Friday 16 December 2011

posho za wabunge ubinafsi-pengo

AONYA BILA KATIBA MPYA UCHAGUZI MKUU 2015 UTAKUMBWA NA GHASIA, AITA USHOGA NI WENDAWAZIMU



ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amezungumzia mambo kadhaa ya kitaifa akisema, ongezeko la posho kwa viongozi wa umma ni ubinafsi na kuonya kama Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 utafanyika bila ya kuwako kwa Katiba Mpya, utagubikwa na ghasia.Pengo alitoa angalizo hilo jijini Dares Salaam jana alipokuwa akitoa ujumbe kwa taifa kuhusu Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru, Sikukuu ya Krismasi na Mwaka mpya.

Posho
Kuhusu posho, Kadinali Pengo alisema viongozi wa Serikali na umma wakiwamo wabunge, wanapaswa kuacha ubinafsi na badala yake wafanye kazi kwa kuwafikiria zaidi wananchi kuliko maslahi binafsi.

“Sisi Wakristu tunaamani kuwa, Kristu licha ya kuwa alitumwa na Mungu Baba kuja kutukomboa wanadamu alifanyika mwili na kuzaliwa katika hali ya umaskini na ufukara ili atukomboe. Viongozi wa Serikali, dini na watumishi wa umma, inatupaswa kuiga mfano huo,”alisema Pengo.

Aliongeza, “Nasisitiza hili kwa viongozi sababu hivi karibuni kumezuka mzozo kati ya wabunge na wananchi ambao wamejiongeza posho kwa madai maisha kuwa  magumu. Viongozi hatupaswi kufikiria marupurupu yetu na maslahi yetu kwanza kabla ya kuwafikiria wananchi tunaowaongoza.”

Hivi karibuni Spika wa Bunge alitangaza kwamba wabunge wameongezewa posho ya vikao kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000 kwa siku kutokana na ugumu wa maisha wakiwa Dodoma. Mbali na posho ya vikao, wabunge hupewa fedha ya kujikimu Sh80,000 na Sh50,000 ya usafiri kwa siku hivyo kuwafanya kupata Sh330,000 kwa siku.

Pengo aliwataka viongozi wa Serikali na umma kuiga mfano wa mwokozi wao, Yesu Kristu aliyesema kuwa, licha ya kuwa na nguvu za Kimungu, alipotumwa na Mungu Baba kwenda duniani kuwakomboa wanadamu, alijishusha na kuzaliwa katika mazingira ya kimasikini na ufukara ili aweze kufanikisha kazi hiyo.

Katiba na siasa
Akizungumzia Katiba Mpya, Kardinali Pengo alisema ni chombo muhimu kinachotakiwa kufanya kazi kwa umakini na kuhakikisha inapatikana kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Pengo alionya kuwa bila Katiba Mpya, taifa linaweza kuingia matatizoni kwa kuwa katiba ndio inayoelekeza wananchi kuchagua viongozi.
“Tukicheza na Katiba, taifa litaingia matatani. Hivi sasa watu wameshailalamikia Katiba iliyopo kuwa ni mbovu na wakati huo huo Rais anachaguliwa kwa mpangilio ulio kwenye Katiba na anaapa kulinda Katiba na kuitetea,”alisema Pengo na kuongeza:
“Tumeshasema Katiba iliyopo kwa sasa ni mbovu, tuchukulie suala hili “very serious (kwa uzito), tukamilishe kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, vinginevyo tutaingia matatizoni”.
Akizungumzia hali ya kisiasa, alisema hadi sasa Watanzania bado wanajifunza namna ya kuishi ndani ya mfumo wa vyama vingi vya siasa baada ya kutoka ndani ya mfumo wa chama kimoja.
Alisema jibu la kufikia kwenye siasa bora ni, kulifanyia kazi suala la Katiba, ambayo ndio itakayoamua wananchi wanataka kutawaliwa na watu wa namna gani.
“Kwa sasa bado tunaishi ndani ya mawazo na mtazamo wa chama kimoja cha siasa katika mfumo wa vyama vingi vya siasa. Ndio sababu, mawazo ya chama ndio yanayochukuliwa kama mwongozo wa Serikali. Lakini tukiweka mkazo katika Katiba, tunapaswa kutambua tunatengeneza katiba ya nchi na si ya chama kimoja,”alisema Kardinali Pengo.
Sherehe za miaka 50 ya uhuru
Kuhusu sherehe za miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Kardinali Pengo alipongeza hatua tuliyofikia akisema ni nzuri na kutaka furaha hiyo iendelee kubaki miongoni mwa Watanzania.
“Desemba 9 mwaka huu tulikuwa na Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Ujumbe wangu, tuendelee na furaha hiyo, lakini suali la kujiuliza sijui ni wangapi tulifurahia sherehe hiyo? Swali hili pia hata viongozi wanapaswa kujiuliza,”alisema.
Katika ujumbe wake huo, Pengo alisema Uhuru wa kweli hauji kwa kubahatisha bali kwa kufanyakazi.
“Mwalimu Nyerere alisema Uhuru ni Kazi. Sisi tukasema Uhuru na Kazi. Lakini ujumbe unabaki kama ulivyo, nami leo ujumbe wangu kwa Watanzania ni kutambua bila kazi hakuna maendeleo,”alisema Kardinali Pengo.
Suala la ushoga
Alipoulizwa kuhusu suala la mataifa makubwa ya Uingereza na Marekeni kutaka mataifa yanayowapa misaada kuwatambua watu wanaojihusisha na ushoga, Kadinali  Pengo alijibu kwa kifupi “Ushoga ni wendawazimu”.

