Friday 13 July 2012

Siri Za Uchunguzi Wa Tukio La Dkt. Ulimboka Zaanza Kuvuja




Siri za uchunguzi wa awali wa tukio la kutekwa na kujeruhiwa kwa Dkt. Stephen Ulimboka zimeanza kuvunja, lakini kwa mshangao wa wanaojua kilichotokea, uchunguzi huo unatoa majibu yenye tata.

Habari za kutoka ndani ya vyombo vinavyochunguza tukio hilo, zinasema katika hatua ya awali zimeibuka na nadharia tatu juu ya kwa nini na nani aliyemteka Dkt. Ulimboka.

Nadharia hizo zinazozua utata wa hali ya juu, zinaonyesha na kutoa maelezo ya hatari, ambayo madaktari hawakubaliani nayo hata kidogo, ingawa wamekiri kuwa nao wameyasikia maelezo hayo waliyoyaita ya ‘kipuuzi’.
1. Nadharia ya kwanza inaelezwa kuwa Dk. Ulimboka alipigwa na madaktari wenzake wanaoamini kuwa alikuwa ‘amepotea njia’ na kuanza kuwauza kwa Serikali na taasisi zinazotoa fedha kufanikisha mgomo huo, “Kuna viashiria kuwa alikuwa anachukua fedha kutoka kwenye baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) na chama fulani, ambao lengo lao ni kutaka vurugu ziendelee kuwapo na nchi isitawalike. Lakini kilichotokea wanasema zile fedha alizokuwa anapewa alikuwa anawapiga panga njiani, hivyo wenzake wakaona wamshughulikie,” kilisema chanzo chetu kwa siri kubwa.
2. Nadharia nyingine ni ikle inayoelezwa kuwa wapo wagonjwa waliofiwa na ndugu yao mbele ya Dkt. Ulimboka hapo Muhimbili, na waliahidi kulipiza kisasi, hivyo hii nayo inafanyiwa uchunguzi na vyombo vya dola kubaini ukweli wake.
3. Nadharia ya tatu na ya mwisho ni ile iliyogusiwa hadi bungeni na wabunge wa CCM - akina Mwigulu Nchemba na Injinia Stella Manyanya - kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinahusika na utekaji wa Dk. Ulimboka kwa nia ya kuwafanya wananchi waichukie Serikali. CHADEMA kupitia Mkurugenzi wake wa Mawasiliano, John Mnyika, imekanusha mara moja na vikali kuhusika na unyama huu, na baada ya kubainika kuwa hoja hii ingeleta machafuko katika ukumbi wa Bunge, Spika wa Bunge Anne Makinda ameamua kuipiga marufuku isizungumzwe bungeni.

Dkt. Ulimboka, ambaye si mwajiriwa wa Serikali, anadaiwa kutekwa usiku wa kuamkia Juni 26, mwaka huu Dar es Salaam. Baada ya kupigwa na kujeruhiwa, inadaiwa kwamba alitelekezwa katika msitu wa Pande, wilayani Kinondoni jijini humo.
• Wakati utata wa tukio hilo ukiendelea kutanda, kumekuwa na taarifa nyingi, lakini zinazotajwa zaidi ni ile ya kwamba Dk. Ulimboka alifanyiwa kitendo hicho na marafiki zake wa karibu. Taarifa kutoka kwa baadhi ya vyombo vya usalama zimedokeza kuwa chanzo cha kadhia hiyo ni kujitokeza kwa mgongano wa maslahi kati yake na wenzake.
• Inaelezwa kwamba wenzake hawakufurahishwa na matumizi ya fedha na misaada mingine iliyokuwa ikitolewa na asasi zisizo za kiserikali, ambazo zimekuwa mstari wa mbele kuunga mkono mgomo wa madaktari nchini, “Jambo hili hatujalithibitisha moja kwa moja, lakini tumepata taarifa kuwa baadhi ya rafiki zake ndiyo walioshiriki kumteka kwa sababu za kimaslahi. Tunaendelea kuchunguza kujua ni maslahi gani ingawa kuna taarifa zinazodai kwamba wenzake walianza kumtilia shaka juu ya mwenendo wake na dhima aliyopewa ya kuwatetea madaktari. “Inasemekana walianza kumtilia shaka kwa ukwasi alioupata ndani ya kipindi kifupi, wenzake wakawa na imani kuwa huenda anajinufaisha na uenyekiti,” kimesema chanzo kingine.
• Kuna madai mengine kwamba tukio la kutekwa na kupigwa kwa Dkt. Ulimboka lilitokana na ndugu wa mgonjwa mmoja aliyefariki dunia kwa kukosa matibabu, bado nayo ni ya kutia shaka kubwa. Hata hivyo, daktari huyo hakuwa mwajiriwa wa serikali, ingawa inadaiwa kuwa kwa nyakati kadhaa alikuwa amepewa nafasi ya kuwahudumia wagonjwa katika Taasisi ya Mifupa (MOI). Mmoja wa wafanyakazi wa MOI aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina amesema; “Kuna ndugu walikasirika baada ya mgonjwa wao kufariki dunia. Hawakufurahishwa na majibu waliyopewa na mmoja wa madaktari (Ulimboka). Walionekana kuchukia. Siku chache baadaye ndipo ukatokea huo utekaji. Baadhi yetu tumelihusisha na kifo cha yule mgonjwa.”

