Wednesday 25 May 2011

MGAO WA UMEME KUISHA MIAKA MITATU IJAYO


 Send to a friend
Tuesday, 24 May 2011 22:02
 
SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco), limesema mgao wa umeme utaisha baada ya miaka mitatu ijayo.Tanesco wamesema hatua hiyo inatokana na serikali kuacha kuwekeza katika shirika hilo kuanzia mwaka 1997 kwa sababu liliwekwa kwa iliyokuwa chini ya Tume ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) ili kusubiri kuchukuliwa na mwekezaji.

Hayo yalisemwa jana na Meneja Uhusiano wa Tanesco, Badra Masoud alipokuwa akihojiwa na Redio Clouds.Alisema miundombinu mingi ya shirika hilo imechakaa kwa sababu ni ya siku nyingi.“Mgao haukwepeki, ingawa hatupendi uwepo kwasababu hata sisi unatukosesha mapato.

 “Kutokana na jitihada mbalimbali tunazozifanya tuna imani katika miaka mitatu ijayo mgawo wa umeme utaisha,”alisema.Alisema mgao unaoendelea sasa umesababishwa na kukosekana kwa gesi ya kutosha katika mitambo ya kuzalishia umeme.

Masoud alisema kampuni ya Pan Afrikan inaiuzia Tanesco gesi ambayo inawekwa  kwenye mitambo ya kuzalishia umeme.Alisema ukarabati unaoendelea sasa katika  kisima cha gesi cha kampuni hiyo umesababisha kukosekana kwa gesi ya kutosha kwa ajili ya kuwekwa kwenye mitambo hiyo.

“Wao walisema ukarabati huo utafanyika kwa siku nane kwa hiyo tunategemea  kufikia Mei 26, mwaka huu, mgao utapungua,”alisema.

Alisema pia wanatarajia kununua mtambo wa kuzalisha megawati 50 badala ya kukodisha.Alisema tayari kampuni nyingine imeanza mchakato wa kuzalisha megawati 70 katika eneo la Majani Mapana Tanga kwa ajili ya kuiuzia Tanesco.

Alisema kampuni hiyo ni kati ya kampuni 17 zilizoomba zabuni hiyo na kushinda na kwamba katika kituo cha Ubungo na Mwanza, kuna mipango mingine inaendelea kwa ajili ya kuzalisha umeme zaidi.

Katika hatua nyingine, Meneja huyo alisema wameshindwa kutumia mitambo ya kuzalishia megawati 120 iliyoko Ubungo kwasababu teknolojia yake imepitwa na wakati.Alisema mitambo hiyo ni ya muda mrefu na hata vipuri vyake havipatikani.

mwananchi

No comments:

Post a Comment