Wednesday 7 December 2011

KIKWETE AGOMA KUSAINI WARAKA WA ONGEZEKO LA POSHO

Wabunge wageukana, sasa 'kidole na jicho'

RAIS wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, anatajwa kugoma kutia saini waraka wa mapendekezo ya viwango vipya vya ongezeko la posho za “kukaa kitako” bungeni zinazolipwa kwa wabunge kutoka Sh. 70,000 za sasa hadi Sh. 200,000, Raia Mwema limeelezwa.

Habari zinasema, wakati Kikwete akigoma kusaini waraka huo wa posho, zipo taarifa kuwa malipo ya posho mpya yamekwishafanyika kinyemela kwa matarajio kuwa angesaini.

Hata hivyo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, amekana kufanya malipo hayo akisema kiasi cha ziada kilicholipwa kwa wabunge ni stahili isiyohusiana na nyongeza ya posho.

Kwa upande wake, Kikwete amegoma kutia saini waraka husika kwa mujibu wa mamlaka yake. Taratibu zilizopo ni kwamba, Rais hufikishiwa mapendekezo hayo na yeye anaweza kuidhinisha kwa kutia saini ikiwa ni kibali kinachowezesha Bunge kwenda Wizara ya Fedha kuchukua fedha hizo tayari kwa shughuli iliyokusudiwa.

Mbali na kibali hicho cha Rais kuwezesha Bunge kupewa fungu la fedha husika kutoka Hazina (Wizara ya Fedha) lakini pia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hufanya ukaguzi wa hesabu husika kwa kutumia masharti yaliyopo kwenye waraka unaotiwa saini na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya uhakika vya habari, Rais Kikwete alipelekewa waraka huo mapema na ilitarajiwa angeweza kutia saini haraka; lakini imekuwa kinyume, kielezwa kuwa ‘kelele’ za makundi mbalimbali ya jamii zimechangia kumfanya asite kutia saini kama ilivyotarajiwa.

“Huo waraka wa mapendekezo ni kweli umefikishwa kwa Rais kwa muda sasa lakini hajatia saini, ingawa anakubali posho za sasa haziwatoshi wabunge lakini pia anatambua kuwa hali ya uchumi kwa mwananchi mmoja mmoja si nzuri, na kwa hiyo, ni vema hili suala kulishughulikia kwa umakini mkubwa”, kilieleza chanzo chetu cha habari kutoka Ikulu.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa upande wa Rais, taarifa za Bunge zinaeleza kuwa mchakato wa nyongeza za posho ulipitia hatua karibu zote katika Bunge.

Hatua hizo ni pamoja na kujadiliwa na kupitishwa na Tume ya Bunge inayoundwa na makamishna ambao ni wabunge pia, Kamati ya Uongozi ya Bunge inayoundwa na wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge na mwisho, wabunge wote kupewa muhtasari husika na kujadili na kisha, kukubali au kutokubali taarifa husika.

Kwa hiyo, Raia Mwema, kupitia vyanzo vyake vya habari, limejiridhisha kuwa Bunge lilifikia uamuzi wa kuongeza posho hizo na wabunge wa kambi ya upinzani na chama tawala kwa ujumla wao, walikubali uamuzi huo.

Inaelezwa kuwa mbunge pekee mwenye msimamo mkali dhidi ya kuchukua posho ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, ambaye hata hizi posho za zamani amegoma kuzichukua kwa muda mrefu sasa.

Hata hivyo, wabunge wenzake katika chama chake wamekuwa wakichukua posho hizo na hata zile za semina mbalimbali kwa wabunge, ikiwamo semina iliyofadhiliwa na fedha kutoka Wizara ya Nishati na Madini, na kugharimu kibarua cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, David Jairo.

Mbali na uamuzi huo wa Rais kutosaini ili kuidhinisha posho mpya, kumekuwa na madai kwamba katika Bunge lililopita wabunge walilipwa posho hizo kwa viwango vipya kabla ya kuidhinishwa na kwamba kwa sasa, wanaweza kutakiwa kuzirejesha kwa njia ya makato yenye utaratibu maalumu.

Kutokana na madai hayo, Raia Mwema iliwasiliana na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila ambaye alikiri wabunge kulipwa kiwango fulani cha ziada cha fedha lakini akikanusha kuwa si nyongeza ya posho kama ilivyoelezwa.

