Joseph Mayanja ‘Chameleone’.
Na Saleh Ally
KUMEKUWA na maswali mengi sana kuhusiana na mgogoro ulioibuka kati ya
Kampuni ya Global Publishers (GPL) na msanii Joseph Mayanja
‘Chameleone’ wa Uganda ambaye anadaiwa dola 3,500 (zaidi ya Sh milioni
5) alizochukua halafu hakuzifanyia kazi.
Global iliingia mkataba na
Chameleone kupitia wakala wake aitwaye George kwa ruhusa ya Chameleone
mwenyewe. Mganda huyo alikubali GPL iingie mkataba na wakala huyo kwa
niaba yake ili aje nchini Julai 7, kutumbuiza katika Tamasha la Usiku wa
Matumaini kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Msanii Kidumu
raia wa Burundi, ndiye aliiwakilisha GPL na baada ya kuwasiliana na
Chameleone, walikutana naye akamtambulisha George. Baada ya kuingia
mkataba huo, dola 3,500 ambazo zilikuwa za utangulizi zikatolewa maana
msanii huyo alitaka dola 5,000 katika malipo yote. Baada ya hapo
maandalizi yakiwemo matangazo ya tamasha hilo yakaendelea.
Alipoanza
kuulizwa kuhusiana na kuja, Chameleone akagoma kwa madai kwamba George
hakumpa fedha! Alipoulizwa kwamba yeye ndiye alimtambulisha wakala huyo,
sasa vipi liwe tatizo la GPL? Akasisitiza haelewi lolote na hatakuja.
GPL
ilishaanza matangazo, hivyo ikaona ni vizuri kuzungumza naye upya ili
imlipe tena dola 5,000. Ajabu, safari hii akageuza bei, akasisitiza kama
wanamhitaji, wamlipe dola 8,000 (zaidi ya Shilingi milioni 12) na si
kwa advance, alitaka alipwe yote.
Kwa ajili ya kulinda heshima kwa
kuwa GPL ilishatangaza kuwa atakuwepo katika tamasha, meneja wake
Abdallah Mrisho, akafunga safari hadi Kampala na kumlipa Chameleone
kitita cha dola 8,000. Mkataba mpya ukatengenezwa, ule wa mwanzo
ukaendelea kuwepo.
Chameleone alitua nchini kwa ajili ya shoo, safari
hii GPL ikiwa imelazimika kulipa tiketi za ndege za watu watatu badala
ya wawili kama yalivyokuwa makubaliano ya mwanzo. Alipewa Range Rover
Vogue ambalo alilitumia kwa safari zake zote akiwa hapa nchini.
Alifikia
katika hoteli inayomilikiwa na GPL. Baada ya shoo, uongozi wa GPL
ulitaka kujua kuhusiana na fedha za mkataba wa kwanza ambazo Chameleone
alitoa maagizo wakala wake asaini mkataba huo halafu baadaye akaruka.
Yakatokea mabishano, naye akaondoka hotelini hata bila ya kuaga.
Kawaida
katika hoteli hiyo kumekuwa na utaratibu wa kuhifadhi pasi za kusafiria
za wageni, baada ya kutokea matatizo kadhaa na wateja kutoka nje ya
nchi. Baada ya kuondoka, siku iliyofuata Chameleone alituma mtu arudie
pasi zake akidai yeye alikuwa Zanzibar katika tamasha.
Uongozi wa
hoteli uligoma kuzitoa hadi afike mwenyewe, naye akagoma kwa madai hana
shida kwa kuwa anajua zitapelekwa. Baada ya hapo, ndiyo akarejea kwao
kufuatia kupata pasi za kusafiria kutoka ubalozi wa Uganda nchini. Mbaya
zaidi akavamia ubalozi wa Tanzania nchini Uganda na kufanya vurugu
akidai pasi zake.
Kwa kuwa uongozi wa hoteli ulikabidhi pasi ya
kusafiria ya Chameleone kwa uongozi mkuu, nao siku chache baadaye
ukazikabidhi kwa serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa.
Baada ya hapo, jambo hilo limezidi kupasua anga huku
baadhi ya watu wakionekana kulikuza bila ya kujua lolote linaloendelea.
Ili mradi wamerukia tu huku wakitangaza eti, pasi ya kusafiria ya
Chameleone ni ya kidiplomasia kwa kuwa alipewa na Rais Yoel Museven,
kitu ambacho ni uzushi mtupu tena usiokuwa na maana.
Wapo
wanaotangaza eti GPL imemtapeli Chameleone, kivipi? Wakati yeye ndiye
amefanya utapeli kupitia wakala wake George, utaratibu ambao amekuwa
akiutumia kwa watu wengine ambao amewahi kuwatapeli. Chameleone maana
yake ni kinyonga, mnyama ambaye ngozi yake inaweza kubadilika rangi
kutokana na mazingira aliyopo, ndicho anachokifanya.
