Wednesday 20 July 2011

BLAH BLAH ZA SAKATA LA RUSHWA ZINAENDELEA

Pinda: Rais amenipa maagizo mapya
 Send to a friend
Tuesday, 19 July 2011 21:26
0diggsdigg
Hoseah naye atangaza kuanza uchunguzi wa kina
Kizitto Noya na Ramadhan Semtawa






















WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda ana siri nzito kuhusu hatima ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini David Jairo baada ya jana kusema kuwa Rais Jakaya Kikwete amempa maelekezo mapya kuhusu suala hilo.

Pinda alisema hayo, baada ya gazeti hili kumtaka aeleze hatua ya kinidhamu iliyochukuliwa dhidi ya katibu mkuu huyo aliyetuhumiwa juzi bungeni kuwa aliziagiza zaidi ya taasisi 20 kuchanga Sh50milioni kila moja kwa ajili ya kufanikisha kupitishwa kwa bajeti ya wizara yake.
"Suala hilo bado tunalifanyia kazi," alisema Pinda alipotakiwa kueleza maagizo aliyopewa na Rais baada ya kuwasiliana naye juzi na jana. "Ndio niliwasiliana naye lakini, ametoa maelekezo mapya kuhusu suala hilo ambayo tunalazimika kuyafanyia kazi kwanza."

Akizungumzia suala hilo la Jairo bungeni juzi, Pinda alisema: "Kwa jinsi jambo hili lilivyokaa, hakuna jinsi mtu unavyoweza kulitetea hata kidogo, nilitamani sana kwamba nije hapa niseme kwamba uamuzi wangu mimi ni huu, lakini haikuwezekana.
Kwa dhati kabisa naomba wabunge tuwe na subira, mara tu mheshimiwa Rais atakapotua South Africa (Afrika Kusini) jioni ya leo (juzi), nitamwarifu na ninaamini tutaelewana kuhusu hatua za kuchukua."Tuhuma za rushwa katika Wizara ya Nishati na Madini ziliibuliwa juzi na Mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shellukindo alipokuwa akichangia Makadirio ya Wizara ya Nishati na Madini bungeni juzi.

Shellukindo alisema, Jairo aliziandikia barua idara na taasisi hizo akiziagiza ziweke fedha hizo kwenye akaunti namba 5051000068 inayomilikiwa na Geological Survey of Tanzania (GST) kwenye Benki ya NMB, Tawi la Dodoma."Tena inaagiza kwamba fedha hizo zikishatumwa kwenye akaunti hiyo, wizara ipewe taarifa kupitia Ofisi ya DP kwa ajili ya utaratibu," alisema Shellukindo akiinukuu barua hiyo.

Kauli ya Dk Hoseah
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imeanza uchunguzi wake juu ya madai hayo ya Wizara ya Nishati na Madini kuzichangisha taasisi zilizo chini yake fedha kwa ajili ya kufanikisha bajeti hiyo.Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah alisema jana kwamba tuhuma hizo ni nzito na tayari taasisi hiyo imeanza kuzichunguza.
Alisema taasisi yake inafanya uchunguzi kwa umakini na kwamba kila anayetuhumiwa atapewa nafasi ya kujitetea na kusisitiza kwamba ofisi yake inalichukulia suala la nishati ya nchi kwa uzito mkubwa."Tumeshaanza uchunguzi... jambo zito kama lile hadi Bunge linaahirishwa unafikiri tunaweza kuliacha hivihivi? Suala la nishati tunalichukulia ‘very serious’. Tutafanya uchunguzi wetu na tutaona matokeo baada ya kukamilika," alisema.

Lema alia na Ngeleja
Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema jana aliomba mwongozo wa Spika akitaka Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja awajibishwe kwa tuhuma za rushwa zinazoikabili wizara yake.

Mbunge huyo alitoa kauli hiyo bungeni ikiwa ni siku moja baada ya wabunge kuikwamisha Bajeti ya Wizara hiyo.
"Ni kwa nini Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja asiwajibishwe kutokana na kitendo kilichofanywa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ambaye Waziri Mkuu alimwona kuwa na makosa katika kufanya ushawishi wa kuitetea bajeti ya wizara hiyo?" Alisema.

Lema alisema haiwezekani Katibu Mkuu kutumia nafasi hiyo kwa ajili ya kuwashawishi wabunge halafu waziri mwenye dhamana asijue kinachoendelea ndani ya wizara yake na hivyo akataka na yeye awajibishwe.Hata hivyo, akijibu mwongozo huo, Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema suala hilo limeshatolewa ufafanuzi na Waziri Mkuu na kwamba mjadala huo umeshafungwa.“Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 99 (1), Waziri Mkuu ameshaomba muda na kwamba suala hilo linakwenda kushughulikiwa... naomba tuwaache wafanye kazi inayostahili, hili jambo lipo administratively (kiutawala),” alisema Makinda.

Jairo anena
Licha ya kuendelea kumiminiwa tuhuma za kuchangisha fedha katika idara zilizo chini ya wizara yake, Jairo amekataa kuzungumzia suala hilo akisema: “Niacheni.”Alisema hayo kwa simu jana akisema kwa sasa si wakati mwafaka kwake kusema chochote kuhusu tuhuma hizo:
"Kwa sasa sina majibu," alijibu kwa kifupi maoni yake kuhusu tuhuma hizo zilizoibuliwa bungeni juzi na Shellukindo.Alipoulizwa kama ana mpango wa kujiuzulu badala ya kusubiri uamuzi wa Rais alijibu: "Niache kwanza, naomba hili nalo nisijibu."


CHANZO:MWANANCHI

No comments:

Post a Comment