“Si kweli wabunge wamelipwa hizo posho mpya. Hakuna aliyelipwa. Mimi nitapata wapi fedha za kuwalipa....kutoka kwenye fungu gani? Kwa sababu hadi sasa hakuna kibali chochote kilichotolewa kutoka mamlaka husika kwamba posho zimeongezwa, haya mambo yanazo taratibu zake za kisheria....si utashi wangu kusema posho imepanda na kwa hiyo niwalipe wabunge.”

“Kwa hiyo, uongozi wa Bunge hauwezi kufanya uamuzi wowote nje ya taratibu za kisheria zilizopo. Hata kama hiyo posho ingekuwa imepanda, kuna maswali mengi ya kujiuliza na kupata majibu. Je, viwango vipya vinapaswa kuanza kulipwa wakati gani, je, ni kuanzia mikutano iliyopita ya Bunge? Je, ni kuanzia mwanzo wa Bunge hili au kuanzia mikutano ijayo ya Bunge?” alisema Kashilila.

Katika hatua nyingine, Raia Mwema imebaini kuwapo kwa mawasiliano yasiyo rasmi kati ya Rais na baadhi ya wabunge, wakimshauri kutoongeza posho hizo kwa sababu kufanya hivyo ni kuzidisha pengo kati ya wenye nacho na wasio nacho katika jamii ya Watanzania, wengi wao wakiwa masikini.

“Wapo ambao wameamua kumpa ushauri Rais kwamba si wakati muafaka kutia saini waraka wa nyongeza ya posho mpya. Wanadhani kwamba kuna sababu nyingi za msingi ambazo zinahusisha hali za Watanzania wa kawaida, wakiwamo watumishi wa Serikali na kubwa zaidi, hali ya uchumi haijatulia kiasi hicho,” alieleza mmoja wa wasaidizi wa Rais Kikwete.

Kutokana na ushauri huo kwake, Rais Kikwete ananukuliwa akiwajibu kwa kusema; “Mimi ndiyo mwamuzi wa mwisho.”

Lakini wakati hali ikiwa hivyo, yapo mapendekezo mengine mbadala miongoni mwa wabunge na baadhi ya viongozi waandamizi serikalini ambao hata hivyo, wamekataa majina yao yasiandikwe gazetini kwa sasa.

Wabunge na maofisa hao wanapendekeza kuwa posho ya ‘kukaa kitako’ bungeni si lazima kuongezwa, lakini malipo kwa wabunge yanayostahili nyongeza ni malipo ya posho ya kujikimu wakiwa nje ya kituo cha kazi (per diem).

Kwa sasa wabunge hulipwa posho ya kujikimu Sh. 80,000 kwa siku. Posho nyingine ni mafuta Sh. 50,000 kila mwezi na posho ya ‘kukaa kitako’ (sitting allowance) bungeni Sh.70,000.

Wabunge na maofisa hao wanashauri nyongeza ya per diem kwa kuzingatia kuwa gharama za maisha zimepanda, ikiwamo hoteli ambazo wengi huishi wakiwa katika shughuli za Bunge Dodoma, ingawa wengine wanazo nyumba zao binafsi.

“Nadhani kama ni ongezeko la per diem sawa kwa sababu gharama za hoteli na masuala mengine zimepanda mno. Hata kama wakilipa Sh.300,000 si tatizo kwa hadhi ya mbunge ambaye huwa na nyaraka mbalimbali na kwa hiyo, ni lazima aishi sehemu ya uhakika.

“Lakini kulipana posho ya kukaa kitako tu kufikia 200,000 ni ngumu sana kueleweka kwa wananchi wetu. Ni kuzidi kujichonganisha na wananchi,” alisema mbunge mmoja katika mazunguzo yake na gazeti hili.

Uchunguzi wa Raia Mwema umebaini kuwa Rais Jakaya Kikwete kwa mara ya mwisho aliwahi kusaini waraka wa nyongeza ya posho kwa wabunge Oktoba, mwaka jana, kupitia waraka namba CAB111/338/01/83.

Waraka huo unatambulika kama waraka wa Rais kuhusu masharti ya mbunge. Hata wakati mjadala wa kususia au kutosusia posho za wabunge ulipoibuka bungeni, hususan Bunge la bajeti mwaka huu, utetezi ambao hata hivyo ni dhaifu, ulieleza kwamba, kuchukua posho ni sehemu ya masharti ya mbunge.

chanzo.raiamwema

HII MAMBO YAO YA KUZUGA ZUGA WANANCHI HII,HAPO NNA UHAKIKA HAMNA LOLOTE ANAWEKA POZI TU KESHO UTASIKIA KASHASAINI HIZO POSHO SIKU NYINGI

No comments:

Post a Comment