Thursday, 23 August 2012

Dkt. Mwakyembe Amsimamisha Kazi Mkurugenzi Mkuu wa BandariWaziri wa Uchukuzi Dkt. Harisson Mwakyembe amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari-TPA-Ndugu Ephrahim Mgawe pamoja na wasaidizi wake wawili ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili.

Wengine waliosimamishwa ni Meneja wa Mafuta ya Ndege Kurasini, Meneja wa JET na Meneja wa Oil Terminal kutokana na tuhuma za kupotea kwa mafuta na kuidanganya serikali kuhusu mafuta masafi na machafu.

Kutokana na kuwasimamisha kazi Wakurugenzi hao Dkt. Harisson Mwakyembe amemteua Injinia Madeni Kipange kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA.

Kufuatia tuhuma hizo zinazofanywa Bandarini Dkt. Mwakyembe ameunda Tume  ya watu saba kufanya uchunguzi kwa wiki mbili na kumpelekea taarifa ofisini kwake ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo zikiwemo za wizi.

Pia ameagiza kufikia Septemba Mosi mwaka huu malipo yote yafanyike benki ili kuondoa rushwa na wizi unaofanyika ndani ya Mamlaka hiyo.

Waziri Mwakyembe anachukua hatua hizo kutokana na wadai wengi sasa hawaitumii Bandari ya Dar es salaam kupitisha mizigo yao kutokana na kutokuwa na imani na watumishi wake hatua inayoifanya serikali kukosa mapato.

Pia ameagiza kusimamishwa mara moja kwa Kampuni ya Singilimo ambayo inajihusisha na kazi ya kubeba mafuta machafu na badala yake itafutwe Kampuni nyingine.

No comments:

Post a Comment