Alisema Mungu alipoumba watu; mwanamke na mwanaume na kuwapa hisia, alitaka watu wazaliane na kuujaza ulimwengu. Akahoji “Huyo mwanaume kwa mwanaume au mwanamke kwa mwanamke wanakutana ili iwe nini?”

Pengo alisema wanaoshiriki ushoga wanamkosea Mungu na kusisitiza, kamwe hakutakuwa na furaha kwa mtu anayekwenda kinyume na mapenzi ya Mungu.

Elimu
Kuhusu matatizo yanayiokabili mfumo wa elimu hapa nchini, Pengo alisema suala hilo linapaswa kuangaliwa pande zote mbili za wananchi na Serikali.

Alipinga njia inayotumiwa na wanafunzi kudai haki kwa maandamano na kulazimisha mambo wanayoyataka kufuatwa na watu wengine.

“Maandamano katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliibuka kwa mara kwanza lilipoanzishwa JKT, wanafunzi katika chuo hicho waliandamana na kumpinga Mwalimu Nyerere kuwa hata kama utatulazimisha hilo tunapinga na tutakwenda huku mioyo yetu ikiwa nje ya hilo,”alisema Pengo.

Alisema siyo jambo jema kwa mtu yeyote anayedai haki kuhamaki kwa viongozi wa nchi na kusisitiza, zipo njia sahihi za kudai haki hizo.

“Iko namna ya kudai haki, miaka iliyopita kulikuwa na mgomo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,vijana walikuja kwangu kuomba msaada, nikawaambia hakuna anayepingana nanyi kudai haki zenu, lakini ninachoogopa ni tendo la baadhi yenu kutumia hata nguvu kulazimisha watu wengine kufuata mnachotaka,”alisema Pengo na Kuongeza:
“Kesho mkiwa viongozi wananchi wakikataa mnayotaka kufanyika mtalazimisha”.

Hata hivyo, alisema ni vema Serikali ikakaa chini na kuangalia madai ya wanafunzi wa vyuo vikuu na kuyafanyia kazi.Alisema kama kuna upendeleo miongoni mwa makundi yanayosoma katika vyuo hivyo, harakati za kudai haki haziwezi kunyamazishwa kwa nguvu.
Pengo alifafanua kwamba mambo yanayoweza kuchochea vurugu katika vyuo ni kitendo cha upendeleo wa utoaji haki, ikiwamo mikopo kwa wanafunzi wanaosoma katika vyuo hivyo.

“Ikiwa utamnyima mikopo mtoto masikini wa mkulima na kumpatioa mkopo mtoto wa mbunge mwenye mshahara unaoridhisha kuwa ndio anayesitahili kamwe harakati hazitazuilika hata kwa kutumia silaha,”alisema.

mwananchi

No comments:

Post a Comment