Thursday 23 August 2012

BBC Idhaa ya Kiswahili Yazindua Dira ya Dunia kupitia Star TV nchini Tanzania


 Mhariri wa BBC Idhaa ya Kiswahili,Ali Saleh (pili kulia) akizungumza wadau mbalimbali walioweza kufika kwenye hafla fupi ya Uzinduzi kipindi cha Dira ya Dunia kupitia Televishioni ya Star TV hapa nchini,ikiwa ni muendelezo wa kutanua wigo wao kwa wasikilizaji.hafla hii inafanyika hivi sasa kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Harbour View,jijini Dar es Salaam.wengine pichani kutoka Kulia ni Mtangazaji Mahiri wa Dira ya Dunia,Salim Kikeke,Hassan Mhelela na Meneja Mipango na Utafiti wa Sahara Media Group,Nathan Rwehabura.
 Meneja Mipango na Utafiti wa Sahara Media Group,Nathan Rwehabura akizungumzia ushirikiano wa Kampini yake na BBC Idhaa ya Kiswahili.
 Mtangazaji wa BBC Idhaa ya Kiswahili hapa nchini,Hassan Mhelela akizungumza machache wakati wa Uzinduzi huo.Kulia ni Mhariri wa BBC Idhaa ya Kiswahili,Ali Saleh.
Mtangazaji Mahiri wa Dira ya Dunia ya BBC,Salim Kikeke akizungumza jambo kwa msisitizo wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa Kipindi cha Dira ya Dunia kupitia televisheni ya Star TV hapa nchini.kipindi kitakachokuwa kikiruka kuanzia siku ya jumatatu mpaka ijumaa,kuanzia saa 3 usiku.
 Baadhi ya Wadau waliohudhulia uzinduzi huo wakifuatilia kwa makini taarifa mbali mbali zilizokuwa zikitolewa ukumbini hapo.

Katika mpango mkubwa wa kutanua wigo wake wa wasikilizaji na watazamaji barani Afrika, BBC imetangaza kuzindua kipindi chake cha kwanza cha habari za dunia kwa lugha ya Kiswahili kiitwacho Dira ya Dunia. Kuanzia Jumatatu Agosti 27, kituo shirika cha BBC Idhaa ya Dunia nchini Tanzania, Star TV, kitarusha kipindi cha Dira ya Dunia cha BBC Idhaa ya Kiswahili. Matangazo hayo ni ya dakika 30 yakiwapa watazamaji fursa ya kupata habari motomoto za dunia na uchambuzi yakinifu kutoka katika shirika hilo la utangazaji la kimataifa ulimwenguni.

Kipindi hicho ambacho kitakuwa kikirushwa kila Jumatatu hadi Ijumaa kitatoa chachu katika matangazo ya Star TV kwa kuwaletea watazamaji habari za kiwango cha hali ya juu kutoka katika kitovu cha habari za dunia cha BBC- Global News. Dira ya Dunia pia itawaletea watazamaji taswira na uchambuzi yakinifu kutoka kwa waandishi wa habari waliotapakaa katika nchi 48 barani Afrika, na hivyo kuleta picha halisi ya bara zima kwa watazamaji wanaozungumza Kiswahili.

Kipindi cha radio cha Dira ya Dunia ni kipindi maarufu sana kwa mamilioni ya wasikilizaji katika eneo la Afrika Mashariki na Kati na hata wasikilizaji wanaoishi nje ya eneo hilo. Kwa kuzindua kipindi cha TV chenye jina kama hilo, BBC ina imarisha zaidi matangazo yake hasa kwa kutumia waandishi wake wa habari waliobobea – watangazaji Salim Kikeke na Charles Hilary, mhariri Mariam Omar pamoja na waandishi waliopo Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Kenya, Nigeria, Rwanda, Afrika Kusini, Sudan Kusini, Tanzania, Uganda na Uingereza.