Kwa nini yeye?
Jiulize mara mbili au tatu kwamba kwani ni mara
ngapi GPL imewahi kufanya kazi na wasanii wa nje bila ya kuzuka mgogoro
wowote? Hata Chameleone mwenyewe hajalalamikia malipo kutoka GPL, badala
yake kampuni ndiyo inamlalamikia yeye kwa utapeli.
Kumjua George:
GPL ingeweza vipi kufika kwa George bila ya
kutambulishwa na Chameleone mwenyewe? Yeye ndiye alimtambulisha George
kwa Kidumu aliyekuwa mwakilishi wa GPL, kwamba aingie naye mkataba kwa
kuwa ndiyo utaratibu wake anaoutumia kwa mawakala. Kama kweli George
hakumpa Chameleone fedha, vipi tatizo liwe la GPL?
Kenya v Uganda:
Rekodi zinaonyesha Chameleone hafanyi shoo Kenya
na hasa Nairobi, ikitokea akaenda huko, basi atalazimika kuwa chini ya
ulinzi mkali. Yote ni kutokana na utapeli mkubwa ambao ameufanya huko
kwa zaidi ya mara moja. Wakenya aliowatapeli, wote alitumia mfumo huohuo
wa wakala.
Angalia Wakenya namna walivyokuwa wakali na kushikilia
msimamo wa kutaka haki zao zilipwe, hapa nyumbani Watanzania wanadai
haki yao kwa Mganda huyo lakini wanaopiga vita tena kwa juhudi kubwa ni
Watanzania wenzao! Yote hiyo ni chuki, ndiyo maana wapo wanaothubutu
kunyoosha mkono kwa GPL bila hata kujua chanzo cha tatizo, yote hiyo kwa
kuwa Watanzania wengi chuki ndiyo msingi unaotuongoza!
DJ JD:
Ameibuka na kusema aliwahi kutapeliwa na Chameleone dola
3,000 (zaidi ya Sh milioni 4.5), hiyo ilikuwa mwaka 2004. Hadi leo
amekuwa akipiga chenga kumlipa na kuna wakati alimwambia aandae onyesho
aje atumbuize ili wawe wamemalizana, akafanya hivyo na kwa mara ya pili
hakutokea tena!
Wapo ambao wanaamini Chameleone hawezi kufanya
utapeli, wanaona ni mtu ‘smati’ sana. Huenda amefanya upuuzi huo sehemu
nyingi lakini hakuwahi kukutana na watu wanaojua kudai haki yao na
wasiokubali kukaa kimya kwa kuhofia kelele za watu wengi ambazo unaweza
kuzilinganisha na za chura.
JD aliwahi kumkimbiza Chameleone kama
mwizi alipokuja hapa nchini, alitaka kumtia nguvuni katika mikono ya
Jeshi la Polisi. Lakini DJ huyo anasema Merrey Balhabou na Rita Poulsen
walimuombea msamaha wakidai atamlipa, naye akaahidi hivyo, hadi leo
changa la macho. Kula fedha za bure kuna utamu wake, lakini mwisho wake
utakuwa mbaya kwake.
Biashara:
Kuna mpango, kampuni moja ambayo hufanya masuala ya
burudani, imeonyesha kufurahia sana kutokea kwa utapeli huo wa
Chameleone. Inachofanya sasa ni kulikuza suala hilo kwa nguvu zote,
kwanza ni kama faraja kwao kusikia GPL inaingia katika mgogoro kwa kuwa
wamekuwa na mafanikio makubwa katika matamasha yao ukilinganisha na wao
ambao hufanya kwa msimu maalum.
Kuna taarifa wanataka kulikuza zaidi
suala hilo ili baada ya muda Chameleone awe gumzo halafu wamlete wao
nchini kutumbuiza. Hivyo, kwa kutumia vyombo vyao na watu wa kutengeneza
katika mitandao, wamekuwa wakilikuza na kusukuma kashfa nyingi, taarifa
tunazo na nguvu ya kupambana nao hadharani na ikiwezekana mafichoni,
tunayo.
Kawaida ya Watanzania huona kila kilicho nje ya nchi ni bora
zaidi, ndiyo maana hadi leo wengi hawaamini kwamba Uwanja wa Taifa ni
mzuri na bora kuliko viwanja vingine ndani ya Afrika Mashariki na Kati.
Huenda kingekuwa Uganda au Kenya, basi wangeambiwa ni bora wangekubali.
Huo
ni utumwa wa mawazo na kuwapa nafasi wale wanaoamini wao ni bora kwa
hisia na kwa kuwa wanakuzidi kuzungumza Kingereza tu, basi unaamini
kweli wao ni bora. Tuache uwoga, hapa GPL tunaheshimu lakini hatuhofii
yeyote yule hata chembe, tena hasa unapofikia wakati wa kudai haki yetu
ambayo tunaamini tunastahili kuipata, sisi ni Watanzania.
GPL