Wednesday 13 April 2011

KIKOMBE KINAENDELEA LOLIONDO


Wakenya 700 wanywa kikombe Loliondo

IDADI ya raia wa kigeni wanaofika Samunge kwa Mchungaji Mstaafu, Ambilikile Mwasapila kupata tiba hadi wiki hii imefikia zaidi ya watu1,000, huku raia wa Kenya wakiwa 700.

Raia hao wa kigeni, wamekuwa wakitua Samunge kwa magari na ndege za kukodi. Hivi sasa Uwanja mdogo wa Ndege wa Wasso umekuwa ukipokea kati ya ndege nne hadi tano tofauti, awali wastani uliwa ndege moja ilitua kwa wiki.

Takwimu ambazo Mwananchi Jumapili limezipata kutoka eneo la kutolea dawa hiyo kijijini Samunge zinaonyesha kuwa raia wa kigeni ambao wameishafika hapo kupata tiba hiyo wanakaribia 1,000 huku raia wa Kenya wakiendelea kuongoza.

Kwa mujibu wa takwimu zilizoanza kutunzwa Machi 18, mwaka huu na hadi juzi mchana, raia wa Kenya pekee ambao wamekishakunywa dawa kwa ilikuwa imefikia 700.

Raia wa nchi nchingine ambao wamefika katika kijiji cha Samunge na kunywa dawa idadi yao kwenye mabano ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC) watu 11, Uganda (7), Jumuiya ya Falme za Kiarabu (7), Zambia (4), Sir Lanka (3), Uholanzi (3), Afrika ya Kusini (3), Marekani (2), Rwanda (2), Finland (1), Malawi (1), Ujerumani (1), Hungary (1) na Uingereza (1).

Hata hivyo, kutokana na kazi ya kuratibu na kutunza kumbukumbu za wageni kuchelewa kuanza ikilinganishwa na kuanza kwa utoaji wa tiba hiyo mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu, upo uwezekano wa idadi ya wageni waliopata dawa hiyo kuwa kubwa zaidi kuliko takwimu zinavyoonyesha sasa.

Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ngorongoro (OCD), Listone Mponjoli, aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa wageni wote wanaoingia Samunge wanalazimika kuwa na nyaraka zote zinazokidhi matakwa ya sheria za uhamiaji na kwamba, watakaobainika kukiuka sheria hizo watachukuliwa hatua za kisheria.

Mwananchi limeshuhudia mara kadhaa magari yenye namba za kigeni, abiria wake wakitakiwa kutoa hati zao za kusafiria na zote zimekuwa zikirekodiwa katika kitabu maalumu cha Idara ya Uhamiaji.

Pia raia wa nchi nyingine ambao hufika kwa magari yenye namba za hapa nchini hulazimika kuonyesha pasi na hati zao za kusafiria na zinazowaruhusu kuishi hapa nchini.

Wagonjwa wakosa uvumilivu

Christopher Maregesi anaripoti kutoka Bunda kuwa, idadi ya wagonjwa wanaoenda Samunge kupitia kituo cha Bunda imekuwa ikiongezeka kila siku, huku kukiwa na idadi kubwa ya wageni wa kutoka nchi jirani.

Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili umebaini kuwa wageni hao wanaotokea nchi jirani za Uganda, Rwanda, DRC na Burundi hufika nchini kupitia mipakani ingawa inadaiwa kuwa baadhi yao wamekuwa wakiingia kwa njia za panya.

Uchunguzi huo unaonyesha kuwa wageni hao ambao yumkini hawana hati za kusafiria wafikapo nchini husaidiwa na marafiki wenyeji na hupanda magari yaendayo Loliondo, hupita maeneo mbalimbali bila kizuizi chochote.

Chanzo kimoja cha habari jana kililiambia Mwananchi Jumapili kuwa wafikapo nchini, wageni hao hutafuta tiketi za mabasi yaendayo kwa Babu kwa gharama yoyote, hali inayochangia kupanda kwa nauli kwa abiria wanaotumia mabasi hayo hasa kwa mikoa ya Kagera na Kigoma.

  “Hawa wakifika nchini hutafuta marafiki wa muda wanaowasaidia kutafuta magari yaendayo Loliondo kwa gharama yoyote,” kilisema chanzo hicho.

Nauli ya awali Kutoka Arusha kwenda Samunge ilikuwa kati ya Sh80,000 na 120,000, lakini baada ya kuibuka mfumuko wa wageni hao nauli hiyo kwa sasa ni kati ya Sh130,000 na 150,000.

Mwananchi Jumapili iliwashuhudia wageni
31 kutoka nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda na DRC wakiwa miongoni mwa kundi la wasafiri wanaongojea kuruhusiwa kwenda Samunge.

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Fransic Isaac alikiri kuwepo kwa wageni hao, lakini hakutaja idadi yao akisema si wote wanaojisajili.

Hata hivyo, utaratibu unaotumika sasa katika kituo hicho, dereva pekee ndiye husajiliwa na kutakiwa kutaja, jina lake, namba ya gari analoendesha na idadi ya abiria aliobeba, hali inayoweza kusababisha wageni kuingia nchini kinyemela.

Wakati hayo yakiendelea, hali bado tete kituoni hapo kutokana na msongamano wa wagonjwa.

Wananchi hao walimwomba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aingilie kati tatizo hilo na kulipati ufumbuzi ili wao wakatibiwe bila kupoteza muda.

Hadi Ijumaa saa 12.00 jioni gazeti hili lilishuhudia magari 378 yenye watu zaidi ya 10,000 yalikuwa yamesajiliwa kituoni hapo na kupiga kambi yakisubiri kupatiwa vibali kwenda Kijiji cha Samunge.

Wastani wa magari yanayoruhusiwa kuondoka kwa siku katika kituo hicho kinachohudumia mikoa yote ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani ni 16.

chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment