Friday 29 July 2011

Majibu ya samaki waliochunguzwa Arusha yatua Wizarani



Send to a friend
Thursday, 28 July 2011 21:03

Wazari wa Afya na Ustawi wa Jamii. Dk Haji Mponda

HATIMAYE Tume ya mionzi hapa nchini (TAEC) imekamilisha zoezi la uchunguzi wa samaki wanaohisiwa kuwa na sumu waliofikishwa mbele ya tume hiyo hivi karibuni huku ikisema wao wameshakamilisha agizo lililotolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Wizara hiyo ilitoa agizo hilo kupitia kwa Waziri wake, Dk Haji Mponda ambaye aliagiza samaki hao wapelekwe Arusha wakapimwe.Pia ilitoa tahadhari kwa wananchi kutokana na baadhi ya samaki hao kuanza kusambazwa sokoni.

Sakata hilo tayari limeshavuta hisia miongoni mwa wabunge katika Bunge ambapo juzi Mbunge Predensiana Kikwembe (Viti Maalumu CCM), aliitaka Serikali kulitolea tamko sakata hilo wakati akichangia hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi katika mwaka wa fedha 2011/12.

Mbunge mwingine, Abdulkarimu Shah (CCM) kutoka Mafia , katika kikao hicho cha juzi alisema kuwa ni aibu kwa Serikali kuagiza samaki kutoka nje ya nchi wakati nchi ina bahari ,maziwa na mito mingi.

Akihojiwa na Mwananchi jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Firmin Banzi alisema tayari Tume yao imeshakamilisha zoezi la uchunguzi wa samaki hao jana na tayari wameshaiwasilisha ripoti ya uchunguzi mbele ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii jana.

Alisema Tume yao ilianza uchunguzi wake mnamo Julai 26, mwaka huu, baada ya kupokea samaki hao kupitia Shirika la Ndege la Presicion ambapo waliwatayarisha na kuwapima kabla ya kuandika ripoti ya uchunguzi kamili.

"Sisi tumeshakamilisha zoezi zima la uchunguzi kama tulivyoagizwa na wizara hivyo wizara ndiyo itakuwa na nafasi nzuri ya kutoa majibu na sio sisi,"alisema Banzi.

Banzi, alibainisha ya kuwa wameituma ripoti ya uchunguzi wa samaki hao jana aa 4:00 asubuhi kwa njia ya nukushi huku akikataa kuzungumzia changamoto walizozipata wakati wakifanya uchunguzi wa samaki hao kwa madai kuwa hawataki kuharibu majibu ya uchunguzi huo.

Ofisa habari na Mawasiliano wa Wizara Nsachris Mwamwaja alipoulizwa juu ya taarifa za uchunguzi huo umefikia wapi alisema taarifa hizo anazo Katibu Mkuu wa Wizara.

Lakini juzi jioni Waziri wa Kilimo,Chakula na Ushirika, David Mathayo aliliambia Bunge kuwa ni mapema mno kuzungumzia suala hilo kwa kuwa liko katika hatua za awali za uchunguzi.

Hivi karibuni serikali ilitahadharisha kuhusu kusambazwa kwa zaidi ya kilo 1,000 za samaki wenye sumu sehemu mbalimbali za nchi na kuwataka wananchi washiriki msako iliouanzisha kuwatafuta.

Mwananchi

No comments:

Post a Comment