Monday 28 February 2011

MAN U YACHAPA WIGAN 4-0

Vinara wa Ligi Kuu ya soka ya England Manchester United, imezidi kujiimarisha kileleni baada ya kuwararua Wigan 4-0 na kuweka wigo wa pointi nne dhidi ya Arsenal wanaoshikilia nafasi ya pili.
Chicharito
Chicharito


Wigan walio katika tishio la kushuka daraja, mwanzoni walionesha soka safi na walipoteza nafasi kadha za kufunga lakini mlinda mlango Edwin Van der Sar, alikaa imara kuzuia mikwaju.
Javier Hernandez alifungua kitabu cha mabao baada ya kuunganisha krosi ya Nani katika dakika ya 17, huku Manchester United wakianza kushika kasi ya mchezo.
Hernandez ama Chicharito kwa mara nyingine akafunga bao la pili, kabla ya Wayne Rooney kupatiwa pasi safi ya Berbatov na kufunga bao la tatu rahisi sana na Fabio akahitimisha karamu ya mabao kwa kupachika bao la nne dakika za mwisho.
Kwa matokeo hayo Manchester United wamefikisha pointi 60 na wanajiandaa kwa mchezo na Chelsea siku ya Jumanne.
Katika mchezo mwengine Aston Villa ikicheza soka safi imeweza kuondokana na wasiwasi wa kuteremka daraja baada ya kuilaza Blackburn 4-1.
Aston Villa wakishangilia bao
Aston Villa wakishangilia bao


Mabao ya Aston Villa ambao kwa sasa wamefikisha pointi 33 wakiwa nafasi ya 12, yalifungwa na Young kwa mkwaju wa penalti, Hanley wa Blackburn aliyejifunga mwenyewe, Downing aliyefunga bao la tatu na alikuwa Young tena aliyepachika bao la nne.
Bao la kufutia machozi la Blackburn liliwekwa wavuni na Nikola Kalinic dakika ya 81.
Jermaine Beckford alifanikiwa kupata bao lake la kwanza la Ligi Kuu ya England, wakati Everton ilipojitutumua na kuwalaza Sunderland mabao 2-0.
Jermaine Beckford
Jermaine Beckford


Beckford alipachika bao hilo baada ya kupatiwa pasi na Leon Osman iliyomgonga mlinzi wa Sunderland, Titus Bramble.
Ilikuwa ni siku njema kwa Beckford ambaye katika dakika ya 39 baada ya kupewa pasi na Mikel Arteta, alipachika bao la pili na kuiwezesha Everton kusogea nafasi ya 10 wakijizolea pointi 33.
Wolves iliyokuwa inaburura mkia katika msimamo wa Ligi Kuu ya England, imefanikiwa kuondoka katika shimo la kuteremshwa daraja baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Blackpool waliokuwa wakicheza pungufu ya mchezaji mmoja baada ya Campbell kutolewa nje.
Wachezaji wa Wolves
Wachezaji wa Wolves


Mabao ya Wolves waliojinasua mkiani yaliwekwa wavuni na Jarvis dakika ya pili tu, O'Hara na Ebanks-Blake alimalizia kazi katika dakika ya 78 na dakika ya 90.
Matokeo hayo yameipandisha Wolves kutoka mkiani nafasi ya 20 hadi nafasi ya 17 wakiwa na pointi 28.

Katika mchezo mwengine Newcastle walilazimishwa kwenda sare ya 1-1 na Bolton baada ya kumpoteza Ryan Taylor aliyetolewa kwa kadi nyekundu kipindi cha pili.

Newcastle wanashikilia nafasi ya tisa wakiwa na pointi 36, huku Bolton wakijiimarisha nafasi ya saba pointi 37.

bbcswahili.

No comments:

Post a Comment