Wednesday 20 October 2010

AJALI YA AINA YAKE DAR








Sheria zinazowalinda majaji huenda zikazuia Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Projesti Rugazia, asipandishwe mahakamani kujibu shitaka la kusababisha ajali ambayo ilisababisha kifo cha mtu mmoja, kujeruhi na kuharibu mali.
Usiku wa kuamkia juzi, gari namba namba T.780 ACB aina ya Toyota Land Cruiser Prado lililokuwa likiendeshwa na Jaji Rugazia (56), mkazi wa Ada Estate Kinondoni, jijini Dar es Salaam, liliua mtu mmoja, kujeruhi watatu na kuharibu magari matano.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleimani Kova, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo juzi na kwamba gari la Jaji Rugazia lilisababisha ajali hiyo baada ya kuacha njia na kuparamia magari matano yaliyokuwa yameegeshwa kandokando ya barabara ya Ali Hassan Mwinyi maeneo ya Victoria karibu na mgahawa wa Wachina wa Zhonghua Garden.
Kova alisema ajali hiyo ilitokea saa 8:baada ya gari hilo kuacha njia na kuelekea kushoto mwa barabara na kuyagonga magari matano yaliyokuwa yameegeshwa kando kando ya barabara.
Magari yaliyogongwa na kuharibiwa kuwa ni T.776 AZK Mitsubishi Pajero, T.213 AZR Toyota Spacio, T.104 BHY Daihatsu Terios, T.395 AKU Toyota Corolla na T.312 ACB Suzuki Escudo.
Aliongeza kuwa gari la Jaji Rugazia pia liliwagonga watembea kwa miguu wanne ambao ni Salehe Omary (30), mkazi wa Msasani ambaye baadaye alifariki dunia wakati akipata matibabu katika Hospitali ya Mwananyamala na kuongeza kuwa mwili wake unahifadhiwa hospitalini hapo.
Waliojeruhiwa katika ajali hiyo kuwa ni Issa Iddi (30), mkazi wa Kinondoni, Nassibu Hassan Kiruwa (28), mkazi wa Kitunda ambao wamelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) wakipatiwa matibabu wakati mtu mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Rahma.
Kwa mujibu wa Kamanda Kova, Jaji Rugazia alifikishwa katika kituo cha polisi Oysterbay kwa ajili ya mahojiano na kwamba baada ya uchunguzi kukamilika Jaji Rugazia atachukuliwa hatua za kisheria.
Jana Kova alisema bado uchunguzi huo unaendelea na kuahidi kutoa taarifa leo.
Hata hivyo, baadhi ya wanasheria wamesema taratibu zilizoko haziruhusu jaji kushitakiwa mahakamani akiwa na wadhifa wake.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, mwanasheria mmoja (jina lake limehifadhiwa), alisema hakuna sheria inayoruhusu jaji kusimama kizimbani mbele ya hakimu.
Mwanasheria huyo alisema hakuna sheria inayoweza kutumika kumpeleka jaji kusomewa mashitaka mbele ya hakimu.
Naye mwendesha mashitaka wa Jeshi la Polisi ambaye aliomba jina lake lisiandikwe gazetini, alisema hakuna mtu aliye juu ya sheria, lakini sio rahisi jaji kusomewa mashitaka mbele ya hakimu, ambaye anamzidi kwa wadhifa.
“Labda avuliwe madaraka ya ujaji kama ilivyo kwetu sisi polisi, lakini vinginevyo haiwezekani hakimu atasikilizaje kesi ya jaji ni vigumu sana... tuache tusubiri itakavyokuwa,” alisema mwanausalama huyo wa raia nchini.
Msajili wa Mahakama ya Rufani, Francis Mutungi, hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo kutokana na kuwa safarini.
Kaimu Msajili wa Mahakama ya Rufani, John Mgeta, alipopigiwa simu na NIPASHE kuzungumzia suala hilo, simu yake ilikuwa ikiita muda mrefu bila majibu baada ya mwandishi wetu kuelezwa kuwa alikuwa na shughuli nyingi nje ya ofisi.
Jaji Mkuu, Austino Ramadhani, alikuwa safarini na katibu wake, alisema suala hilo linaweza kuzungumziwa na Msajili wa Mahakama ya Rufaa Tanzania.

SOURCE: NIPASHE

ajali magari matano,usiku saa nane judge anatoka mizungushoni,na nasikia baada ya ajali jamaa akapata zawadi ya vibao toka kwa mkewe pale pale,haya usishangae jamaa akaachiwa bila shtaka lolote.kwa bongo lolote lawezekana.

No comments:

Post a Comment