Saturday 4 June 2011

GADNA NA CREDO WAZUA TIMBWILI BONGO

Mastaa wawili wanandoa Bongo, ‘diva’ wa muziki wa Kizazi Kipya, Judith Wambura Mbibo ‘Lady Jaydee’ au ‘Jide’ na aliyekuwa mtangazaji wa Radio Clouds FM, Gardner G. Habash ‘Kaptaini’ (pichani) wametibuliwa ‘laivu’ kufuatia timbwili zito lililojiri kwenye mgahawa wao.

HABARI KAMILI
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, tukio hilo lilichukua nafasi ndani ya mgahawa unaomilikiwa na mastaa hao uitwao Nyumbani Lounge Kinondoni, Dar es Salaam usiku wa Jumapili (Mei 29, mwaka huu).

Chanzo hicho kilidai kwamba, Credo Mwaipopo ambaye ni rafiki wa karibu wa mastaa hao anayecheza mpira wa kulipwa Sweden, alitimba mgahawani hapo akifuatana na ‘brazameni’ aliyetajwa kwa jina moja la Pacha.

Kilidai kwamba, Jide alipomuona Mwaipopo alimlaki kwa shangwe kisha wakakaa meza moja wakibadilishana mawazo.

Chanzo hicho kilidadavua kwamba, wakati mambo yakiendelea huku watu ‘wakila bata za ajabu’ ndani ya mgahawa huo, ghafla Pacha alianza kufanya vurugu kinyume na utulivu uliokuwa eneo hilo.

Ilidaiwa kuwa, Pacha aliagiza vinywaji ambapo alipewa bili ya shilingi 10,000 ndipo akazidisha vurugu akisema kwamba, hakutumia kiasi hicho na badala yake akalipa shilingi 4,500.

Ilisemekana kwamba, kufuatia hali hiyo, Gardner alimtaka jamaa huyo kuwa mtulivu ili kutoharibu starehe za watu wastaarabu waliokuwa wakijiachia mahali hapo.
Ilidaiwa kwamba, Pacha hakumwelewa na badala yake alimtemea mate Gardner ambaye hakuwa na namna, ikabidi amtoe kwa msaada wa mabaunsa.

Chanzo kilizidi kudai kwamba, Mwaipopo alipoona hali hiyo aliagana na mastaa hao kisha akamfuata Pacha wakaondoka kuelekea katika Klabu ya New Maisha Masaki, Dar.

Ilidaiwa kwamba, baada ya mastaa hao kumaliza shughuli zao mgahawani hapo, nao walielekea Maisha ambapo walikutana tena na Pacha ambaye aliendelea kuwafanyia fujo za kufa mtu huku akichomoa sime.

Ikasemekana kwamba, Gardner alipoona hali hiyo alimchukua Jide akampeleka kwenye gari na kuondoka eneo hilo.

GARDNER AFUNGUKA
Baada ya kuzitia kibindoni habari hizo, Risasi Jumamosi lilimtafuta Gardner ili kusimulia mkasa mzima ambapo mbali na kukiri kutokea kwa timbwili hilo, alikuwa na haya ya kusema:

“Kwanza Mwaipopo ni rafiki mkubwa wa familia yangu na mambo mengi huwa tunashirikiana kwa hiyo si kweli kwamba alikuwa na lengo baya na mke wangu (Jide) kama ambavyo huyo Pacha alikuwa akijitapa kwamba nilimwondoa kwa sababu ya wivu.

“Nyumbani Lounge ni sehemu ya wastaarabu kwa hiyo nilihisi jamaa anataka kutuondolea amani iliyokuwa imetawala siku hiyo.

“Nililazimika kutumia nguvu kumtoa Pacha ili kuepuka athari kwa wateja wengine.
“Zoezi hilo lilifanikiwa na tukajua mambo yamekwisha, lakini nilishangaa baadaye tulipofika New Maisha Club ili kukutana na Mwaipopo ambaye tulipanga kuonana mahali hapo, jamaa alitutibua tena alipoanza kututukana na kusababisha vurugu nyingine.

“Kuepuka vurugu zake, tuliamua kukatisha mipango yetu, tukaondoka eneo hilo ambapo tulikutana na Mwaipopo siku iliyofuata.”

PACHA ATAKA ‘HELA’ ATOE STORI
Kwa upande wake Pacha alipotafutwa na gazeti hili alikuwa na haya ya kusema:
“Ni kweli vurugu zilitokea lakini kama mnataka ‘full’ stori, nipeni ‘hela’ ili niwape mkanda kamili.”

CHANZO:GLOBAL PUBLISHERS

1 comment: