Monday 11 April 2011

CHUPA MPYA MVINYO WA ZAMANI

Mukama Katibu Mkuu CCM



SIKU moja baada ya Kamati Kuu ya Chama Chama Mapinduzi (CCM)na Sekretarieti kujiuzulu, taarifa zilizovuja jana
kutoka kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) mjini Dodoma zilisema kuwa Bw. Wilson Mukana ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho kushika nafasi iliyoachwa na Bw. Yusuf Makamba.

Wengine waliotajwa kuwamo kwenye sekretarieti hiyo ni Bw. Abdulahaman Kinana (Naibu Katibu Mkuu (Bara), Bw. Nape Nnauye (Katibu wa Itikadi na Uenezi), Bi. Zakia Megji (Fedha za Uchumi) na Bi. Rehema Nchimbi (Organazesheni).

Chanzo chetu ndani ya NEC kilisema kuwa wajumbe walikuwa tayari wametangaziwa uteuzi huo, lakini chanzo chetu kingine, kikadokeza kuwa pia kulikuwa na uwezekano wa kuteuliwa Jaka Mwambi, Balozi wa tanzania nchini Russia na aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM katika sekretarieti ya kwanza ya Rais Kikwete.

Bw. Mukama alikuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, kabla ya kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI na baadaye Katibu Mkuu Wizara ya Afya. Kwa sasa ni mstaafu, akiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Magazeti ya TSN.

Bw. Makamba, aliyekuwa akiongoza sekretarieti hiyo amelazimika kujiuzulu kabla ya mwaka 2012 aliokuwa ametangaza kutoka na tuhuma mbalimbali dhidi yake, zikiwamo za kukigawa chama na kushindwa kumsaidia mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete.

Kutokana na tuhuma hizo, juzi usiku, kiongozi huyo, sekretarieti nzima iliyo chini yake, pamoja na Kamati Kuu, isipokuwa Mwenyekiti na Makamu wake wawili, Bw. Pius Msekwa (Bara) na Aman Abeid Karume (Zanzibar) walilazimika kujiuzulu, katika kile kinachotajwa kama chama hicho kujivua gamba.

Wengine waliojiuzulu katika secretarieti ni manaibu makatibu wakuu wa CCM Bara na Visiwani, Bw. George Mkuchika, Bw. Saleh Ramadhan Feruzi na Katibu wa Itikadi na Uenezi, John Chiligati, Katibu wa Uchumi na Fedha, Bw. Amos Makala, Katibu wa Mipango, Bi. Kidawa Saleh na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mambo ya Nje, Bw. Bernard Membe.

Kwa maamuzi hayo, Rais Kikwete amepata fursa nyingine ya kuteua sekretarieti mpya na Kamati Kuu nyingine ikiwa ni takriban mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu wa chama hicho kufanyika mwakani, ikiwa ni njia ya kukinusuru chama hicho kilionesha kupauka mbele ya macho ya umma, kutokana na tuhuma mbalimbali, kubwa ikiwa ni kukumbatia ufisadi.

Waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu iliyoondolewa ni Bw. Makamba (Katibu Mkuu), Mkuchika - Naibu Katibu Mkuu (Bara)Salehe Ramadhan Ferouz - Naibu Katibu Mkuu (Z'bar), Dr. Ali Mohamed Shein - Mjumbe, Edward Lowassa na Shamsi Vuai Nahodha.

Pia walikuwamo marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Dkt. Salmin Amour. Wengine ni John Malecela, John Chiligati, Amos Makala, Bernard Membe, Kidawa Hamid Salehe, Samuel Sitta, Pandu Ameir Kificho na Anna Abdallah.

Wajumbe wengine ni Rostam Aziz, Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Pindi Chana, Andrew Chenge, Dkt. Maua Daftari, Samia Suluhu Hassan, Mohamed Seif Khatib, Haji Omar Kheri, Dkt. Abdallah Kigoda, Abdurahman Kinana, Anne Makinda, Fatuma Said Ali, Zakia Meghji, Omar Yussuf Mzee, Dkt. Emmanuel Nchimbi, Ali Ameir Mohamed na Yussuf Mohamed Yussuf.

Habari kutoka Dodoma zilisema kuwa kulikuwa na juhudi za wajumbe mbalimbali, hasa wanaotuhumiwa kwa ufisadi kutaka uamuzi wa kuitema sekretarieti ushindikane, lakini baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu wakawa mbogo na kutoa uamuzi huo, huku wakimweleza mwenyekiti kuwa kamati hiyo wanaiacha mikononi mwaka kwa kuwa baadhi ya wajumbe ni marafiki zake.

Kwa mujibu wa habari hizo, mmoja wa watuhumiwa hao alijitetea akitaka tuhuma za ufisadi ambazo hazijathibitishwa na mahakama yoyote zisiwe kigezo cha kufanya maamuzi hayo, kwa madai kuwa hazikuwa sabau ya kupunguza kura za CCM katika uchaguzi mkuu uliopita wala kukichafua chama.

Inasemekana kuwa kigogo huyo alijitetea kuwa hata wao (watuhumiwa) walichaguliwa kwa kura nyingi kuwa wabunmge, na Rais Kikwete alipata kura nyingi kwenye majimbo yao.

chanzo:majira

1 comment:

  1. tusubiri wanazuoni watupe ya ukweli,kama safu hii mpya itakinusuru chama,ama ndo yaleyale!

    ReplyDelete