Rais wa Liberia, Mhe. Ellen Johnson Sirleaf.
---
Rais wa Liberia, Mhe. Ellen Johnson Sirleaf, anatarajiwa kuwasili nchini tarehe 17 Julai, 2012 kwa ziara ya kikazi ya siku tatu. Ziara hiyo ya Mhe. Sirleaf inafuatia mwaliko wa Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mhe. Sirleaf ambaye atawasili siku hiyo saa 8.00 mchana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, atapokelewa na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.
Akiwa hapa nchini, Mhe. Sirleaf anatarajiwa kukutana kwa mazungumzo rasmi na Mhe. Rais Kikwete tarehe 17 Julai 2012, ikifuatiwa na Dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake na Mhe. Rais Kikwete, Ikulu, Dar es Salaam.
Aidha, Mhe. Sirleaf pia anatarajiwa kuzindua Ofisi za Mradi wa Viongozi wa Afrika wa Kudhibiti Malaria (ALMA) tarehe 18 Julai, 2012 na siku hiyo hiyo Mhe. Sirleaf atatoa Mhadhara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhusu “The Role of Women in African Development”.
Vile vile, tarehe 19 Julai, 2012 Mhe. Sirleaf atatembelea Kiwanda cha Kutengeneza Vyandarua cha A to Z kilichopo Arusha kabla ya kuondoka siku hiyo hiyo kurejea nchini kwake.
IMETOLEWA NA:
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA,
DAR ES SALAAM.
16 JULAI, 2012
No comments:
Post a Comment