Monday, 16 July 2012

Madaktari wasitisha maandamano


CHAMA cha Madaktari Tanzania (MAT), kimesitisha maandamano ya amani yaliyokuwa yafanyike kesho na badala yake wataendelea kuomba kibali kwa ajili ya wiki ijayo.
Madaktari hao juzi walitoa tamko la kufanya maandamano makubwa ya amani jijini Dar es Salaam ili kupinga dhuluma na uonevu dhidi ya taaluma muhimu ya udaktari na madaktari wenyewe.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa MAT, Dk. Rodrick Kabangila, alisema pamoja na hatua ya Jeshi la Polisi kuyapiga marufuku maandamano hayo bado wataendelea kuomba kibali kwa siku zijazo kwani ni haki ya raia.
Alidai kuwa sababu zilizotolewa na jeshi hilo ni za kisiasa kwa kuwa hoja zilizotolewa na wanataaluma hao hazina uhusiano na mgomo unaoendelea nchini.
“Hatuwezi kuandamana maana wanaweza kutudhalilisha na makoti yetu meupe ingawa jeshi hilo limetumika kisiasa …sisi tutaendelea kupigania haki zetu kwa kuomba tupewe kibali kwa siku zijazo za wiki ijayo,” alisema.
Katibu huyo alisema kuwa jeshi hilo halina sababu ya kuhofu vurugu kuibuka katika maandamano hayo kwa kuwa ina vikosi vya kutosha kuweza kukabiliana na fujo zozote.
Alisema kuwa madaktari wataendelea kupigania haki zao na kupinga unyanyasaji wanaofanyiwa na serikali likiwemo suala la kutekwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madakatri, Dk. Steven Ulimboka.
Kwa mujibu wa Dk. Kabangila, alitaja lengo la maandamano ilikuwa ni kupinga na kusikitishwa na dhuluma inayofanyiwa taaluma hiyo kwa kuzingatia uwiano duni wa madaktari hapa nchini ambapo daktari mmoja hutibu wagonjwa 30,000 kwa mwaka chini ya viwango vya kimataifa.
Alisema jumla ya madaktari 400 walio chini ya usimamizi wa madaktari bingwa, wamesitishiwa usajili wao na wengine kusimamishwa kazi bila kujali umuhimu wao kwa mustakabali wa taifa na wananchi wake.
Dk. Kabangila alisema kuwa nyingine ni kushinikiza serikali iunde tume huru kwa ajili ya kuchunguza suala la Dk. Ulimboka itakayofanya kazi haraka na wahusika wote wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
“Maandamano hayo yalipangwa kuanzia nje ya Hospitali ya Taifa Muhimbili, tutaishia kwenye geti la Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, tukiwa na mabango ya kulaani kitendo cha kutekwa, kupigwa na kutelekezwa kwenye msitu wa Pande alichofanyiwa Dk. Steven Ulimboka,” alisema.


chanzo.MTANZANIADAIMA

No comments:

Post a Comment