Friday, 6 July 2012

DK ULIMBOKA MAHUTUTI


Hali ya afya ya Dk. Steven Ulimboka ambaye anatibiwa Afrika Kusini, imebadilika ghafla na kuna habari kuwa yuko mahututi.
Habari zilizoifikia Tanzania Daima kutoka vyanzo mbalimbali vya habari ndani na nje ya nchi, zimesema kuwa Dk. Ulimboka alikuwa amepoteza fahamu, na juhudi za kuokoa maisha yake zilikuwa zikiendelea chini ya jopo la madaktari bingwa wa nchi hiyo na wale wa Tanzania.
Inadaiwa kwamba hali ya kiongozi huyo wa jumuiya ya madaktari nchini ambaye alikimbizwa nchini humo wiki iliyopita, awali ilielezwa kuwa inaendelea vema, lakini ghafla ikabadilika na kufikia kiwango cha kupoteza fahamu.
Mwandishi wa habari wa Shirika la Habari la Uingereza (BBC) alikaririwa akisema kuwa hali ya Ulimboka ilikuwa mbaya, na kwamba kulikuwa na ulinzi na usiri mkubwa kuhusiana na hali hiyo.
Jijini Dar es Salaam, mmoja wa madaktari aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina, alisema kuwa walipata taarifa za kuzidiwa kwa Dk. Ulimboka kutoka kwa ndugu yake aliyeko Afrika Kusini kwamba alikuwa yuko kwenye hali mbaya, hali iliyowachanganya mno.
Mmoja wa madaktari alikiri kupokea taarifa za kuzidiwa kwa mwenyekiti wao kutoka kwa kaka wa Dk. Ulimboka.
“Leo asubuhi baada ya kupokea taarifa za kuzidiwa kwa Dk. Ulimboka kikaitishwa kikao cha dharura cha madaktari wote tunaelekea huko,” alisema.
Hata hivyo, majira ya mchana habari zilivuma kwamba Dk. Ulimboka alikuwa amefariki, hali iliyozidi kuzusha wasiwasi mwingi miongoni mwa madaktari, viongozi wa vyama vya kijamii na wananchi wa kawaida waliokuwa wakihaha kupata ukweli wake.
Uvumi huo hata hivyo, ulikanushwa baadaye na msemaji wa Hospitali ya Muhimbili Kitengo cha Mifupa MOI Almasi Jumaa lakini akakiri kupata taarifa za kubadilika kwa hali ya mgonjwa huyo.
Huduma za matibabu MOI zasimama tena
Taarifa za kutatanisha kuhusiana na hali ya Dk. Ulimboka, zilisababisha kusitishwa kwa huduma za matibabu katika Kitengo cha Mifupa cha Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI) baada ya madaktari karibuni wote kwenda katika mkutano wa dharura kujadili tukio hilo.
Habari za kuaminika kutoka MOI, zimethibisha kuwa taarifa za kuzidiwa na hata kuzuka kwa habari nyingine kwamba Dk. Ulimboka alikuwa amefariki, ziliwachanganya kwa kiasi kikubwa madaktari hao, ambao walilazimika kusitisha huduma na kuwapangia wagonjwa tarehe nyingine za kurudi.
Kutokana na hatua hiyo ya madaktari, wagonjwa waliofika MOI baada ya kusikia kwamba huduma zimerejea, walishindwa kupata tiba badala yake waliandikishwa majina, wakalipia na kupewa tarehe ya kurudi kwa madai kwamba hakuna madaktari wa kuwahudumia.
Taarifa ya kurejea kwa madaktari hao ilitolewa juzi hospitalini hapo jana na Mwenyekiti wa Bodi ya MOI Balozi Charles Mtalemwa na kusisitiza kwamba hospitali hiyo haiko katika mgomo kwa sasa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wagonjwa waliokosa tiba, walidai kuchoshwa na usumbufu huo huku wakiwaomba madaktari hao kurejea kazini.
“Nimekuja hapa tangu saa moja kulikua na foleni; wenzetu waliowahi walionana na madaktari lakini ilipofika saa nne tukaambiwa wote tuliojiandikisha turudi Alhamisi ijayo kwa sababu madaktari wanaenda kwenye kikao,” alisema Abdallah Haji mkazi wa Kimara.
Kwa upande wake Jenipher Suka alisema inasikitisha kuona hivyo kwa sababu mama yake ambaye ni mgonjwa mkazi wa Dodoma amekuja akitegemea kupata tiba matokeo yake ameambiwa arudi tarehe 10 mwezi huu kwa kuwa hakuna madaktari kwa sasa.
“Kwa nini serikali isiseme ukweli maana tunahangaika kuja mpaka huku halafu hakuna huduma? Vyombo vya habari vimetangaza kwamba mgomo umesitishwa lakini bado wanatudanganya wananchi kwa faida ya nani?” alilalamika Jenipher.
