaliwa na rushwa na haiaminiki kuwatendea haki wananchi wake,” alisema Bw. Membe.

Alisema kuwa uamuzi huo unakwenda mbali zaidi kwa kupuuza ahadi iliyokuwa
imetolewa na Serikali ya Tanzania na Uingereza kuwa fedha hizo zitasimamiwa vyema, hivyo akasema Tanzania haiko tayari kukubaliana na uamuzi huo na badala yake inataka fedha hizo zirejeshwe serikalini ambako ndo ziliibwa.

Alisema kuwa kampuni hiyo inataka kujaribu kujikosha mbele ya asasi mbalimbali zisozo za kiserikali za Uingereza baada ya kukosolewa sana kwa kashfa ya rushwa, hivyo kutaka kujionesha kuwajali zaidi Watanzania.

“Serikali yetu ina uhusiano mzuri sana na Serikali ya Uingereza na serikali hiyo imekuwa mfadhili wetu mkubwa wa miradi ya maendeleo kwa miaka yote, tunaiomba Uingereza ituunge mkono katika kushinikiza BAE kurejesha fedha zetu Tanzania,” alisema Waziri Membe.

Akielezea matumizi ya fedha hizo ambayo yaliwasilishwa na Tanzania pamoja na Uingereza kuonesha namna zitakavyotumika, Bw. Membe alisema zingenunua vitabu vya kiada vya sh. milioni 4.4 kwa ajili ya shule za msingi, vitabu vya miongozo ya mitaa vya masomo 12 kwa shule 16,000, madawati 200,000, kujenga nyumba 1,196 za walimu katika wilaya zote nchini vifaa vya kufundishia na kujenga vyoo 2,900.

Awali BAE ilishtakiwa kwa kuongeza gharama za mauzo ya rada kwa Serikali ya Tanzania ambapo waendesha mashtaka wa SFO na BAE walikubaliana kuimaliza kesi hiyo nje ya mahakama kwa BAE kukiri kosa la kutoweka sawa kumbukumbu za fedha na mahesabu katika mchakato wa mauzo ya rada kwa Tanzani.

Kutokana na hali hiyo, BAE ilikubali kulipa sehemu ya faini hiyo kwa Tanzania kama sehemu muhimu ya makubaliano hayo.

Baada ya miezi sita BAE imekuja na uamuzi wa kuunda jopo litakalosimamia fedha hizo ikiwa na maana ya kutotoa fedha hizo kwa Serikali ya Tanzania  bali kwa asasi zisizokuwa ya kiserikali.
MAJIRA
SEREKALI YA TANZANIA INA VIONGOZI MABOGA KWELI,SASA HIVI NDIO WANAGUNDUA UMUHIMU WA HIYO PESA?MBONA HAWAJAWACHUKULIA HATUA YOYOTE WALIOHUSIKA NA UFISADI HUO WALA HATA KUHUDHURIA KESI HAWAJAONYESHA INTEREST,LEO HII WAMESIKIA HELA HIYO INAKUJA(WAKANDAA UMA NA KISU NA KUKAA MKAO WA KULA KUISUBIRI ILI WAICHAKACHUE TENA) WALIPOAMBIWA HAIJI CASH ILA INAELEKEZWA MOJA KWA MOJA KWA HUDUMA ZA WANANCHI WAMENG"AKA HAO MPAKA MAPOVU YANAWATOKA MDOMONI,HUKU WANAPIGA MIKWARA KIBAO.NAONA HAWA JAMAA WAMEJISAHAU SANA UNAMTISHIA NYAU MTU MZIMA?WAENDELEENI KUPIGA KELELE NAONA HATA HAWASOMI ALAMA ZA NYAKATI.BEN ALLI,MUBARAQ,GBAGBO,GHADAFFI YUKO MBIONI WOTE HAO WALIKUWA WABISHI NA WAKAIDI HIVYO HIVYO,BONGO NA NYIE SUBIRINI ZAMU YENU ITAFIKA TU.

No comments:

Post a Comment