Tuesday 28 June 2011

WAKENYA WAICHAKACHUA SAMUNGE KWA BABU

*Waanza kutoa takwimu potofu kuwadanganya watu
*Wageni sasa wapitia Kenya kuelekea Samunge
*Mbunge ataka Serikali iingilie kati, ikanushe uongo
Na Mregesi Paul, Dodoma


MBUNGE wa Ngorongoro (CCM), Kaika Telele, amesema Wakenya wameanza kujitangaza kimataifa, kwamba Kijiji cha Samunge kilichopo Loliondo Mkoa wa Arusha, hakiko Tanzania bali kiko Kusini mwa Kenya.
Telele alitoa madai hayo bungeni jana alipokuwa anachangia mjadala wa hotuba ya makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012.
“Napenda kumzungumzia Babu wa Loliondo kwa sababu amefanya mambo makubwa sana na naishukuru Serikali kwa kumpa ushirikiano wa karibu.
“Nawashukuru pia wote waliokwenda Loliondo kupata kikombe cha Babu, waliopona ndiyo wanaojua Babu amewasaidiaje kwa sababu hiyo ni siri yao.
“Pamoja na kwamba Kijiji cha Samunge kiko Tanzania hivi sasa Wakenya wanajitangaza kwamba kijiji hicho kiko kusini mwa Kenya… huu siyo ukweli kabisa kwa sababu wanafanya hivyo ili wageni wanaokuja kwa Babu wapitie Kenya.
“Wanawadanganya watu kwamba, kutoka KIA hadi Samunge ni kilomita 800, wanasema kutoka Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyata hadi Nairobi ni kilomita tatu, wanasema kutoka Nairobi hadi Samunge kupitia Loliondo ni kilomita 45 wakati usahihi ni kwamba ukitoka Loliondo hadi Narok ni kilomita 156 na umbali halisi wa kutoka Narok hadi Samunge ni kilomita 200.
“Hawa Wakenya ni watu wa ajabu sana. Wanawadanganya watu kwa sababu kila kitu kizuri kinapopatikana Tanzania wanasema ni chao. Serengeti wanasema ni yao, Kilimanjaro wanasema ni yao, kwa nini Serikali yetu haikanushi taarifa hizi?
“Mimi sielewi kwa nini Serikali yetu iko kimya. Wakenya sasa wanapata umaarufu wa Samunge wakati siyo kijiji chao. Serikali isikae kimya, ijibu kauli hizo na iwaeleze watu ukweli badala ya kuendelea kukaa kimya.
“Halafu muelewe kwamba wagonjwa wengi wanaoingia Samunge wanatoka Kenya, wengi wao siyo Wakenya bali ni wageni kutoka nchi nyingine wanaolazimika kupitia katika nchi hiyo kutokana na taarifa za uongo zinazotolewa,” alisema Telele.
Katika hatua nyingine, alisema mgonjwa mmoja kutoka nchini Malawi amemzawadia Babu gari aina ya Toyota pick up lenye namba za usajili BL 9238 baada ya kupona kupitia kikombe cha Babu.
“Nawaambia Babu yuko juu kama mkungu wa ndizi. Kuna mtu mmoja kutoka Brantyre, Malawi alifika Samunge akapata kikombe, baada ya kupona kabisa ugonjwa wake, sasa ameamua kumzawadia gari Babu,” alisema.
Akizungumzia ujenzi wa barabara ya kutoka Mto wa Mbu -Loliondo kupitia Mbuga ya wanyama ya Serengeti, mbunge huyo alisema lazima barabara hiyo ijengwe kama ilivyoainishwa katika ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Aalisema kuwa, pamoja na kwamba baadhi ya wanaharakati hawataki barabara hiyo ipitishwe katika Mbunga ya Serengeti, ujenzi wa barabara hiyo ni lazima kwa kuwa haitakuwa barabara ya kwanza kupitishwa katika mbuga za wanyama.
Katika maelezo yake, mbunge huyo liitolea mfano barabara inayotoka Dar es Salam kwenda Iringa ambayo inapitia katika Mbunga ya Wanyama ya Mikumi ingawa mbuga hiyo ina idadi kubwa ya Wanyama.
Kwa mujibu wa Telele kinachotakiwa wakati wa ujenzi wa barabara hiyo ni kuwekwa matuta kadiri itakavyowezekana ili kudhibiti mwendo mkali wa magari yanayoweza kuwagonga wanyama pindi yanapokuwa yakipita katika barabara hiyo.
“Ujenzi wa hii barabaa ni muhimu sana na wananchi wa Ngorongoro wanaihitaji sana na nafurahi kwamba iko katika Ilani ya CCM na imetengewa Sh bilioni 1.600.
“Kwa hiyo, lazima ijengwe kwa kiwango chama lami kama ilivyoelekezwa na hii hoja ya kwamba barabara haiwezi kupitishwa katika Mbunga ya wanyama hatuwezi kuikubali kwa sababu wanyama hawawezi kuwa kikwazo cha maendeleo,” alisema.
Hata hivyo, wakati mbunge huyo ana msimamo huo, Serikali imekwishapeleka barua Ufaransa kueleza kuwa kilomita 53 zinazokatiza kwenye mbunga zitabaki kuwa za changarawe na lami itaishia kwenye kingo za mbunga.

chanzo:mtanzania gazeti

NB
SISHANGAI MAANA TUMESHAZOEA KUPIGWA BAO,ACHA TUENDELEE KUPIGA USINGIZI KIDOGO TUKIJA AMKA (KAMA SI KUAMSHWA) TUTATIA AKILI

No comments:

Post a Comment