Tuesday 5 April 2011

NCHI YA VIKOMBE-KIKOMBE KINGINE MBARALI KWA 20,000/=


TIBA ya 'Kikombe cha Babu' imeendelea kuibuka katika mikoa mbalimbali ambapo Mkazi wa Kijiji cha Kigowe, Kata ya Mahongole wilayani Mbarali
, Bi. Rose Ngota (55) ameibuka na kudai kuwa ameoteshwa na Mungu kutibu Ukimwi kwa kutumia mzizi wa mbuyu kwa kikombe kimoja.

Akizungumza na gazeti hili jana wilayani hapa, Bi. Ngota alisema kuwa yeye ni mganga wa tiba za jadi tangu mwaka 2009 alipooteshwa, akisisitiza kuwa ilikuwa kabla ya Babu wa Loliondo ambaye amepata umaarufu kwa kudaiwa kutibu magonjwa mengi sugu.

Alisema kuwa tangu miaka ya nyuma alitoa dawa za magonjwa mbalimbali lakini mwaka 2009 alitokewa na mizimu ambayo ilimpeleka katika mti wa mbuyu na kumuonyesha kuwa mti huo ni dawa ya kutibu ukimwi.

“Mimi ningekuwa wa kwanza kuliko hata Babu wa Loliondo kwani baada ya kuoteshwa nilipuuzia na sasa ninaona kuwa mizimu hii inaniotesha kweli, hivyo nimemua kufika katika Ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Mbarali kuomba dawa ifanyiwe utafiti na wataalamu ili niweze kugawa kwa watu wanaoumwa maradhi mbalimbali," alisema.

Hata hivyo, Bibi huyo alisema kuwa baada ya kupata majibu kama dawa hiyo haina madhara kwa binadamu ataanza kutoa tiba hiyo kwa kuwapa wagonjwa kikombe kimoja cha dawa kwa gharama ya sh. 20,000 na mgonjwa kupona ndani ya siku nne.

Alibainisha kuwa alianza mwaka 2009 kwa kutibu ugonjwa wa kuwashwa mwili, tumbo la kuahirisha muda mrefu, upungufu wa nguvu za kiume pamoja na kichwa kuuma mfululizo bila kupata nafuu.

Akizungumzia gharama kubwa anayotarajia kutoza kwa wagonjwa Bibi huyo alisema dawa hiyo anaitoa mbali na yeye ni mwanamke, hawawezi kutembea umbali mrefu kwa kuwa dawa hiyo ipo porini.

Aidha alisema dawa hiyo mpaka ipimwe na wataalamu ili kujua kama ina madhara yeyote kwa binadamu ndipo aanze kutoa tiba hiyo kwa wananchi na akaongeza kuwa wananchi ambao hawatakuwa na kiasi hicho cha fedha atawasaidia kuwatibia bure.

“Hizi dawa zote nilioteshwa kwa wakati mmoja lakini ambazo nimekuwa nikitumia kutibu ni za maradhi ya tumbo, kichwa, upungufu wa nguvu za kiume na kuwashwa mwilini lakini hii ya Ukimwi mpaka ifanyiwe utafiti na wataalamu kujua kama haina  sumu kwa binadamu," alisema bibi huyo.

majira.

No comments:

Post a Comment