Tuesday 19 April 2011

Usajili kwenda kwa babu wasitishwa


KUANZIA leo vituo vyote vya kuratibu safari za kwenda kupata kikombe cha Mchungaji Ambilikile Masapila wa Samunge Loliondo wilayani Ngorongoro, Arusha
vimetakiwa kutotoa ruhusa hadi wiki ijayo ili kuitikia mpango wa Babu wa kutokutoa tiba siku ya Ijumaa Kuu na Siku kuu ya Pasaka.

Wakati Serikali ikitoa agizo hilo, hali ya msongamano katika kijiji
hicho imezidi kuwa mbaya baada ya kituo cha Bunda Mkoa wa Mara kinachohudumia Kanda ya Ziwa kuvunja utaratibu na kuruhusu idadi kubwa ya wagonjwa kuingia Samunge kwa siku tatu mfululizo tangu Alhamisi iliyopita.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Isidore Shirima alisema jana kuwa kutokana na hali hiyo mwisho wa wagonjwa kusafiri kuelekea huko ni leo kwa vituo vyote licha ya kuwepo kwa msururu mrefu unaokadiriwa kufikia kilomita 25 wenye magari zaidi ya 2,000 hadi jana.

“Kwa mujibu wa taarifa ya Mchungaji Masapila hakutakuwepo na huduma ya uponyaji kituoni Samunge siku ya Ijumaa Kuu na siku ya Pasaka, hivyo kesho (leo) ni siku ya mwisho ya kuruhusu magari kuelekea huko hadi Jumatatu ijayo watakaporuhusiwa tena,” alisema Bw. Shirima.

Habari zilizopatikana kutoka vituo cha Bunda zimedai serikali wilayani humo imeshindwa kudhibiti hali hiyo wakidai kuwa wamechoka kulaumiwa na wagonjwa kuwa hawana sababu ya kuwazuia kwenda huko kwa wakati huo.

Akizungumzia hali hiyo, Bw. Shirima alisema wadau wote wa safari za Samunge ni wajibu wao kufuata taratibu walizojiweka bila kujali kulaumiwa kwani kwa kukiuka masharti utekelezaji wa tiba hiyo unakuwa mgumu.

“Hali hii ya kuongezeka kwa msongamano Samunge kunatokana na mashinikizo mbalimbali hususan kwa wasafirishaji wanaolazimisha kupitisha wagonjwa wao bila kufuata taratibu zilizowekwa na kwa kituo cha Bunda hawana budi kufuata taratibu hizo,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa kuwepo kwa wagonjwa wengi Samunge si suluhisho la kupata tiba hiyo kwa wakati kwani kinachotokea huko na uhaba wa huduma muhimu kama maji, chakula na malazi huduma ambazo wangezipata huko katika vituo vyao kabla hawajaanza safari.

Alisema kituo cha Bunda hakina sababu ya kuachia wagonjwa kuingia bila kufuata utaratibu kwani kilishapata upendeleo wa kuruhusu wagonjwa 1,000 wakati vituo vingine vikitakiwa kuruhusu wagonjwa 500 tu.

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dkt. Francis Issack akizunguzia tuhuma hizo juzi kwa njia ya simu alikanusha kituo hicho kukiuka masharti ya kuingia Samunge na kudai kuwa wagonjwa wote wamekuwa wakiruhusiwa kwa utaratibu maalumu.

majira

No comments:

Post a Comment