Mhariri wa BBC Idhaa ya Kiswahili, Ali Saleh anasema: “Uzinduzi wa Dira ya Dunia kupitia TV, ni kwenda na mabadiliko makubwa tunayoyashuhudia ya jinsi watu wanavyofuatilia habari barani Afrika, na pia mahitaji wa mashabiki wa BBC Ihdaa ya Kiswahili. Tunavyoarifu na kuchambua habari za eneo letu na hata duniani, iwe siasa, uchumi au utamaduni, Dira ya Dunia itatoa taswira halisi ya Afrika, tofauti na jinsi ambavyo bara hili limekuwa likiripotiwa kwa miaka mingi. Kipindi chetu kitakuwa kinashirikisha watazamaji, na pia kuzigatia misingi ya BBC ya muda mrefu ya uhuru, uhakika na bila upendeleo”

Kinara wa Dira ya Dunia, Salim Kikeke ameongeza kwa kusema: “Ni heshima kubwa na nafasi ya kipekee kuwa katika mradi huu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC wa TV. Tumepitia mengi hadi kufika hapa, na kila sekunde ya safari hiyo ilikuwa ni ya kuvutia.Ni imani yangu kuwa kipindi hiki kipya cha TV kitavutia wengi katika eneo la Afrika Mashariki na Kati.”

Uanzishaji wa Dira ya Dunia katika TV ni sehemu ya mabadiliko makubwa ya matangazo yaliyofanyika ndani ya BBC mwaka huu katika bara la Afrika, katika TV na redio. Uzinduzi huu umekuja muda mfupi baada ya kuzinduliwa kwa kipindi cha TV kwa lugha ya Kiingereza kwa Afrika, Focus on Africa, ambacho pia kinarushwa kupitia Star TV. Mwezi Julai, siku chache kabla ya kuanza kwa michuano ya Olimpiki jijini London, BBC Idhaa ya Ulimwengu ilizindua kipindi kipya cha redio, Newsday – Kipindi ambacho kimelenga zaidi wasikilizaji wa redio wa asubuhi barani Afrika.

Mhariri wa BBC wa eneo la Afrika, Solomon Mugera, naye amesema: “Miongo mingi ya utangazaji katika lugha mbalimbali barani Afrika, BBC imejenga uhusiano wa kipekee na wasikilizaji wetu wa redio, kwa kueleza ya Afrika duniani, na kuipeleka dunia barani Afrika. Kukua kwa njia za utangazaji za BBC ni ushahidi wa kuwepo kwa mizizi ya muda mrefu na ufahamu wa bara la Afrika. Tunavyoanza safari hii mpya, kwa kweli tuna hamasa kubwa hasa kwa kushirikiana na mashirika ya utangazaji yenye hadi kubwa katika eneo letu.”

Nathan Lwehabura, Meneja mipango na utafiti wa SMG Ltd, anasema: “ Ni heshima kubwa kwa Star TV kujumuisha Dira ya Dunia katika vipindi vyake vya kila siku – tunaamini kipindi hiki kitavutia watu wengi. Kipindi cha BBC cha Kiingereza kilichozinduliwa hivi karibuni kupitia Star TV, Focus on Africa, kinazidi kujipatia umaarufu mkubwa, sio tu miongoni mwa watazamaji wetu, bali pia hata miongoni mwa mashirika mengine kutokana na kuzingatia fani ya uandishi, utangazaji na ubora wa kipindi. Ni matumaini yetu kuwa ushirika kati ya BBC na Sahara Media Group utaimarisha matangazo yetu ya TV hasa tunavyoelekea katika matangazo ya kisasa ya mfumo wa digital.”

Dira ya Dunia kutoka Idhaa ya Kiswahili ya BBC itakuwa ikitangazwa Jumatatu hadi Ijumaa, saa tatu usiku kupitia Star TV nchini Tanzania. Pia matangazo hayo yatapatikana kupitia wavuti wa BBC Idhaa ya Kiswahili – bbcswahili.com.

BBC ilirusha matangazo yake ya kwanza kabisa barani Afrika zaidi ya miaka 80 iliyopita. Idadi kubwa ya wasikilizaji kwa ujumla kupitia redio na TV inaifanya BBC kuwa shirika kubwa zaidi la kimataifa la utangazaji barani Afrika.

chanzo:matukio michuzi

No comments:

Post a Comment