CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeingia kwenye mgogoro baada ya baadhi ya wabunge kupandwa na hasira dhidi ya wenzao wanaoendesha kampeni ya kutaka posho za vikao kwa wabunge ziondolewe.Mkwaruzano huo iliibuka ndani ya kikao cha wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe.
Kikao hicho kiliitishwa na kambi hiyyo kwa lengo la kuweka msimamo wa kupinga posho za vikao kwa wabunge, lakini kikageuka uwanja wa vita uliozusha vurumai kubwa kiasi cha kushindwa kufikia muafaka.
Baada ya kikao hicho kufunguliwa, John Mnyika (Ubungo-Chadema) aliwasilisha hoja hiyo ya kutaka wabunge wa upinzani kuweka msimamo wa pamoja wa kupinga posho hizo ili mkakati huo ulioanzia kwenye Bunge hilo la Bajeti, uweze kufanikiwa.
Akifikiri ataungwa mkono, Mnyika aliwataka wabunge kuonyesha moyo huo wa kishujaa kwa kutosaini kitabu cha mahudhurio bungeni, lakini wawepo ndani ya vikao.
Kauli hiyo ya Mnyika ilikuwa sawa na kumwaga petroli kwenye moto unaowaka ambapo wabunge watatu wa Chadema (majina tunayahifadhi kwa sasa) walikuja juu na kupinga vikali hoja hiyo.
Upinzani huo mkali uliotolewa na wabunge hao ulidhihirisha kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyesema kuwa ingawa baadhi ya wabunge wa chama hicho wanajionyesha kimbelembele kusisitiza mpango huo, wengine wa chama hicho pia wanaumia kimoyomoyo, lakini hawasemi.
Suala la kukataa posho bungeni lilianzishwa na Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini-Chadema) akisema zinaenda kinyume na mpango wa Taifa wa kupambana na umasikini kwa kuondoa posho zisizo na tija.
Zitto akionekana kuwa na ushupavu mkubwa ilifikia mahali akaamua kutosaini mahudhurio Bungeni ili jina lake lisiorodheshwe miongoni mwa watakaolipwa licha ya Spika, Anne Makinda kutishia kuwa kitendo hicho kinaweza kumfukuzisha bungeni.
Mkakati wa Mnyika ulikuwa ni wabunge wote wa upinzani kuwa na mshikamano katika hilo jambo ambalo sasa limeonekena kuwa ni nyongo kiasi cha wengine kutaka kuwararua wenzao wakisema ni msimamo usio na maana.
Posho za mafutaWakati hayo yakiendelea, suala hilo liolichukua sura mpya ndani ya Bunge kutokana na kuwepo hoja ya kutaka malipo ya nauli kwa wabunge nayo yaondolewe ili kuipunguzia mzigo Serikali.
Suala hilo jipya liliibuliwa bungeni jana na Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Esta Matiko akisisitiza Bunge lisitishe malipo hayo kwa ajili ya mafuta kwa magari ya wabunge.
Akiwa mchangiaji wa saba katika mjadala wa hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2011/2012 uliokuwa ukiendelea bungeni jana, Matiko alisema wabunge wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuisaidia Serikali katika kupunguza matumizi yake.
''Tuondoe transport allowance za wabunge za ndani na Serikali idhibiti matumizi ya magari yake ili fedha hizo zipelekwe kwenye sekta nyingine nyeti, kama kweli tunataka kufanikiwa katika mpango huo wa maendeleo ya miaka mitano," alisema Matiko ambaye kwa msisitizo, aliwataka wabunge wote wamuunge mkono.
Ingawa Matiko hakueleza kiasi cha fedha anacholipwa mbunge kama nauli ya kutoka jimboni kwake mpaka bungeni, vyanzo vya habari vililieleza gazeti hili jana kuwa nauli ya safari inalipwa kutokana na kilometa anazosafiri mbunge kutoka jimboni kwake hadi kwenye vikao vya Bunge.
"Mbunge analipwa Sh2,500 ili anunue lita moja ya mafuta ambayo ataitumia kusafiria kwa kilometa tano. Analipwa hivyo kwenda kwenye vikao na kurudi jimboni kwake," alisema Matiko baadaye katika ujumbe wake uliopenyezwa kwa waandishi wa habari baada ya kumaliza kuchangia mjadala huo.
Kuhusu Serikali kupunguza matumizi yake, mbunge huyo ameishauri kudhibiti matumizi ya magari ya Serikali katika nyakati ambazo sio za kazi na kuanza kutumia utaratibu wa marejesho ya matumizi (retirement) kwa fedha inayotumika kununua mafuta kwa ajili ya magari hayo.
"Serikali pia iwe na udhibiti mzuri wa matumizi ya magari yake, ianzishe utaratibu wa retirement za fedha za mafuta na ipunguze ukarabati wa nyumba zake kila mwaka. Hivi kweli tunahitaji kutumia fedha zote hizi kukarabati nyumba hizo kila mwaka?" alihoji na kuendelea " hata majumba yetu yenyewe hatuyakarabati kila mwaka."
"Ushauri wangu kwa wabunge ni kukumbuka kuwa tumetumwa na wananchi na ikitokea mbunge ana wazo nzuri..." aliendelea kabla ya kugongewa kengele ya kumaliza muda wake wa kuchangia hoja.
Hoja hiyo mpya ya kutaka wabunge wakatwe fedha za nauli, inaonekana kuwa ni mwiba mwingine kwa baadhi ya wabunge ambao tayari wameonyesha msimamo wao kukataa kuondolewa kwa posho za vikao.