Dkt. Ulimboka kwa sasa anatibiwa nje ya nchi. Taarifa za awali zilisema alipelekwa Afrika Kusini, ingawa kumekuwapo na taarifa nyingine kwamba anatibiwa katika moja ya nchi barani Ulaya.

Madaktari wenzake walikataa msaada wa Serikali wa kumpeleka nchini India kwa matibabu, jambo ambalo Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamaja, amenukuliwa akisema limeisikitisha Wizara na Serikali kwa jumla.

Pamoja na kukataa ofa ya matibabu, madaktari hao walizuia viongozi wa Serikali kwenda kumjulia hali Dk. Ulimboka alipokuwa amelezwa MOI.
• Serikali ndiyo mtuhumkiwa mkuu katika sakata la kutekwa na hatimaye kujeruhiwa kwa Dkt. Ulimboka. Maelezo yake ya awali, ya kwamba alitekwa na watu wenye silaha, yamewafanya baadhi ya watu waamini kuwa alitekwa na polisi.
• Aidha, maelezo yake mengine ya kwamba alipotekwa aliwekwa katika gari lililoelekea Barabara ya Bagamoyo, na kwamba walipofika eneo la Victoria alifunikwa uso kwa kitambaa cheusi, yameibua hisia za kuihusisha Idara ya Usalama wa Taifa. Ofisi za Usalama wa Taifa zipo jirani na eneo la Victoria, ingawa mmoja wa viongozi wao alipowasiliana na JAMHURI mwishoni mwa wiki alikanusha vikali wao kuhusika, “Wasihamishie matatizo yao kwetu. Sisi hatupo kwenye siasa zao. Hiki ni chombo huru na wala hatutaki kazi zetu kuingiziwa siasa. Na wala hatutaki kutoa jibu lolote kwenye vyombo vya habari,” alisema Afisa wa Usalama wa Taifa kwa ukali.

Viongozi wengi wa Serikali akiwamo Waziri Mkuu Mizengo Pinda, wameshatoa taarifa za kukanusha madai hayo.

Rais Jakaya Kikwete, katika hotuba yake ya kila mwezi kwa wananchi, alikanusha madai hayo na kuahidi kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vitafanya kila linalowezekana ili ukweli wa jambo hilo uweze kujulikana kwa uwazi.

Katika hotiba hiyo, Rais Kikwete alisema; “Napenda kuungana na Watanzania wenzangu wote kuelezea masikitiko yangu makubwa na kuhuzunishwa kwangu na kitendo cha kinyama alichofanyiwa Dkt. Stephen Ulimboka usiku wa Juni 26, 2012.

“Kitendo hicho ni kinyume kabisa na mila na desturi zetu. Watanzania hatujayazoea mambo hayo. Nimeelekeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli ujulikane. Nimesema kuwa ningependa ukweli huo ujulikane mapema ili tuondoe wingu baya la kutiliana shaka na kulaumiana kunakoendelea hivi sasa.

“Natambua kuwa Serikali nayo inatajwa katika orodha ya wanaotiliwa shaka. Mimi nimeshangazwa sana na hisia hizo kwani siioni sababu ya Serikali kufanya hivyo. Dkt. Ulimboka alikuwa mmoja wa viungo muhimu katika mazungumzo baina ya Serikali na madaktari. Ni kweli kwamba yeye si mtumishi wa Serikali, hivyo hakustahili kuwa sehemu ya majadiliano haya.

“Kulikuwa na rai ya kutaka asiwepo, lakini nilisema wamuache maadamu madaktari wanamwamini kuwa anaweza kuwasemea vizuri zaidi kuliko wao wenyewe walioajiriwa na Serikali.”

Madaktari wasisitiza Serikali haijinasui

Katibu wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Edwin Chitage, aliiambia JAMHURI kuwa hata yeye ameyasikia maelezo hayo kwamba madaktari ndiyo waliomteka au wanatumiwa na vyama.

“Ukweli utabaki kuwa ukweli. Tunajua waliohusika wanajitahidi kweli kweli kujiondoa katika hili, ila itakuwa ngumu. Katika hili Serikali ina kazi ya ziada kujitoa. Tangu mwanzo tumeikataa Tume iliyoundwa na tunasema tunataka uchunguzi huru,” alisema Dk. Chitage.

Alisema wao wanahitaji uchunguzi huru unaopaswa kuwahusisha majaji na kada ya watu wanaoheshimika katika jamii, kitu anachosema kitasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha imani ya wananchi katika taifa.

Dkt. Ulimboka alindwa na Interpol
Habari zilizolifikia Gazeti la JAMHURI muda mfupi kabla ya kwenda mitamboni, zilieleza kuwa Dkt. Ulimboka alikuwa akilindwa kwa karibu na polisi wa kimataifa (Interpol) kutokana na maombi yaliyofikishwa kwao na wanaharakati.

Hata hivyo, habari hizi hazikuweza kuthibitishwa mara moja, kwani waliotajwa kufanya kazi hiyo ambao ni Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Helen Kijo-Bisimba na Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Ananilea Nkya, hawakuweza kupatikana mara moja.

chanzo:jamhuri newspaper

No comments:

Post a Comment