Akizungumza kwa sharti la kutochapisha jina lake gazetini mmoja wa maofisa waandamizi wa hospitali hiyo alikiri kutokuwepo kwa huduma baada ya madaktari kupokea taarifa za kuzidiwa kwa Dk. Ulimboka.
“Unajua huduma zinazoendelea kwa sasa ni kliniki na upasuaji kwa waliowahi lakini hawa madaktari wamechanganyikiwa baada ya daktari mwenzao aliyeongozana na Dk. Ulimboka kuwaeleza kwamba hali ya mgonjwa ni mbaya mno.
Kukosekana kwa huduma kulichangiwa na madaktari wanafunzi ambao hupokea na kuwahudumia wagonjwa kuwa katika maandalizi ya mitihani ya mwisho wa mwaka itakayoanza Jumatatu ya Julai 9, 2012 hivyo kusababisha huduma utoaji wa huduma kutokuwepo kabisa.
Pinda abanwa
MJINI Dodoma, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ameshindwa kuliambia Bunge endapo serikali iko tayari kuunda tume huru kuchunguza tukio la kutekwa na kupigwa kwa Dk. Ulimboka.
Waziri Mkuu Pinda, alishindwa kutoa kauli wakati akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe (CHADEMA).
Katika swali lake la nyongeza, Mbowe alisema kumekuwa na ongezeko la vitendo vya mauaji yanayodaiwa kufanywa na Jeshi la Polisi.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alitolea mfano wa tukio la kupigwa kwa wabunge wawili wa CHADEMA mkoani Mwanza na tukio la hivi karibuni la kutekwa na kupingwa kwa Dk. Ulimboka.
“Kwa kuwa kumekuwa na ongezeko la matukio ya mauaji kwa raia wasio na hatia na kumekuwa na hisia kwamba matendo hayo yanafanywa na Jeshi la Polisi. Mfano wa matukio hayo ni pamoja na lile la kupigwa kwa wabunge wawili na hili la hivi karibuni la kutekwa kwa Dk. Ulimboka, tukio ambalo limelichafua taifa; je, serikali iko tayari kuunda tume huru kuchunguza matukio hayo?” alihoji Mbowe.
Akijibu swali hilo, Pinda kwanza alisema sio kweli kwamba tukio la kupigwa kwa Dk. Ulimboka limechafua sifa nzuri ya taifa.
“Mh. Mbowe, kwanza tukio la Ulimboka sio mfano mzuri sana kwa sababu hakuna mwenye ushahidi wa serikali kuhusika kumteka na kumpiga Dk. Ulimboka.
“Kama nilivyosema awali, sioni sababu ya serikali kuhusika na kipigo cha Ulimboka ambaye tulikuwa tukishirikiana naye vizuri kwenye vikao vya majadiliano,” alisema Pinda.
Hata hivyo katika kujibu swali hilo, Pinda hakusema chochote kuhusu swali la Mbowe aliloitaka serikali kuunda tume huru kuchunguzwa tukio la Dk. Ulimboka.
Badala yake alisisitiza kuwa serikali itafanya uchunguzi wa kina kubaini waliohusika kumipiga Dk. Ulimboka.
Akijibu swali la msingi la Mbowe aliyehoji utekelezaji wa sheria ya uchunguzi wa vifo vyenye utata, Waziri Mkuu Pinda alikiri kuwa mwaka jana aliahidi Bungeni kwamba serikali ingelikuja na sheria ya uchunguzi wa vifo vyenye utata ili kuharakisha matokeo ya uchunguzi huo.
Alisema serikali bado inaendelea na mchakato wa kuandaa sheria hiyo ili ianze kutumika.
Mbowe alisema kumekuwa na kasi ya ongezeko la vifo vyenye utata vya raia wasio na hatia na vyombo vya dola, hasa polisi wamekuwa wakihusishwa na vifo hivyo.
Alisema kuwa Waziri Mkuu Pinda alikiri kuwapo na hali hiyo na kuahidi kuwa serikali ingekuja na sheria ya kuchunguza vifo vya aina hiyo.
Ulimboka alitekwa na watu wasiojulikana, kupigwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili, kisha kutupwa katika msitu wa Pande, nje kidogo ya jiji Dar es Salaam.
Jeshi la Polisi limeunda jopo kuchunguza tukio la utekaji nyara na shambulio la kudhuru mwili wa Dk. Ulimboka.
Tangu kuibuka kwa tukio hilo, wabunge mbalimbali kwa nyakati tofauti wamekuwa wakiibua hoja ya mgomo wa madaktari na kipigo cha Ulimboka, lakini kiti cha Spika kimekuwa kikizima kwa hoja kuwa jambo hilo liko mahakamani

chanzo:mtanzania daima.


No comments:

Post a Comment