Mbali na wabunge hao kupinga, Serikali kupitia Waziri Mkuu Mizengo Pinda imeshatoa msimamo wake kuwa jambo hilo haliwezekani ila linajadilika, kwa kuwa lipo kwa mujibu wa Sheria na Katiba.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Pinda ilipingwa vikali na Chadema juzi ambao wamemtaka aifute kwa kile walichoeleza kuwa sio ya kweli kwani katiba na sheria zingine hazitaji kiwango cha posho.
Pinda alitoa kauli hiyo wakati wa kujibu maswali ya hapo kwa papo Alhamisi iliyopita baada ya mbunge wa Mkanyageni Habib Mnyaa kumtaka atoa msimamo wa Serikali kuhusu wabunge wanaopinga posho kwa kuwa huku ni kuvunja katiba.
Jana Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira alipotakiwa kuzungumzia hoja hizo za Chadema kutaka posho na nauli hizo zifutwe, alijibu," Sina cha kusema."
"Mimi niulizwe mambo makubwa ya kitaifa, posho sio jambo kubwa kiasi hicho, hizo (posho) zinapangwa na kufutwa na kama Chadema wanaona wanapewa nyingi sana, wao waache,"
Bajeti yazidi kuwagawa wabungeMjadala wa hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2011/2012 umeendelea kuwagawa wabunge ambao jana walioonekana kumeguka makundi mawili ya wabunge wa CCM na Chadema katika kuitetea na kuibeza.
Mbunge aliyeanza kuchokoza moto huo ni Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM) ambaye katika mjadala wake ametumia muda mwingi kuiponda bajeti mbadala ya wapinzani akisema imejaa giza na yenye lengo la kutekenya fikra za watu.
"Serikalini kuna watalaamu na kwenye vyama vya siasa kuna wanasiasa. Hii ni bajeti iliyojaa matumaini kwa Watanzania, imepunguza utegemezi kutoka asilimia 57 hadi asilimia 17 na imetuonesha kuwa matarajio ni kupunguza utegemezi huo hadi asimilia 10," alisema mbunge huyo na kuongeza:
"Bajeti ya wapinzani imejaa giza na imeletwa kutekenya fikra tu ina elementary contradiction, huwezi kuongeza mshahara bila kueleza vyanzo vya mapato."
Kauli hiyo ilipingwa na mbunge wa Ilemela (Chadema) Highnes Kiwia ambaye aliiponda bajeti hiyo na kuipongeza bajeti iliyotolewa na wapinzani akisema ndiyo iliyopaswa kutekelezeka.
"Bajeti mbadala ilipaswa kusomwa na positivu mind kwani ikisomwa na negative mind sio tu msomaji ataona giza, bali atatumbukia gizani," alisema Kiwia na kuongeza:
"Sisi tunachofanya sio kubeza mafanikio, ila tunasema mafaniko yaliyopo hayaendani na wingi wa rasilimali tulizonazo, hatusemi hakuna kilichofanyika. Nyerere alisema, ili kuwa na maendeleo tunahitaji viti vitatu; watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora hakutaja fedha.
"Alisema (Nyerere) hatuwaondoi wakoloni kwa sababu tunachukia rangi zao, ni matendo yao. Sasa mkoloni wa leo ni ufisadi. hakuna namna Tanzania tukaondokana na umaskini kama hatuwezi kuondoa ufisadi."
Mbunge huyo ambaye ametishia kuikwamisha bajeti hiyo aligeukia sekta ya umeme akimtaka waziri Ngeleja kuongeza kasi ya utendaji wake ili huduma hiyo iwafikie watu wengi zaidi kuliko ilivyo sasa. "Namwambia ndugu yangu, Ngeleja, watu hawataki mahesabu ya Megawati, wanataka umeme," alisema
Ritha Mlaki Viti Maalum (CCM) alisema bajeti ni nzuri kwa kuwa inaangalia maeneo mengi muhimu isipokuwa kinachotakiwa sasa ni utekelezaji.
"Mimi nashauri tu kwani bajeti ni nzuri ila nitaongelea maeneo machache. hatufikirii kuondoa msoangamano katika jiji la Dar es salaam. Maeneo mengine jiji kama Dar eS Salaam linakuwa na bajeti lake," alisema.
Leticia Nyerere Viti Maalumu (Chadema) alisema bajeti ya serikali ya mwaka ujao ni mbovu kwa kuwa miradi mingi inategemea fedha kutoka kwa wafadhili. "Kama wahisani hao wakibadilisha mawazo, hakuna kitakachofanyika" alisema.
Mbunge huyo alipendekeza kuondolewa mpango wa kuviondolea kodi vifaa avya ulinzi na usalama akieleza kuwa hakuna maana na badala yake viendelea kutozwa kodi ili fedha itumike katika maeneo mengine.
"Mwisho mheshimiwa mwenyekiti naomba nimalizie kwa kuuliza maswali yafuatayo; bajeti hii inazingatia wajawazito, watoto wa mitaani, machinga wasiokuwa na mitaji, mishahara ya walimu na madaktari, mahakimu na wazee wastaafu?
Lakini katika mchango wake Mbunge wa Njombe Kaskazini (CCM) Deo Sanga aliomba ushirikiano wa wabunge wote ktika kutekeleza bajeti hiyo badala ya kuiachia serikali peke yake
"Haya yote yafanikiwa kama tutajenga umoja na mshikamano, humo ndani kuna mashekhe na wachungaji, tunaomba mtuombee tuwe kitu kimoja katika hili" alisema.
chanzo:mwananchi